Vyakula vyote unavyoweza kuvitengeneza kwa haraka, na kula kwa haraka siyo vyakula vizuri kiafya.
Mwendo wa haraka siyo mwendo salama kiafya.
Njia ya haraka ya kufikia mafanikio huwa haileti mafanikio ya kudumu.
Suluhisho la haraka la matatizo yetu huwa linatengeneza matatizo makubwa zaidi baadaye.
Majibu ya haraka kwenye swali lolote huwa siyo majibu bora na wakati mwingine huharibu kabisa hali ya mambo.
Lakini cha kushangaza, tunaishi kwenye dunia ya haraka, ambapo kila kitu kinatakiwa kwenda haraka, kula haraka, fanya haraka na jibu haraka.
Haraka inatuletea msongo wa mawazo kwa sababu tuna vitu vingi vya kufanya lakini muda tulionao ni mchache. Hivyo badala ya kupunguza vile ambavyo siyo muhimu, tunakazana kupitia vyote kwa haraka, tunachoka na wakati huo tunakosa kile muhimu ambacho tulikuwa tunataka.
Usikubali kudanganywa na dunia na kuingia kwenye mchezo huu wa haraka, jipe muda wa kufanya kile ambacho ni muhimu kwako. Na unapoona kuna dalili za haraka, jiulize kama haraka hiyo ina matunda mazuri au siyo mazuri.
Haraka pekee unayotakiwa kuikubali ni ile haraka ya dharura, nyingine zote, kama hakuna dharura, epuka haraka. Fanya kilicho muhimu na siyo kinachowezekana kwa haraka.
SOMA; Badilika au potea; aina mpya ya ushindani kwenye biashara.
TAMKO LANGU;
Ninajua ya kwamba vile vitu ambavyo ni vya haraka mwisho huwa havina majibu mazuri. Haraka pekee ninayohitaji kuizingatia ni pale ambapo kuna dharura. Hizi haraka nyingine nitaachana nazo na nitafanya kile ambacho ni muhimu kwako na kitaniletea matokeo bora.
NENO LA LEO.
Tunaishi kwenye dunia ambayo inathamini haraka kuliko matokeo bora.
Kuna vyakula vya haraka, mwendo wa haraka, maamuzi ya haraka na hata kujifunza kwa haraka.
Lakini matokeo ya haraka huwa siyo matokeo bora, labda kwa dharura pekee.
Epuka mkumbo huu wa haraka na fanya kile ambacho unajua ni muhimu na kitakuletea matokeo bora. Haraka huwa haina matokeo mazuri.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.