Uhuru ndiyo kitu ambacho tunakipigania na kukitafuta, kwa sababu uhuru kwenye maisha ndiyo unaotuwezesha kuishi yale maisha ya ndoto yetu, ambayo ni bora na yenye furaha.
Kwa bahati mbaya sana kwenye jamii zetu, uhuru umewekwa pamoja na fedha. Kwamba kama unataka kuwa huru basi unahitaji kuwa na fedha nyingi, tafuta fedha na zitakuweka huru. Lakini hii siyo kweli mara zote.
Ukweli ni kwamba fedha inakuletea uhuru wa kuchagua, kadiri unavyokuwa na fedha nyingi ndivyo unavyokuwa na uwezo wa kuchagua kile ambacho unakitaka. Kama huna fedha basi na nguvu yako ya kuchagua unaipoteza, badala yake unachukua chochote ambacho unaweza kukipata.
Uhuru wa maisha mara nyingi hautokani na fedha, bali unaanza na sisi wenyewe. Kwa mfano mtu anaweza kuwa na fedha nyingi sana, lakini ameajiriwa sehemu ambayo inamnyima uhuru wake, anafanya vitu ambavyo hapendelei kufanya. Mtu huyu hawezi kuondoka kwenye ajira hiyo kwa sababu anahofia kipato chake hakitakuwa cha uhakika tena. Mtu huyu licha ya fedha alizonazo, hana uhuru. Au mtu anaweza kuwa na fedha nyingi ambazo amejipatia kwa shughuli zake za kujiajiri lakini akawa mtumwa wa fedha zile, akashindwa kufanya mambo mengine muhimu kwenye maisha yake kwa kuogopa kuzipoteza, akajawa na hofu kwamba kama zikipotea maisha yake yatakuwa ya hovyo sana, hapa napo mtu hana uhuru.
Na kitu kimoja ambacho naona kinawapotosha wengi ni pale wanapoanza na kutafuta fedha wakijua ya kwamba zitawaletea uhuru wa maisha. Hapa ndipo wanapoingia kwenye mtego ambao wanashindwa kunasua.
Kuanza kinyume na hii ndiyo inaweza kuwa bora zaidi, badala ya kuanza na fedha ndiyo upate uhuru, hebu tuanze na uhuru na uhuru huu utatuletea fedha ambazo zitatufanya tuwe huru zaidi. Ule msingi ambao tunautengeneza tangu mwanzo ndiyo unaamua maisha yetu ya baadaye yaweje. Kwenye swala la uhuru wa maisha, tuanze na uhuru kwa kufanya kile ambacho tunajua ni muhimu kwetu na kutoyashikisha maisha yetu kwenye kitu chochote. Usijiambie kwamba siwezi kuishi bila kitu fulani au mtu fulani. Jua ya kwamba chochote kitakachotokea kwenye maisha yako, wewe pekee ndiyo una nguvu ya kufanya maamuzi. Tumia nguvu hii kufanya maamuzi sahihi ambayo yatakufanya uendelee kuwa huru.
TUPO PAMOJA.
SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.