Mteja yeyote anayekuja kununua kwenye biashara yako kwa mara ya kwanza anakuwa na hofu kama kweli kile unachotaka kumuuzia kitamsaidia, au kitakuwa na sifa ambazo unazisema. Anachukua hatari kubwa sana kununua kwa mtu ambaye hamjui kabisa.
Mtu yeyote anayekuajiri kwa mara ya kwanza anakuwa na hofu kama kweli utaweza kutimiza majukumu yako, ana hofu kama utakuwa hazina kwenye kazi au utakuwa mzigo. Mwajiri huyu anachukua hatari kubwa kuingia mkataba na wewe wa kukuajiri wakati hajakujua vizuri.
Watu unaojaribu kuwashawishi wakubaliane na wewe kwenye kile unachotaka wafanye au unachotaka wakusaidie wanachukua hatari kubwa ya kukubaliana na wewe hasa inapokuwa mara ya kwanza. Wanakuwa na hofu kama kweli utatimiza kile unachosema au wataishia kupoteza muda wao na fedha zao.
Mazingira ya sasa yamekuwa magumu kwa watu kuwa na uhakika kwa chochote wanachoambiwa kwa sababu kuna wengi ambao wanaahidi lakini hawatekelezi. Kuna wafanyabiashara wengi ambao wanaahidi bidhaa au huduma zao ni bora na zitamsaidia mteja lakini matokeo yanakuwa tofauti na mteja alivyotegemea.
Kuna watu wengi wanaotafuta kazi, ambao wapo tayari kusema na kuahidi chochote ili tu wapate kazi hizo, lakini baada ya kuzipata wanakuwa mzigo kwenye kazi zao.
Hali hizi zimewafanya watu kuwa na wasiwasi na waangalifu zaidi, kutokukubali haraka kile ambacho wanaambiwa na watu ambao hawawajui. Hili limekuwa kikwazo kwa wengi kupata kile ambacho wanakitaka.
Je tunawezaje kuvuka hili? Tunawezaje kuwauzia watu kwa mara ya kwanza kwa kuwaondoa wasiwasi? Je tunawezaje kuwaaminisha watu kwamba tunaweza kazi wanayotaka kutupa?
Hakuna njia nyingine zaidi ya kujenga uaminifu kwenye kila jambo unalofanya, hata kama ni dogo kiasi gani. Fanya kila kitu kwa uaminifu wa hali ya juu, hata kama ni kitu kidogo unaahidi, kitimize. Watu wataliona hilo na watawaambia wengine kuhusu wewe. Na kama ni kwenye biashara waambie wale wateja ambao tayari wanakuamini watoe taarifa zako kwa watu wao wa karibu. Kama ni kwenye ajira muombe mwajiri wako akupe barua ya mapendekezo ale unapotaka kuondoka kwenye kazi hiyo.
Kadiri unavyokuwa mwaminifu, na unavyotimiza kile unachoahidi, watu wengi watapenda kufanya biashara na kazi na wewe. Itawasaidia kuondokana na hofu ya kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi kwao.
Kocha.