Maisha ni kama mchezo, kuna ambao wapo uwanjani wanacheza na kuna ambao wapo pembeni kuangalia wengine wakicheza. Kuna ambao wanafanya biashara na kuna ambao wanawaangalia wengine wakifanya biashara na kusema siku moja na mimi nitafanya. Kuna ambao wanaweka juhudi kubwa kwenye kazi zao na kupata matokeo bora na kuna ambao wamekaa pembeni na kusema hata mimi nitakuja kufanya hivyo. Wanaofanikiwa ni wale ambao wanaingia kucheza na siyo kukaa pembeni na kuangalia wengine wakicheza.
Ila kabla hujaingia kucheza kuna vitu vitatu unatakiwa kuvijua ili uweze kucheza vyema na kupata matokeo bora.
Kwanza jua sheria za mchezo. Kila mchezo una sheria zake, kila kitu unachofanya kwenye maisha kina taratibu zake. Kuna namna ambavyo ukifanya unapata matokeo mazuri na kuna namna ambavyo ukifanya unapata matokeo mabaya. Ni muhimu ujue hayo kabla hujaanza kufanya ili usipoteze muda wako kwa kufanya mambo ambayo hayana faida kwako.
Pili jua manufaa utakayopata. Ni lazima ujue mapema kabla hata hujaanza ni manufaa yapi utayapata kwenye kile ambacho unakwenda kufanya. Usianze tu kufanya ukifikiria mbele ya safari utajua. Jua kabisa tangu mwanzo ni kitu gani unategemea kupata na hapa utafanya kazi kuhakikisha unakipata. Na unapoangalia manufaa pia angalia ni juhudi kiasi gani unahitaji kuweka, bila ya kusahau changamoto ambazo utakutana nazo katika kufikia kile unachotaka.
Tatu jua wakati wa kuacha na kusonga mbele. Japokuwa unaweza kuwa na maandalizi mazuri sana kabla hujaanza kufanya kitu, bado huwezi kujua kila kitu kabla ya kuanza. Unaweza kuanza kufanya na ukakutana na changamoto ambazo hukutegemea, au kupata matokeo ambayo hukutaka kupata. Hapa ndipo pagumu kwa sababu unahitaji kujua je uendelee kung’ang’ana au uache na kufanya kingine. Ni lazima kabla hujaingia kwenye jambo lolote, uainishe awali kwamba ni wakati gani utakuwa sahihi kwako kuacha, ili usiwe njia panda pale mambo yanapokuwa hayaendi kama ulivyotegemea. Kwa kujua vigezo vya kuacha utajua ni wakati upi wa kung’ang’ana na upi wa kuacha na kusonga mbele.
Jua sheria hizi tatu za mchezo wowote ambazo unahitaji kuzitumia kwenye kila jambo unalofanya kwenye maisha yako. Kuanzia kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla. Na hata kama utaamua kuzivunja sheria hizi, basi zivunje ukiwa umeshazijua, maana hapo utakuwa na njia bora zaidi. Usiingie kwenye kitu chochote bila ya kujua mambo hayo matatu muhimu.
TUPO PAMOJA.
KOCHA.