Fedha, fedha, fedha, leo imepata nafasi kwenye falsafa yetu mpya kwa sababu ni moja ya vitu vinavyogusa maisha yetu moja kwa moja. Ni moja ya vitu muhimu sana kwenye maisha yetu baada ya hewa tunayovuta. Hii ni kwa sababu kila kitu kinapimwa thamani kwa fedha, chochote tunachotaka, tunaweza kukipata kwa kubadilishana na fedha.

Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu, nina imani uko vizuri na unaendelea kuishi kwa misingi ya falsafa ambayo tunajijengea. Najua mpaka sasa unaongoza maisha yako kwa falsafa kwa sababu unajua maisha yasiyo na falsafa ni maisha ambayo hayana maana kuyaishi. Na nguzo kuu ya falsafa yetu mpya ya maisha ni UPENDO, upendo kwetu binafsi, upendo kwa wanaotuzunguka na upendo kwa kile ambacho tunakifanya. Tukishakuwa na upendo wa kweli, kila kitu kitakwenda vizuri.

Karibu kwenye makala yetu nyingine ya falsafa mpya ya maisha ambapo tutaangalia moja ya maeneo muhimu kwenye maisha yetu ambayo ni fedha. Fedha ni muhimu kwenye maisha yetu, lakini pia fedha imekuwa chanzo cha kuharibu maisha yetu. Hii inatokana na wengi kutokujua kwa kina ni kiasi gani cha fedha wanahitaji ili maisha yao kuwa bora. Hivyo wanayatesa maisha yao, wanakiuka misingi yao katika kuhakikisha wanapata fedha, halafu wakishazipata ndiyo wanagundua kwamba wamepoteza maisha yao ya thamani kwa kitu ambacho hakileti thamani kubwa kwao.

Kupitia makala hii tutaangalia kwa undani kuhusu fedha, na uhusiano wake na mafanikio, furaha na maisha bora.

Je fedha ndiyo chanzo cha furaha?

Swali la kwanza na la msingi sana tunaloweza kuanza nalo leo ni kama fedha ndiyo chanzo cha furaha kwenye maisha yetu. Hili linaleta mkanganyiko kwa wengi na wengi kupoteza maisha yao wakiamini baada ya kupata fedha basi watakuwa na furaha. Cha kushangaza fedha wanazipata lakini bado wanaona kuna upweke fulani kwenye maisha yao. Kwa kuwa hawajajifunza wanakazana tena kupata fedha zaidi na hii inaleta upweke zaidi. Kabla hawajajua wanajikuta kwenye mzunguko wa kutafuta fedha zaidi kila mara huku wakishindwa kufurahia maisha yao.

Kuhusu fedha na furaha, kuna mpaka tafiti zimefanywa na zimeonesha wazi kwamba fedha inaweza kuongeza furaha kwenye maisha mpaka kufikia kiwango fulani. Baada ya hapo hakuna tena furaha inayoongezeka hata fedha zingeongezeka kiasi gani.

Kwa mfano kwa mtu ambaye hana fedha kabia, au ana fedha kidogo ambazo hazimtoshelezi kupata mahitaji yake ya kila siku, kama chakula, malazi, usafiri na kadhalika, akipata fedha ambazo zinampa mahitaji haya muhimu anakuwa na furaha. Kama unakula mara moja kwa siku, tena unakula ugali tembele kwa sababu huna uwezo wa kula chakula kizuri, ukipata fedha za kukuwezesha kula mara tatu kwa siku, na kula chochote unachotaka utakuwa na furaha. Lakini ukishakuwa na uhakika wa kula vizuri, kulala vizuri, kupata kile unachokitaka na kwa wakati unaotaka, hata fedha zinapoongezeka zaidi haziongezi furaha kwako.

Hivyo tunaweza kuhitimisha kwamba fedha siyo chanzo kikuu cha furaha kwenye makisha yetu, kwa sababu mtu akishakuwa na uhakika, fedha zaidi hazina tena mchango kwenye maisha yake.

Je ni kiwango gani cha fedha ambacho unahitaji ili kuwa na maisha bora na yenye furaha?

Hapa ndipo swali kuu la kifalsafa lilipo na pia kuna utata. Kwa sababu kama mtu hujajua ni nini unataka kwenye maisha, hakuna kiwango cha fedha kitakachokutosha. Kabla ya kujua ni kiasi gani cha fedha tunahitaji, ni vyema tukajua kwanza ni aina gani ya maisha tunataka.

Kuna yale maisha ambayo ni ya msingi, ambapo mtu unapata kile ambacho ni muhimu na unakihitaji ili maisha yako yaweze kwenda vizuri. Halafu kuna yale maisha ya anasa ambapo mtu anataka kupata vitu ili kuonekana na wengine. Ili kuonekana na yeye anakwenda na wakati au kuonekana ana uwezo.

Yale mahitaji ya msingi ni rahisi na yanawezekana kupatikana kwa kila mtu. Lakini mahitaji ya anasa ni magumu na kuyapata mtu anasumbuka sana. Kwa sababu kununua vitu kwa sababu vinakwenda na wakati au unataka uonekane na wewe upo utalazimika kuendelea kufanya hivyo kila mara hata kama huhitaji kile unachonunua.

Katika kujijengea falsafa yetu mpya ya maisha, tunakwenda kujenga maisha yetu kwenye yale mahitaji ya msingi. Yale mahitaji ambayo tunahitaji kweli ili maisha yetu yaweze kwenda vizuri na siyo ili kuonekana na wengine kwamba na sisi tuna vitu fulani.

Na ili kupata mahitaji haya, huhitaji kutumia sehemu kubwa ya fedha zako katika kufanikisha maisha yako. Na hivyo hii inakupa uhuru mkubwa hata kama kipato chako siyo kikubwa. Kwa sababu ukishatimiza yale mahitaji yako ya msingi, unakuwa na nafasi ya kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako.

Hivyo kiwango cha fedha ambacho mtu unahitaji ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio ni kile kiwango ambacho kitakuwezesha kuwa na mahitaji yako ya msingi kwenye maisha. Unahitaji kuwa na uhakika wa kupata chakula, kupata malazi bora kwa kadiri unavyotaka, kupata mavazi ya kusitiri mwili wako na kuwa na uwezo wa kukamilisha shughuli zako kama zinahitaji wewe kusafiri. Baada ya hapo unahitaji kuweka juhudi zako kwenye kufanya makubwa zaidi kuliko kuteswa na matumizi yasiyo ya msingi kwako.

Falsafa hii haimaanishi uwe masikini.

Baadhi ya falsafa na hata dini zimekuwa zinahubiri umasikini, kwamba huhitaji mengi ili kuwa na maisha bora, hapo wapo sawa, ila pale wanasisitiza kwamba mtu asiwe na umiliki wowote wa mali, hapo ndipo wanapokosea. Hii ni kwa sababu hakuna tatizo la wewe kumiliki mali kama mali hizo hazijakumiliki wewe.

Unapojua mahitaji yako ya msingi ni yapi na kuyatimiza, fedha zako zinazobaki unaweza kuwekeza kwenye maeneo ambayo yataongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine. Hapa unaweza kuanzisha biashara ambapo utawapa watu mahitaji yao na hata kuajiri watu wengine. Au ukawekeza kwenye kilimo ambapo ukachangia kupatikana kwa mazao na pia kuajiri watu wanaofanya kazi.

Kwa falsafa hii tunajenga kitu kimoja ambacho ni muhimu sana kwa uhuru wa maisha yetu. Tunajijengea uhuru wa kifedha kwa kuacha kuwa watumwa wa matumizi ambayo siyo ya msingi kwetu. Na wakati huo kutumia fedha zetu katika kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine, na huku tukiendelea kufaidika zaidi.

Tunahitaji kuwa matajiri siyo ili tuonekane na wengine kwa maisha ya kifahari tutakayoishi, bali ili tuweze kuongeza thamani kwa wengine na kuwa na mchango chanya kwenye maisha ya wengine. Kwa sababu siku utakayokuwa unavuta pumzi yako ya mwisho hutakumbuka ni magari mangapi ya kifahari uliyomiliki, bali utakumbuka ni maisha ya watu gani ambayo umeyagusa. Utakapoondoka hapa duniani watu hawatakukumbuka kwa maisha ya anasa uliyokuwa nayo, bali watakukumbuka kwa mchango uliokuwa unatoa kwenye maisha ya wengine.

Watu wote wanaokumbukwa hawakumbukwi kwa fedha zao, bali wanakumbukwa kwa mchango waliotoa kwenye maisha ya wengine. Ni wakati sasa wa kudai uhuru wetu kutoka kwenye fedha ili tuweze kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine.

Mahitaji ya msingi ni rahisi kuyapata na yanafanya maisha yetu kuwa bora. Mahitaji ya anasa ni magumu kuyapata na yanafanya maisha yetu kuwa hovyo zaidi. Chagua mahitaji ya msingi na peleka nguvu zako kwenye kufanya kile ambacho kitakuwa na mchango kwenye maisha ya wengine.

Nakutakia kila la kheri kwenye maisha haya ya falsafa mpya ya maisha.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz