Asili ya maisha ni kwamba kuna kupata na kukosa, hii ni kwa kila mtu licha ya kuwa yupo wapi au ana wadhifa gani.
Hakuna mtu ambaye anapata kile anachokitaka kwa wakati anaotaka na kwa kiwango anachotaka mara zote.
Unaweza kupanga vizuri na kuweka juhudi lakini usipate kabisa kile ambacho unakitaka. Au ukakipata lakini ikawa siyo kwa kile kiwango ambacho ulikuwa unataka kupata. Au ukapata kwa kiwango ulichotaka ila ukawa umechelewa, yaani usipate kwa wakati ambao ulipanga kupata.
Hivi ndivyo maisha yalivyo, hakuna ambaye ana uhakika kwa asilimia 100 kwa chochote anachotaka kufanya.
Ni rahisi kuona kama wale ambao wana mafanikio wanaweza kupata chochote ambacho wanakitaka, siyo kweli. Kuna vitu vingi ambavyo wanavitaka na hawavipati, au wakivipata siyo kama walivyotaka.
Pia kuna vitu ambavyo haviwezi kwenda pamoja, kwa kupata kimoja unapoteza kingine. Kwa mfano kwa kuajiriwa unaweza kupata uhakika wa kipato, lakini ukakosa uhuru wa maisha yako. Au kwa kujiajiri unaweza kuwa na uhuru na maisha yako lakini ukakosa uhakika wa kipato, kila siku ukawa na wasiwasi ikiwa utaendelea kupata wateja wa kutosha kukidhi gharama zako na kubaki na faida.
Ndivyo maisha yalivyo, hakuna anayeweza kupingana na sheria hii ya asili, hata akiweza ni kwa muda mfupi, baadaye mambo yataenda kama yanavyokwenda, na inaweza kuleta hasara kubwa sana kwa mtu huyo. Kwa mfano mtu ambaye hakubali kwamba kuna kukosa, na hivyo kutumia njia ambazo siyo sahihi kupata, kama kuiba, atapata kwa sasa, lakini baadaye itamletea matatizo makubwa.
Kwa nini ni muhimu sana ujue na kuzingatia hizi:
Kwa sababu utakosa mengi ambayo utapanga kupata, hivyo usikate tamaa, jua ni sehemu ya maisha na kuna wakati utapata, endelea kuweka juhudi.
Kwa sababu unahitaji kutenganisha furaha yako na kile ambacho unakitaka. Watu wengi wamekuwa wakijiambia kwamba wakipata kile wanachotaka watafurahi sana. Sasa hii ni hatari sana kwa sababu siyo mara zote utapata unachotaka na hivyo utajikuta unakosa furaha mara nyingi. Furaha haipaswi kutoka kwenye vitu bali ndani yako mwenyewe.
Kuna wakati utapata na kuna wakati utakosa, jua hilo na lisikusumbue kwenye maisha yako. Muhimu ni kujua ni kipi unataka na njia ipi ya kufikia, weka juhudi kukipata na usikate tamaa pale inapotokea hupati kama unavyotaka.
Uwe na wakati mwema rafiki.
Kocha.
SOMA; UKURASA WA 294; Unachotaka Kwako, Taka Na Kwa Wengine.