Moja ya tabia zetu binadamu ni kuhakikisha tunakwenda sawa na maamuzi yetu, yaani yale maamuzi ambayo tunayafanya, tunahakikisha tunaweza kuyatetea na yanaendana na sisi.

Kuna rafiki yangu mmoja alikuwa ananieleza ni jinsi gani kumiliki gari binafsi siyo muhimu kwake. Kwamba ni kutumia fedha ambazo hazina malipo kwake. Alinielewa kwa mifano na kupiga mahesabu ni jinsi gani gharama za kuwa na gari binafsi zilivyo kubwa na haitamsaidia kufikia malengo yake. Baada ya muda alinunua gari binafsi na tulipokutana tena alinieleza ni jinsi gani kumiliki gari binafsi kuna faida kwake. Na alitumia hesabu zile zile ambazo alitumia awali kuonesha kwamba gari binafsi halina msaada ila wakati huu alizigeuza na zikaonesha gari binafsi ni muhimu sana.

Sisi binadamu huwa tunatafuta njia ya kutetea kile ambacho tunakifanya. Na huwa tunapata njia ya kufanya hivyo. Na wakati mwingine tunaweza kutetea kitu hata kama awali tulikuwa tunakikataa.

Huu ndiyo upendeleo ambao kila mmoja wetu anao. Tunapendelea kusifia kile ambacho tunakifanya. Tunapendelea kuona kwamba ndiyo kitu sahihi kwetu kufanya na tunatafuta sababu hata kama siyo za msingi za kuunga mkono kile ambacho tunakifanya.

Tabia hii ya upendeleo mara nyingi inatuzuia kuuona ukweli wa mambo kwenye mambo mengi yanayotuzunguka kwenye maisha yetu. Kwa sababu sisi tumeshachagua kile ambacho tunaona ni sahihi na kwa kuwa tupo tayari kukitetea basi tunaondoa nafasi ya kufikiria vingine ambavyo vinaweza kuwa bora zaidi.

Kwa sababu tumeshachagua kufanya kazi fulani, tunajishawishi hii ndiyo kazi bora kwetu kufanya na hivyo tunajinyima fursa ya kufanya kazi nyingine bora zaidi.

Kwa sababu umeshaamua kufanya biashara fulani, unajishawishi hiyo ndiyo biashara pekee kwako unayoweza kufanya, na kujipa sababu za kutetea hilo. Hii inakuzuia kuweza kuona fursa nyingine nzuri za kibiashara.

Tuvue miwani hii ya upendeleo na tuone kila kitu kama kilivyo. Tuone vitu bila ya kuvihukumu na tuwe tayari kujifunza kupitia kila kitu. Kwa njia hii tutaziona fursa nyingi na pia tutajifunza mengi zaidi.

TUPO PAMOJA,

KOCHA.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kinachotuzuia Kuujua Ukweli.