Kitu kimoja unachotakiwa kujua kwenye kupata fedha ni kwamba fedha zinakuja na gharama. Yaani hupati tu fedha hivi hivi, bali kuna kitu lazima utoe au upoteze ndiyo uweze kupata fedha. Iwe ni kwenye ajira au biashara, unatoa kitu ambacho unacho na unapata malipo kwa kutoa kitu hiko.
Katika utoaji huu ndipo masikini na matajiri wanapotofautiana sana. Na tofauti hii inaanza na utayari wa kutoa na kujua unatoa nini.
Utayari wa kutoa.
Matajiri wote wanajua ya kwamba hakuna kitu cha bure, wanajua kama wanataka kupata fedha basi lazima kuna kitu wanatakiwa watoe. Na wanakijua kitu hiko ni nini na wanakuwa tayari kukitoa kwa moyo wao wote. Kwa upande wa masikini hawapo tayari kutoa, wana mawazo yao kwamba kuna njia rahisi ya kupata fedha. Na hivyo utawakuta wakipoteza muda wao kucheza kamari, au kusubiri mtu aje awasaidie.
Wakati masikini wanapoteza muda kutafuta njia ya mkato ya kupata fedha, matajiri wanatoa kile wanachotakiwa kutoa ili kupata fedha. Baada ya muda watu hawa wawili wanakuwa tofauti kabisa, hata kama wana uwezo sawa na wameanzia pamoja.
Kujua kwamba unatakiwa kutoa kitu chenye thamani ili kupata fedha, na kuwa tayari kutoa kitu hiko, ni msingi wa kwanza wa kufikia utajiri.
Unatoa nini?
Tofauti nyingine kati ya masikini na matajiri ni kwenye kile ambacho wapo tayari kutoa. Matajiri wapo tayari kutoa thamani ambayo wanaitengeneza, lakini hawapo tayari kutoa maisha yao kwa ajili ya fedha. Wanajua ya kwamba maisha yao yana thamani kubwa kuliko fedha, hivyo wanahakikisha maisha yao yanakuwa katika hali nzuri. Kwa upende mwingine masikini wanapokuja kustuka kwamba wanatakiwa kutoa ndipo wapate, na wanapokuwa hawana namna nyingine, wanakuwa tayari kutoa na wanatoa chochote. Wapo tayari hata kutoa maisha yao ili wapate fedha na hapa ndipo wanapofanya maamuzi mabovu yanayowafanya waendelee kubaki kwenye umasikini. Wanajikuta kwenye hali ngumu zaidi na hivyo maisha yako kuwa magumu mno.
Jua kwamba unatakiwa kutoa thamani kwa wengine ndiyo uweze kupata fedha. Pia jua ni kipi hutakiwi kutoa, usiharibu maisha yako kwa ajili ya kupata fedha, maisha yana thamani kubwa kuliko fedha, ukipoteza fedha unaweza kuzipata tena, ukipoteza maisha ndiyo imetoka.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Biashara Kubwa Kwa Kuanzia Chini Kabisa, Hata Kama Huna Kitu.