Karibu tena rafiki yangu kwenye kipengele chetu hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufikia malengo makubwa tuliyojiwekea kwenye maisha yetu. Kama ambavyo wote tunajua, changamoto zipo na zitaendelea kuwepo na hivyo tunachohitaji siyo mbinu za kuzikwepa changamoto bali kuweza kuzitatua na kupata matokeo bora kabisa.
Leo katika kipengele hiki tutakwenda kuiangalia changamoto ya kukosa uthubutu wa kuingia kwenye biashara. Watu wengi wamekuwa wanapenda kuingia kwenye biashara lakini wanapojaribu wanakutana na changamoto ambazo zinawaletea hasara. Hii inawafanya washindwe kuendelea na biashara zao na wasithubutu tena kwa wakati mwingine.

Wapo watu wengine ambao waliwaamini watu waliowashawishi waanze nao biashara lakini wakaambulia kupata hasara. Wapo wengine walioanzisha biashara na kuwapa watu wao wa karibu wazisimamie lakini wakaishia kupata hasara. Biashara zimekuwa na changamoto nyingi na hivyo kuwafanya wengi wakose uthubutu wa kuingia.
Je kuna njia yoyote inayoweza kumwondolea mtu hali hii ya kukosa uthubutu w akuingia kwenye biashara na akaweza kuingia kwenye biashara itakayomfikisha kwenye ubilionea? Hiki ndicho tunachokwenda kujadili kwenye makala yetu ya leo. Tafadhali twende pamoja ili tuweze kujifunza na kuchukua hatua.

FOLORUNSHO ALAKIJA, Bilionea wa Kinigeria.

Kabla hatujaangalia kwa undani unawezaje kuondokana na hali ya kukosa uthubutu, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia akitaka ushauri juu ya changamoto hii;

Changamoto yangu ni kushindwa kuthubutu licha ya kuwa na mtaji. Kuogopa kupoteza hela Sijajua ni shughuli gani itaniletea kipato kikubwa kwa muda mfupi japo nimeshaona kilimo cha vitunguu natarajia kujaribu. Ushauri wa biashara gani nzuri isiyohitaji usimamizi wa karibu sana kwani nimeajiriwa na kipato changu cha ajira hakiniridhishi kabisa lakini naogopa kutoka kwa sababu sijaona kazi itakayonipa kipato cha kutosha na kuwa tajiri mkubwa kama Folorunso Alakija (mama wa Kinigeria bilionea namkubali sana kwa kweli ninatamani siku moja nami niwe Mwanamke bilionea tokea Tanzania) Naomba msaada wako.
Fatuma M.

Habari Fatuma,
Pole sana kwa changamoto unayopitia ya kukosa uthubutu wa kuingia kwenye biashara, licha ya kuwa na mtaji. Hii ni hali ambayo imekuwa inawakuta watu wengi na imewazuia wengi kuweza kufikia malengo yao makubwa ya uhuru wa kifedha.
Fatuma hongera kwa malengo makubwa uliyonayo ya kibiashara, hasa kwa mtu wa mfano uliyenaye ambaye ni mwanamke wa pili kwa utajiri Afrika na wa tatu kwa utajiri duniani kwa wanawake wenye asili ya Afrika. Hii inaonesha ni jinsi gani una ndoto kubwa na umeshawaona ambao wamefikia ndoto kama zako na unataka kujifunza kutoka kwao.
Kutokana na maelezo yako uliyotoa kama yanavyoonekana hapo juu kuna mambo muhimu napenda kukushauri ili uweze kuondokana na hali ya kukosa uthubutu, uweze kuanzisha biashara na kuweza kufikia mafanikio makubwa ya kuwa bilionea. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

Uthubutu ni kufanya.
Huwezi kupata uthubutu wa kibiashara kwa kusoma au kusikiliza wengine, unapata uthubutu kwa kufanya. Pamoja na mambo mazuri utakayojifunza kuhusu biashara, pamoja na mifano mizuri utakayoipata kwa wengine, bado hayo yote hayawezi kukujengea uthubutu. Uthubutu unatokana na kufanya.
Biashara ni mwalimu mzuri sana, kwa sababu katika biashara utapata nafasi ya kujifunza mambo mengi. Biashara hazikosi changamoto hata kama ungeingia ukiwa na maandalizi makubwa kiasi gani.

Unachohitaji kufanya ni kuanza biashara, na anza kidogo kwa lengo la kujifunza. Haijalishi una ndoto kubwa kiasi gani, wala haijalishi una mtaji mwingi kiasi gani, unapoingia kwenye biashara kuna changamoto utakutana nazo na nyingi zitakuingiza kwenye hasara. Hivyo anza kidogo kwa lengo la kujifunza, na unapokutana na changamoto usikimbie, badala yake itatue na jifunze kupitia changamoto hiyo.
Njia ya uhakika kabisa ya kutokupoteza fedha kwenye biashara ni kutokuingia kabisa kwenye biashara. Biashara zote kuna wakati zinapoteza fedha, hasa mwanzoni mwa biashara, hivyo kama unataka kuingia kwenye biashara ni vyema ukaondokana na hofu hii. Unahitaji kujua kwamba kupoteza fedha kwenye biashara ndiyo somo kuu la biashara, usihofu hili bali jua ndiyo njia ya kujifunza. Hata biashara kubwa ambazo zimekuwepo miaka na miaka siyo kwamba zinatengeneza faida kila wakati, kuna wakati zinapoteza fedha.

Biashara yenye faida kubwa ndani ya muda mfupi.
Fatuma, moja ya vitu ulivyoomba kushauri ni biashara gani unayoweza kufanya ambayo itakuletea faida kubwa ndani ya muda mfupi. Naomba nisikupotezee muda wowote hapa, jibu ni kwamba hakuna biashara halali ambayo inaweza kukuletea faida kubwa ndani ya muda mfupi, haipo. Na kuwa makini sana usidanganyike kwa hili, tena usiwaambie watu unatafuta biashara ya aina hiyo, maana hapo ndipo watakapopatumia kukupoteza na wao kunufaika. Siku zote watu wanaotapeliwa ni wale ambao wanataka makubwa kwa haraka.
Biashara zote zina changamoto, biashara zote zinahitaji muda ili kuweza kukua. Jua hilo na jiandae, hakuna njia ya mkato.

Kufanya biashara au kujaribu.
Hongera kwa kupata wazo la kuingia kwenye kilimo cha vitunguu, ila pia umesema unataka kujaribu. Hapa naomba nikupe tahadhari moja, kujaribu ni kitu kibaya sana kwenye biashara, kwa sababu utajaribu mara nyingi kwenye vitu tofauti na hutapata unachotaka.
Amua kuingia kwenye biashara fulani na ipe kila kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako, usijaribu bali fanya. Unapojaribu kitu maana yake kuna vitu ambavyo huweki, sasa ukijumlisha na changamoto zilizopo kwenye biashara yoyote, kujaribu ni kupoteza muda wako.
Licha ya hadithi nzuri ulizosikia kuhusu vitunguu, mara ya kwanza utakapolima hutapata matokeo uliyotarajia kupata, huenda hata mara ya pili pia usipate, labda hata mara ya tatu. Huu ni wakati wa kujifunza. Hivyo kama unajaribu, ile mara ya kwanza tu inakutosha kukata tamaa na kuacha, lakini kama umechagua kufanya, ukifika mara ya tatu utakuwa na utaalamu wa kutosha kuhusu vitunguu.
Usijaribu biashara, chagua kufanya biashara.

Kuendesha biashara ukiwa bado umeajiriwa.
Ni kweli kama ulivyosema huwezi kuondoka kwenye ajira mara moja na kwenda kwenye biashara ikiwa bado hujajua ni biashara gani inaweza kukutengenezea kipato cha kuweza kuendesha maisha yako. na pia ni kweli kabisa ya kwamba kuendesha biashara ukiwa bado umeajiriwa ni changamoto kubwa, wengi wamepata hasara kubwa na kushindwa kabisa kuendesha na kukuza biashara zao.

Nimeandika kitabu kinaitwa BIASHARA NDANI YA AJIRA, jinsi ya kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa. Ndani ya kitabu hiki utajifunza matumizi bora ya muda wako, usimamizi mzuri wa biashara yako na aina za biashara unazoweza kuanza ukiwa bado umeajiriwa. Pia nimegusia mifereji nane ya kipato ambayo unaweza kuitengeneza ukiwa bado umeajiriwa. Nashauri sana usome kitabu hiki, kuna mengi ya kujifunza. Kitabu hiki kipo katika nakala tete (pdf) na unaweza kukisomea kwenye simu au komyuta. Kinatumwa kwa email na gharama yake ni tsh elfu kumi. Kupata kitabu hiki tuma fedha tsh elfu kumi kwa mpesa 0755 953 887 au tigo pesa 0717 396 253 (majina Amani Makirita) kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu.
Soma kitabu hiko, ni mwongozo wa biashara kwa kila mtu, walioajiriwa na hata wale ambao wamejiajiri kwenye biashara zao, utapata mbinu za kuwa na usimamizi mzuri kwenye biashara yako.

Jifunze kutoka kwa ROLE MODEL wako.
Kitu cha mwisho nitakachokwenda kugusia kwenye ushauri huu ni kuhusu mtu uliyemchagua kuwa wa mfano kwako (role model) ambaye ni mwanamama Folorunso Alakija ambaye ni raia wa Nigeria. Kulingana na takwimu za Forbes, jarida maarufu kwa kufuatilia matajiri duniani, mwanamama huyu ana utajiri wa dola bilioni 1.75 (sawa na tsh trilioni 3 na zaidi), anashika nafasi ya 1121 duniani na nafasi ya 13 barani Afrika huku akishika nafasi ya 4 nchini Nigeria. Utajiri wake unatokana na biashara zake yeye mwenyewe. Ni mwanamke wa 80 kwa ushawishi duniani.

Umechagua mtu mzuri sana wa mfano kwako, ni mwanamke na ni mwafrika. Swali kubwa ninalopenda kukuuliza hapa ni je umeshamfuatilia mtu huyu kwa karibu, je unajifunza kutokana na maisha yake aliyopitia na anayofanya kwa sasa? Au unafurahia kumwangalia kwa nje pekee. Uzuri ni kwamba huna haja ya kuwa karibu naye ndiyo ujifunze, kuna mtandao wa intaneti na pia kuna vitabu ambavyo amenadika yeye kama yeye. Nakushauri ujifunze kuhusu yeye, soma taarifa zake, soma vitabu alivyoandika na jua ni jinsi gani ameweza kufika pale alipofika sasa. Ukisoma kwenye tovuti yake mwenyewe anaandika kwamba alikuwa ameajiriwa kwenye kazi za uongozi, baadaye benki na aliamua kuacha na kujiajiri mwenyewe. Alianza biashara yake ya kwanza mwaka 1983, na hakuanza akiwa bilionea, amepita miaka kama 20 kwenye biashara mbili ndiyo akaja kuwa bilionea. Hivi ni vichache lakini kuna mengi sana ya kujifunza kupitia mtu huyu. Jifunze na fanyia kazi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.