Mambo makubwa sana yangefanyika kwenye jamii zetu na dunia kwa ujumla kama tusingejali sifa zinakwenda kwa nani. Kama tungekuwa tayari kujitoa kufanya ile sehemu yetu, bila ya kujali nani anapewa sifa, tungefanya makubwa sana.
Lakini hali haipo hivyo, wengi wetu tunaangalia kama kuna sifa ambazo tutapata kwa kufanya kitu fulani. Tunaangalia kama tunaonekana na wengine kwenye kile ambacho tunakifanya ili watusifie kuwa tunafanya vizuri.
Wakati mwingine watu wanapoona watu hawajajua kama wao ndiyo wamefanya basi huamua kujisifia wao wenyewe, kwa kuwasisitizia watu kwamba mimi ndiyo nimefanya hiki au kile.
Hakuna ubaya wowote kwenye kutaka sifa au kujisifia, kama unafanya mambo mazuri unastahili kupata sifa na pongezi pia. Ubaya upo pale ambapo mtu anashindwa kufanya jambo kwa sababu hakuna wa kumpa sifa, au kwa sababu sifa zinakwenda kwa mtu mwingine. Hapa ndipo tunapoharibu mambo mengi na kujikuta tunashindwa kushirikiana na wengine.
Ni muhimu tujikumbushe ya kwamba asili ya dunia ni ushirikiano bila ya kujali nani anapata sifa. Kila siku unakula wali ambao umetokana na mpunga, unasifia wali ni mtamu lakini hujawahi kusifia majani ya mpunga ambayo yalitengeneza wali huo, kutokana na jua na hewa ya kaboni. Kila siku unafurahia kula mboga za majani ambazo zinafanya afya yako kuwa bora zaidi, lakini hujawahi kusifia mizizi ya mboga hizo ambayo ilinyonya maji na madini ardhini ili kuwezesha mboga hizo kustawi.
Tunahitaji kufanya kile tunachofanya, siyo kwa sababu tutapata sifa kutoka kwa wengine, ila kwa sababu ndiyo kitu ambacho tumechagua kufanya, ndiyo kitu ambacho ni muhimu zaidi kwetu na tukifanye kwa juhudi zetu zote.
Kama unataka sifa huna haja ya kuzipigania kwa kuhakikisha unafanya kile ambacho utasifiwa, au unafanya pale ambapo unaonekana. Sifa zinakuja zenyewe kama utaweka juhudi kwenye chochote ambacho umechagua kufanya. Hata kama hupati sifa kwa sasa, jua kuna wengi wanaona, na mara zote matendo yana sauti kubwa kuliko maneno.
Tekeleza sehemu yako, bila ya kujali unasifiwa au la, na mafanikio yatakuwa yako daima. Usiwe mtu wa kuendeshwa na sifa na mambo mengine ya nje, bali kuwa mtu wa kufuata kile ambacho ni muhimu kwako na kina mchango mkubwa kwako na kwa wengine. Hii ndiyo nguzo kuu ya maisha ya mafanikio na furaha.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA;