UCHAMBUZI WA KITABU; The Seven Lost Secretes Of Success (Siri Saba Za Mafanikio Ambazo Wengi Hawazitumii).

Linapokuja swala la mafanikio wapo watu wachache wanaofanikiwa sana kwenye kila wanachofanya na pia wapo wengi ambao wanashindwa kufanikiwa. Na hawa wanaoshindwa siyo kwamba hawapendi kufanikiwa, wanapenda sana ila kuna vitu wanakosa, ambavyo wale wanaofanikiwa wanavyo.

Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa siyo vitu vikubwa, bali vitu vidogo vidogo ambavyo watu wengi hawapo tayari kuvifanya na hivyo vinakuwa kama siri. Lakini kiukweli hakuna siri yoyote. Mwandishi Joe Vitale ameyaangalia maisha ya mtu ambaye aliwahi kufikia mafanikio makubwa sana katika uandishi na uandaaji wa matangazo huko marekani aliyeitwa Bruce Barton. Kupitia bwana Bruce, Joe ameweza kugundua siri saba ambazo zilimwezesha Bruce kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa kwenye maisha yake. Na ametushirikisha mambo hayo kwenye kitabu chake ambacho tunakwenda kukichambua leo. Karibu sana tujifunze kwa pamoja.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA PICHA AU MAANDISHI HAYA.


1. Biashara ndiyo mwalimu bora sana duniani. Biashara inakuwezesha kufanya maamuzi ya hatari, kuziendea ndoto kubwa, kukabiliana na hofu, kudhibiti hisia zako na hata kuweza kuenda na watu wasumbufu na kujifunza jinsi ya kupangilia mambo yako. kama unataka kupata funzo halisi la maisha, anzisha biashara, hakuna kitu ambacho biashara haitakufundisha. Kila siku kwenye biashara ni siku ya kujifunza, kupitia changamoto na mafanikio unayopata.

2. Dunia ya sasa watu tumekuwa tunabebwa na upepo wa nini kipya badala ya kuangalia kipi kinafanya kazi. Ndiyo maana kinapokuja kitu kipya watu wengi wanakikimbilia wakifikiri ndiyo fursa kubwa, na hapo wanaacha vile vitu ambavyo vimeshajidhibitishia kwamba vinaleta matokeo bora. Usikubali kubebwa na upepo huu w akukimbilia kila kitu kipya, badala yake jua ni matokeo gani unataka na vitu gani vitakupatia matokeo yale.

3. Mteja ndiye mfalme kwenye biashara yako. Mteja ndiyo anakuwezesha wewe kula, ndiye anayelipia gharama zako zote za maisha, ndiye anayekuwezesha wewe kufikia ndoto zako kubwa. Huyu ni mtu unayepaswa kumjali sana kwenye biashara yako, kuhakikisha anapata huduma ambazo ni bora kulingana na mahitaji yake.
Kama umeajiriwa, bosi au mwajiri wako ndiyo mteja wako mkuu. Jua namna ya kutoa huduma bora kwa mteja huyu.

4. Mteja hawezi kujua wewe unauza nini kama hutamwambia, na kumwambia mara moja haitoshi, unahitaji kumwambia tena na tena na tena. Mteja wako lazima ajue kwamba upo na atajua kama utaendelea kumwambia upo, huku ukimwambia ni kwa namna gani unaweza kumtatulia matatizo yake. Hapa ndipo kuitangaza biashara yako kunapokuwa muhimu sana kwako na kwa biashara yako. Kwa sababu ni kupitia matangazo ndiyo wateja watajua upo na unawezaje kuwasaidia.

5. Kila siku wateja wapya wanazaliwa, na wateja wa zamani wanakufa. Kila siku kuna watoto wanazaliwa, watoto wanakuwa vijana, vijana wanakuwa watu wazima na watu wazima wanazeeka. Haijalishi biashara yako inalenga wateja wa aina gani, wateja wako hawabaki vile vile, wanabadilika kila siku na hivyo unahitaji kubadilika pia na kuweza kuwafikia wale watu wapya ambao wanafaa kuwa wateja wako. Kuitangaza biashara yako kila mara ni njia mojawapo ya kuweza kuwafikia wateja wapya mara zote.

SOMA; Ijue sababu hii kubwa iliyopo nyuma ya biashara yako itakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

6. Demokrasia ya kweli ipo kwenye biashara, ambapo mteja ana uhuru wa kweli wa kuamua kuchagua ni mtu gani afanye naye biashara. Sasa hivi kuna watu wengi wanaofanya biashara zinazofanana, na hivyo mteja halazimiki kununua kwa mtu mmoja pekee, bali ana uhuru wa kuchagua wapi anunue kwa zile huduma anazopata. Hivyo kila siku wewe kama mfanyabiashara unauza sera zako na mteja anachagua anunue kwa nani. Kwenye demokrasia hii hakuna kuhonga, bali ni lazima utimize ulichomwahidi mteja, kushindwa kutimiza wala hahangaiki kukusikiliza tena, anakwenda kwa mwingine.

7. Watu wana mahitaji haya saba ya msingi sana, ambayo wanayapigania kila siku ili wayapate. Mahitaji hayo ni usalama, mapenzi/ngono, mamlaka, kuishi milele, utajiri, furaha na uhuru. Angalia biashara yako inamwezesha mteja wako kupaya hitaji lipi la msingi katika mahitaji hayo.

8. Biashara ni hadithi na wale ambao wanaweza kutengeneza hadithi nzuri kuhusu biashara zao ndio wanaofanikiwa sana kwenye biashara hizo. Watu hawanunui tu kwa sababu unauza, bali wananunua ile hadithi iliyopo nyuma ya biashara yako. kwa mfano mtu anaweza kuuziwa soda mtaani kwa shilingi elfu moja, na soda hiyo hiyo akauziwa kwenye hoteli ya kifahari kwa shilingi elfu tano. Atanunua bila ya kulalamika kwa sababu kuna hadithi ya kuelezea gharama hiyo kubwa, ameinywa kwenye hoteli ya kifahari.
Ni hadithi gani ambayo ipo nyuma ya biashara yako?

9. Mafanikio ya biashara bado yanabaki kwenye misingi mikuu ambayo ni kupenda kile unachouza, kukiamini kwamba kinaweza kuwasaidia watu na kuwa mwaminifu. Haijalishi unauza mkaa au unauza magari, misingi hiyo ya biashara ni muhimu. Bila misingi hiyo hata uwe na wazo bora kiasi gani, hata uwe na mtaji mkubwa kiasi gani, hutaweza kudumu kwenye biashara kwa muda mrefu.
Badala ya kupoteza muda kufikiria ni wazo lipi la biashara litakutoa, angalia ni kitu gani unachokipenda kweli, na unaamini kinaweza kuwasaidia watu na tafuta wanaokihitaji na wapatie. Jenga uaminifu na wale unaoanza nao na utajenga biashara kubwa.

10. Kitu pekee kitakachowafanya wateja waendelee kuja kwako ni uaminifu wako. Kumbuka mtaja anapokutana na wewe kwa mara ya kwanza hakujui na hana uhakika ya kwamba utampatia kweli kile ambacho uliahidi kumpatia. Anaposikia kwa wengine wakisifia kwamba wamepata huduma bora kwako, atashawishika kununua na kama utampa huduma bora atakuwa mteja mzuri na atawaambia wengine wengi zaidi.
Linda sana uaminifu wako kwenye biashara, hiki ndiyo kitu pekee kinachokuweka kwenye biashara, ukikiharibu huna tena biashara.

11. Unapochagua kuingia kwenye biashara, hakikisha unaipa biashara hiyo kila kilicho ndani yako. usiingie kwenye biashara kwa kujaribu, utapoteza muda wako. Ingia kwenye biashara ukijua ya kwamba una kitu ambacho kinakwenda kubadili maisha ya wengine na kuyafanya kuwa bora zaidi. Weka juhudi zako zote kuhakikisha unafikia lengo lako hilo, kwa njia hii hakuna kitu kinachoweza kukuzuia.

12. Faida ni zao la huduma bora unazotoa kwa wateja wako. Kabla hujawa na wasiwasi kuhusu faida, kuwa na wasiwasi kama kweli unatoa huduma bora kwa wateja wako. Jiulize kama unatoa thamani kwa wateja wako, kama wateja wako watakukosa iwapo utaondoka leo. Kwa kuwa na wasiwasi kwenye hilo utaweka juhudi zaidi, hapa utatoa huduma bora na faida lazima utaipata. Kinachowaponza wengi ni kufikiria faida pekee bila ya kuangalia mchango wanaotoa kwa wateja wao na hivyo kujikuta wanakosa wateja kwa kutoa huduma mbovu.

13. Binadamu ni viumbe wa mantiki na hisia, wanasukumwa na hisia kufanya maamuzi na wakati huo pia wanatumia mantiki kupata maana ya vitu. Ili kujenga mahusiano mazuri na wateja wako, tumia vyote viwili, mantiki na hisia. Watu wanapenda kujua sababu ya vitu kwa nini vipo kama vilivyo. Kwa mfano nikikuambia kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu gharama ni laki moja, unaweza kustuka kwamba gharama hiyo ni kubwa. Lakini nikikuambia kwamba ushauri nitakaokupa utakwenda kuongeza thamani kubwa kwenye kile unachofanya ukilinganisha na gharama unazochangia, hutoshangaa kama awali. Waeleze wateja sababu ya vitu vilivyo na watakuwa tayari kukubaliana na wewe.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Hali Ya Kukosa Uthubutu Na Kuingia Kwenye Biashara Itakayokufikisha Kwenye Ubilionea.

SIRI SABA ZA MAFANIKIO AMBAZO WENGI HAWAZITUMII.
Na sasa karibu kwenye siri saba za mafanikio ambazo mwandishi Joe Vitale amejifunza kutoka kwa Bruce.

SIRI YA KWANZA; Waoneshe watu biashara ambayo hawaijui. Badala ya kufanya biashara kwa kutoa kile ambacho unakitoa, jua sababu kubwa iliyopo nyuma ya biashara yako na wapatie watu sababu hiyo. Badala ya kuuza chakula, uza huduma za watu kuwa na afya bora kupitia ulaji. Badala ya kuuza magari uza njia bora za usafiri kwa watu. Unapoifikiria biashara yako kwa namna inavyomsaidia mteja, unaweza kuwashawishi wengi kununua kutoka kwako.

SIRI YA PILI; Jitengeneze kuwa mtu aliyebobea kwenye biashara unayofanya. Mfanye mteja akifika kwako ajue amefika kwenye suluhisho la changamoto zake. Jiweke kwenye hali ambapo huwi tu mfanyabiashara, bali pia unakuwa mshauri wa wateja wako. Washauri vyema kwa namna watakavyonufaika na siyo kuwalaghai ili wanunue kwako.

SIRI YA TATU; Tumia mifano kuwasukuma wateja kuchukua hatua. Unaweza kuwashawishi wateja wanunue kwako kwa kutumia hadithi za mifano ya watu ambao wamenufaika kupitia biashara yako. watu wanapenda hadithi zinazoendana na changamoto zao au malengo wanayotaka kuyafikia. Tumia nafasi hiyo kuwawezesha kuondokana na changamoto zao au kufikia ndoto zao.

SIRI YA NNE; Wape wateja changamoto bila ya kuwatukana. Unapotangaza biashara yako, wafanye watu waweze kuchukua hatua kwa haraka, lakini usiwatukane wala kuwadanganya. Kwa mfano matangazo mengi yanakuwa na taarifa kwamba wahi nafasi ni chache, inawezekana nafasi siyo chache kweli, lakini watu hawasukumwi kuchukua hatua mpaka waone wanakosa kitu.

SIRI YA TANO; Jenga uaminifu na wateja wako na uza kitu ambacho unakiamini kweli. Wateja wanajua ni mtu gani yupo halisi kwa anachofanya na mtu gani anataka tu kupata faida. Usiwe mtu ambaye yupo kwa ajili ya faida pekee, bali kuwa pale kwa sababu kuna mchango unaoweza kuwapatia wengine.

SIRI YA SITA; Kuwa mtoaji. Japokuwa upo kwenye biashara ili upate faida, unahitaji kutoa ili kupata zaidi baadaye. Unapojitolea kwenye baadhi ya mambo, unajenga uaminifu mkubwa kwa wateja wako na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kukuza biashara yako. usiwe mtu wa kuangalia nanufaikaje kwenye kila kitu, wakati mwingine angalia unachangia nini kwa wateja wako na kwa jamii yako pia.

SIRI YA SABA; Kuwa bora zaidi kila siku, kuwa bora kwenye kile unachofanya, huduma unazotoa, matokeo unayotoa. Kila wakati kuwa tayari kubadilika kadiri mambo yanapobadilika. Unaporidhika na kuona umeshamaliza kila kitu, jua umeshamalizwa.

Tumia siri hizi saba katika kuboresha biashara yako ili uweze kuikuza kwa kufikia wateja wengi zaidi na kujenga mahusiano bora na wateja wako.
Nakutakia kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuongeza maarifa na kuweza kuwa na MAISHA BORA, YENYE FURAHA NA MAFANIKIO MAKUBWA tembelea MOBILE UNIVERSITY, www.mobileuniversity.ac.tz Maarifa yapo kwenye vitabu, karibu tuyachimbe.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: