Watu wengi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kutaka kuwaonesha wengine au kuonekana wao ni watu wa aina gani.
Wapo ambao wanatumia nguvu nyingi kujieleza kwamba ni watu wema na wanaojali sana kuhusu wengine. Pia wapo ambao wanatumia nguvu nyingi kuwatishia wengine ili waonekane kwamba siyo watu wa kuchezewa.
Lakini binadamu wana tabia moja ya kipekee sana, wanajua kutofautisha kipi halisi na kipi ‘feki’. Mara nyingi kitu chochote ambacho mtu anatumia nguvu sana kufikisha kwa wengine huwa siyo halisi. Na hivyo kadiri unavyokazana kuhakikisha kinawafikia wengine ndivyo nao wanavyokazana kisiwafikie, au wasijali kuhusu kitu hiko.
Kadiri unavyokazana kuwashawishi watu kwamba wewe ni mwema na unajali kuhusu wao ndivyo wanavyozidi kutafuta vitu vya kuonesha kwamba wewe siyo mwema. Kadiri unavyokazana watu wakuone kwamba wewe ni mtu makini na usiyependa mambo ya hovyo hovyo ndivyo watu wanavyozidi kukuona ni wa kawaida.
Ipi njia sahihi?
Njia sahihi ni kuwa, unapokuwa watu wanaona na kuelewa zaidi kuliko pale unapotumia nguvu kuwafanya watu waone na kuelewa. Chochote kila ambacho unataka watu wakione au wakipate kutoka kwako, kuwa kitu hiko. Kuwa kwa kufanya, kwa kuchagua hayo ndiyo maisha yako, na baadaye watu wakikuona wanajua wewe ni mtu wa aina gani na unasimamia nini.
Huhitaji kutumia nguvu nyingi kujaribu kuwalazimisha watu wakuchukulie kama mtu wa aina fulani, unachohitaji ni wewe kuwa yule mtu, kwenye kila kitu unachofanya, iwe ni hadharani au siyo hadharani.
Matendo yanaongea kwa sauti kuliko maneno, hivyo badala ya kupoteza muda wako katika kutumia maneno kuwashawishi watu wakuone wewe kwa namna fulani, tumia matendo kwa kuwa vile unavyotaka kuonekana.
Kama unataka kuonekana kuwa mwema, chagua kuishi maisha ya wema, ya kujali wengine na kufanya kile ambacho kitawanufaisha wengine na siyo wewe tu. Na unafanya hivi kwenye kila kitu, kuanzia mambo madogo mpaka mambo makubwa.
Uzuri mwingine wa kuchagua kuwa ni kwamba hutachoka. Unapojaribu kuwashawishi watu kwa namna nyingine, tofauti na kuwa, unajikuta unaigiza baadhi ya vitu. Maigizo yoyote huwa yana mwisho wake. Lakini unapochagua kuwa, huchoki kwa sababu ndiyo maisha uliyochagua kuishi.
Vyovyote vile unavyotaka watu wakuone, kuwa hivyo katika maisha yako kwa matendo. Matendo yanaeleweka zaidi kuliko maneno.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; NENO LA LEO; Mawazo, Maneno, Matendo, Haiba Na Hatima Yako.