Tatizo la kusubiri ni kwamba ndiyo njia rahisi sana ya kutokuchukua hatua.

Huwa inakuwa hivi, unapata wazo zuri sana ambalo unaona kama utalitekeleza, basi maisha yako yatakuwa bora sana. Au unaiona fursa nzuri sana, ambayo kama utachukua hatua utanufaika sana.

Lakini kama ilivyo kwa wengi, unasema nitaifanya, subiri kwanza hili na hili likae vizuri. Na unajipa sababu za msingi kwa nini unahitaji kusubiri kabla ya kuanza.

Na hapa ndipo linapokuja tatizo kubwa la kusubiri, ambapo ni kutokuchukua hatua. Unaposema unasubiri, ile hamasa uliyokuwa nayo inapoa, na kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo inavyokuwa vigumu kusema utaanza. Kila mara utapata sababu kwa nini huwezi kuanza, na hivyo utaendelea kusubiri.

Na tatizo jingine linakuja pale unapogundua kuna mtu mwingine ameshaanza kufanyia kazi lile wazo ulilokuwa nalo, tena kwa mtindo ule ule uliokuwa unafikiria wewe na kwa eneo lile lile.

Unachohitaji kufanya ni kuwa mtu wa kuchukua hatua, unapopata wazo au unapoona fursa ambayo unajua kabisa ni muhimu wewe kuifanyia kazi, basi usisubiri, badala yake angalia unaweza kuanzia wapi, kwa hapo ulipo na kile ulichonacho. Sahau kufikiria kile ulichokosa, badala yake angalia kile ulichonacho sasa kinakusaidiaje kuanza.

Unapoanza, unapata msukumo wa kuendelea zaidi, kuliko kusema unasubiri. Usisubiri tena, anza kuchukua hatua. Wakati haukusubiri na hata wengine hawakusubiri, fursa uliyoiona wewe na wengine pia wataiona, chukua hatua.

SOMA; UKURASA WA 05; Anzia Hapo Ulipo, Anza Na Ulichonacho.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kinachonikwamisha mimi kuchukua hatua kwenye fursa ninazozipata ni tabia yangu ya kupenda kusubiri. Nimekuwa nikisubiri mpaka mambo yangu yaende vizuri ndiyo nichukue hatua. Kwa njia hii nimekuwa napoteza hamasa na kutoa nafasi kwa wengine kuanza. Kuanzia sasa sitosubiri tena, nitakapoiona fursa inayonifaa, nitachukua hatua mara moja.

NENO LA LEO.

Unapopata wazo au fursa nzuri kwako, usiseme unasubiri mpaka mambo yako yawe sawa. Badala yake anza kuchukua hatua mara moja kwa pale ulipo na kile ulichonacho kwa wakati huo.

Ukisema unasubiri ile hamasa ya kufanya itapotea na utashangaa kuona wengine wakifanya kile ulichofikiria ungefanya.

Unapopata fursa au wazo, anza kufanyia kazi mara moja.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.