Inawezekana huna akili sana kama ambavyo watu wengine wanaonekana kuwa nazo.

Inawezekana huna vipaji ambavyo unaona vimewawezesha wengine kufika pale ambapo wamefika.

Inawezekana hukupata elimu bora na ya juu kama ambayo wengine wameweza kupata.

Inawezekana huna mtandao mzuri na mkubwa unaoweza kukupa fursa nzuri kama ambavyo wengine wana mitandao hii.

Inawezekana umetokea mazingira magumu sana ambayo hayakupi wewe nafasi ya kuweza kufanikiwa.

Lakini haya yote hayakuzuii wewe kufanikiwa, kama upo tayari kujitoa kwa kitu hiki kimoja; KUFANYA KAZI KWA JUHUDI KUBWA NA MAARIFA.

Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ndiyo kitu pekee kinachoweza kukutoa chini na kukufikisha kwenye mafanikio hata kama umekosa vile ambavyo wengine wanavyo. Kuwa tayari kuweka juhudi kubwa kutakuwezesha wewe kuvuka vikwazo vyote ambavyo unaona vinakuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Kwa hiyo hakuna kitu chochote kinachoweza kukuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa, hakuna kwa sababu hakuna anayeweza kukuzuia wewe kuweka juhudi kubwa kwenye kitu ambacho umechagua kufanya. N kwa mantiki hii tunaweza kusema kwamba kinachokuzuia kufikia mafanikio makubwa ni wewe mwenyewe, kwa kutokuwa tayari kuweka juhudi kubwa kwenye chochote ulichoamua kufanya.

Unapokuwa tayari kuweka juhudi kubwa, lazima utafika mbali zaidi. Utatoa matokeo bora ambayo yatawanufaisha wengine na watakuwa tayari kukulipa kile unachotaka wakulipe.

Kuwa tayari kuweka juhudi kubwa sana kwenye kile unachofanya, usijali wengine wanafanyaje au wanasemaje. Wewe jua ni matokeo gani unayotaka kupata na weka juhudi kubwa kuhakikisha unapata matokeo hayo. Weka juhudi kubwa zaidi ya wengine wanavyoweka, na pia jifunze kuhusu kitu hiko zaidi ya wengine wanavyojua. Kwa kufanya hivi utakuwa umejipa tiketi ya kufikia mafanikio, kwa sababu hakuna kinachoweza kumzuia mtu anayejua kwa undani kile anachofanya, na aliyejitoa kuhakikisha anapata matokeo bora.

Hakuna anayeweza kukuzuia kuweka juhudi na hivyo maamuzi ya ufanikiwe au ushindwe, yapo kwenye mikono yako. Amua kufanikiwa na weka juhudi kubwa kuhakikisha unafikia mafanikio yako.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Getting Results The Agile Way (Mbinu Za Kuwa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Na Kupata Ufanisi Mkubwa.)