Dunia imekuwa inatoa adhabu kali sana kwa kila mtu.
Wale wanaojifunza kutoka kwenye adhabu ya kwanza wanaepuka adhabu nyingine za baadaye. Lakini wale ambao wanashindwa kujifunza, wanaendelea kuadhibiwa na dunia kila siku.
Dunia haina huruma kwenye adhabu hii, wale ambao hawajifunzi wanaendelea kuadhibiwa mara zote, bila ya kujali ni adhabu kiasi gani wameshapokea.
Kuna watu ambao wanaadhibiwa maisha yao yote na hivyo kuona maisha yao ni kama kisirani, wakati ni wao wenyewe wanakaribisha adhabu ya dunia.
Dunia imeweza kuwepo mpaka leo kwa sababu kuna misingi, kuna sheria za asili ambazo zinaiwezesha dunia kuendelea kuwepo mpaka leo na tutaiacha iendelee kuwepo.
Kwa mfano ukienda kwenye mbuga ambapo kuna viumbe mbalimbali, huwa kuna mlinganyo wa viumbe hao. Kipindi ambacho kuna hali ya hewa nzuri, na majani yakawa yanapatikana, wanyama wanaokula majani wanakuwa wengi, chakula kipo na hivyo wanazaliana. Kadiri wanavyokuwa wengi, wanyama wanaokula wanyama nao wanaongezeka, kwa sababu chakula kipo. Sasa hawa wanaokula wanyama wanapokuwa wengi, wanawapunguza wale ambao wanaliwa na wanapopungua chakula kinakuwa shida na hivyo wanaokula wanyama nao wanapungua. Kama majani yamestawi, swala watakuwa wengi, swala wakiwa wengi simba wanakuwa wengi, simba wakiwa wengi swala wanapungua, na swala wakipungua simba nao wanapungua. Hakuna anayesimamia hilo, bali ni sheria ya asili ya dunia.
Sheria hii ipo kila mahali kwenye maisha yako, kwenye kazi na hata kwenye biashara.
Kama kila kazi unayopata unafukuzwa, ni dunia inakuadhibu, kuna makosa ambayo unayafanya.
Kama upo kwenye kazi muda mrefu na hujawahi kupandishwa cheo upo tu na kipato chako hakiongezeki, ni dunia inakuadhibu, kuna makosa ambao unayafanya.
Kama unafanya biashara lakini kila siku unapata hasara, ni dunia inakuadhibu, kuna vitu ambavyo hufanyi au unafanya kwa makosa.
Unapoona mambo hayaendi kama unavyotarajia, usikimbilie kutafuta mchawi wala mtu wa kumlaumu, jiulize ni kwa nini dunia inakuadhibu.
Baadhi ya makosa ambayo dunia inaadhibu kwa ukali sana ni haya;
- Kukosa uaminifu.
- Kukosa uadilifu.
- Uvivu.
- Kukosa umakini.
- Kukosa nidhamu.
- Kutumia muda vibaya.
- Kutumia fedha vibaya.
- Kutafuta njia ya mkato.
- Wizi
- Kutegemea wengine kwa kila kitu.
Angalia vizuri tabia hizo kumi na nyingine zinazofanana na hizo, na utaona jinsi dunia inavyotoa adhabu kali kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria za asili za dunia.
Unapoadhibiwa jifunze na acha kufanya kile kilichokuletea adhabu. Na hapo ndipo maisha yako yatakapokuwa bora.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.