Tumekuwa tunaona watu wengi ambao wanaelekea kwenye mafanikio.

Watu hawa wanakuwa wamejitoa kweli, wanaweka juhudi kubwa na dalili zinaonesha kwamba watafika mbali.

Lakini ghafla tunaona wanaporomoka na kuondoka kabisa kwenye uelekeo wa mafanikio.

Tunaweza kupata sababu nyingi za nje zinazopelekea hali hizo, lakini mara zote sababu huwa zinaanzia ndani ya mtu mwenyewe.

Leo katika ukurasa huu, tutaangalia vitu vitatu ambavyo vinawaangusha wengi, na jinsi ya kuvidhibiti ili visituangushe na sisi. Ili safari yetu hii ya mafanikio iwe ya kudumu na tufurahie matunda ya juhudi zetu.

Kitu cha kwanza ni HASIRA.

Kila mtu anapata hasira, hasa pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo ya mtu. Na hasira inakuwa kubwa zaidi pale ambao mtu mwingine anakuwa amesababisha mambo kuharibika, na anakuwa amefanya hivyo kwa makusudi au kwa uzembe.

Kitu ambacho kinawaangusha wengi ni kushindwa kudhibiti hasira zao, badala ya wao kuzimiliki hasira, hasira zinawamiliki wao na kujikuta wanafanya maamuzi ambayo wanayajutia sana baadaye. Watu wengi wamefanya makosa makubwa na baadaye wanagundua hawakufikiri kwa usahihi kwa sababu hasira zilikuwa zimewatawala.

Dhibiti hasira zako, usikimbilie kuchukua hatua yoyote pale ambapo unakuwa na hasira, badala yake tulia na pumua. Chukua muda kufikiri kwa kina na fanya maamuzi ambayo ni sahihi.

Mwanafalsafa mmoja amepata kusema kukasirika ni rahisi, lakini kumkasirikia mtu sahihi, kwa jambo sahihi na kwa kiwango sahihi ni vigumu mno. Usikubali hasira zikutawale, na kama huwezi kuzizuia basi usifanye maamuzi yoyote ukiwa na hasira, utayajutia.

Kitu cha pili ni ULIMI.

Wanasema ulimi ni kiungo kidogo lakini chenye madhara makubwa sana. Ulimi unaweza kuvunja familia, unaweza kuua watu, unaweza kuangamiza jamii nzima na hata nchi. Kushindwa kuudhibiti ulimi kuna madhara makubwa sana kwa mtu yeyote.

Dhibiti ulimi wako, usiwe mtu wa kusema hovyo na usiwe mtu wa kusema mambo ambayo ni hasi, yale yanayowakatisha tamaa wengine. Ufanye ulimi wako kusema mambo ambayo ni muhimu na unaweza kuyasimamia, pia sema maneno ambayo yanawapa wengine matumaini na hamasa ya kuweka juhudi kwenye kile wanachofanya.

Usikubali ulimi wako kuwa sehemu ya kuharibu maisha ya wengine. Anapokuja mtu na kukuambia mambo ya umbeya kuhusu wengine, uzuie ulimi wako kusambaza umbeya huo kwa wengine zaidi.

Weka thamani kwenye maneno yako, kwamba hutaongea neno ambalo halina thamani kwako na kwa wengine. Na simamia hili.

Kitu cha tatu ni HAMU.

Binadamu ni viumbe ambao mawasiliano yetu na miili yetu ni kupitia hamu. Unakuwa na hamu ya chakula, hamu ya mapenzi, hamu ya kunywa, hamu ya kupumzika na hamu nyingine nyingi.

Kushindwa kudhibiti hamu ni kitu ambacho kimewazuia wengi kufanikiwa, au kuanguka baada ya kufanikiwa. Ni muhimu sana kudhibiti hamu zako, usikubali mwili wako ukuendeshe, bali wewe ndiyo uuendeshe mwili wako.

Kila kitu fanya kwa kiasi, iwe ni kula, kunywa, kupumzika, kufanya mapenzi. Chochote ambacho kinafanywa kupita kiasi kinaleta madhara makubwa kwenye maisha ya mtu.

Nimalize kwa kusema kwamba “mtu awezaye kudhibiti hasira zake, akaudhibiti ulimi wake pamoja na kudhibiti hamu zake, hata kama ana uwezo mdogo kiasi gani, ni lazima atafanikiwa.”

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kwa Nini Hisia Bado Zinatushinda Kudhibiti Na Namna Ya Kuzidhibiti.