Kama kuna mchango wowote unaoweza kutoa kwenye dunia hii, basi unautoa kwa jinsi ulivyo wewe. Na siyo kwa jinsi unavyofikiri au kusema utatoa mchango gani kwenye dunia hii.
Jinsi ulivyo, haiba yako na matendo yako ndiyo vinavyotoa mchango kwenye dunia hii kwa kuanzia na wale wanaokuzunguka. Mchango wako unatokana na yale unayofanya na siyo yale unayosema au kusema utafanya.
Kwa jinsi ulivyo pekee, unaweza kuwa unawahamasisha watu au kuwakatisha tamaa watu. Kuna watu wakikuangalia wanaona matumaini, wanaona inawezekana au wanakosa matumaini na kukata tamaa.
Kile unachofanya kinagusa maisha ya wengine, kinaweza kuyagusa kwa wema na kuwafanya wawe na maisha bora zaidi, au kinaweza kuwagusa kwa ubaya na kufanya maisha yao kuwa magumu zaidi.
Kwa kila tabia uliyonayo, inawagusa wengine. Kwa kila unachofanya iwe unafanya hadharani au kwa kificho, kinawagusa wengine. Ni muhimu kuliangalia hili ili uweze kutuma ujumbe mmoja kwa watu kuhusu wewe na nini unachodhamiria kufanya. Usipokuwa makini na hili unaweza kujikuta unatuma ujumbe tofauti kwa njia ya maneno na vitendo.
Maneno yako yanapokuwa tofauti na vitendo vyako watu hawakuamini, hivyo unakosa wateja, unakosa watu wa kukuajiri na pia kukosa wa kushirikiana nao. Jinsi ulivyo ndiyo mchango ulionao kwenye jamii inayokuzunguka, hakikisha unakuwa bora wakati wote.
Uwe na siku njema rafiki yangu, siku ya tofauti na yenye matokeo bora, kwa kuchagua kuwa bora zaidi.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; SIKU YA 14; Jinsi Ya Kutengeneza Haiba Inayoendana na Mabadiliko.