Hakuna mtu ambaye hapendi kufanikiwa, hakuna mtu ambaye anataka maisha yake yawe magumu siku zote, kila siku awe mtu wa kuteseka na kuhangaika. Lakini bado watu wengi wamekuwa hawayapati mafanikio licha ya kuyatamani sana. Sababu kubwa ya wengi kushindwa kufikia mafanikio licha ya kuyatamani ni kutokujua hasa ni kipi wanataka na pia kutokujua dalili kama wanaelekea kwenye mafanikio au la.
Hili ndilo lililomsukuma E. W. Kenyon kuandika kitabu sign-posts on the road to success. Kupitia kitabu hiki tunajifunza mambo yote muhimu kuhusu mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi wa kitabu hiki;

1. Endelea kufanya. Kinachowatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni uvumilivu kwenye kile wanachofanya. Kwa kila jambo ambalo mtu anafanya, changamoto na vikwazo huwa havikosekani. Wale wanaoshindwa huwa hawawezi kuvumilia kwa muda mrefu na hivyo kukata tamaa. Wanaofanikiwa wanaendelea kung’ang’ana na hivyo kupata mafanikio.
Chochote ambacho umechagua kufanya, endelea kufanya hata kama mambo yanaonekana magumu kiasi gani. Hata usiku uwe na giza kiasi gani, kutakucha na jua litawaka tena, hivi ndivyo mafanikio yalivyo.

2. Kuwa bora zaidi ya wakati uliopita. Kila unapopata nafasi ya kufanya kile ambacho umechagua kufanya, hebu kifanye kwa ubora kuliko ulivyofanya wakati uliopita. Ongeza ubora zaidi na kamwe usifanye kwa mazoea. Unaweza kuongeza ubora kidogo sana lakini baadaye ukapata matokeo bora sana.
Mafanikio makubwa hayatokei kama ajali, bali yanatokana na vitu vidogo vidogo vilivyofanywa kwa muda mrefu.

3. Jitegemee wewe mwenyewe. Hakuna kinachowazuia wengi kufikia mafanikio kama kuwategemea wengine. Ili uweze kufanikiwa lazima uwe tayari kusimama mwenyewe, unawategemea wengine moja kwa moja kwa kila kitu ni kupoteza nguvu zako. Hutakuwa na uwezo wala uhuru wa kufanya kile ambacho unajua ni bora kwako.
Kuwa tayari kusimama mwenyewe, kuwa na nidhamu na jitume sana, hakuna kitakachokuzuia.

4. Kila kitu unachohitaji ili kufikia mafanikio makubwa tayari kipo ndani yako. unachohitaji ni wewe kuweza kujua kile ambacho unacho na kuweza kukitumia. Ndani yako kuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo ambayo wengine hawawezi kufanya, jijue vizuri na fanyia kazi kile ambacho kipo ndani yako.

5. Ufanye mwili wako kuwa mtumwa wako. Safari ya kufikia mafanikio siyo rahisi kama ambavyo wengi wanaota. Safari hii ni ngumu na mwili wako haupendi vitu vigumu, hivyo utajaribu kukufanya wewe uwe mtumwa wa mwili wako. Wewe utataka kuamka mapema ili kufanya yale ya muhimu lakini mwili wako utakudanganya ulale kidogo kwa sababu bado umechoka.
Kufanikiwa unatakiwa kuufanya mwili wako kuwa mtumwa wako, siyo wewe usikilize mwili bali mwili ukusikilize wewe na kufanya vile unavyotaka kufanya.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

6. Ni wewe mwenyewe unayeweza kujiletea mafanikio makubwa.
Ni wewe mwenyewe unayeweza kujua ni kipi hasa unachoweza kukifanya.
Ni wewe mwenyewe utakayeweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya hilo kwa ajili yako. wengine wanaweza kuanzisha tu moto, ila ni wewe unayetakiwa kuuchochea ili uendelee kuwaka.

7. Ipe akili yako mlo kamili. Mlo kamili wa akili yako ni maarifa sahihi yanayoendana na kile ambacho unafanya na unataka kufanikiwa. Jifunze mbinu bora za kufanya kile unachotaka kufanya, ifanye akili yako iweze kuzioana fursa na kuzitumia vizuri.
Watu wengi wamekuwa wanalisha akili zao uchafu ambao unazidumaza zaidi. Uchafu huu ni habari za udaku, kufuatilia maisha ya wengine, habari zenye hofu na mengine ambayo hayana manufaa.

8. Nidhamu binafsi ni kitu kimoja muhimu sana ambacho kitaamua kama mtu anafanikiwa au la. Bila ya nidhamu binafsi huwezi kupata mafanikio, na kama ukiyapata basi yatakuwa hatari sana kwako kuliko ambavyo ulikuwa kabla ya kufanikiwa. Ni muhimu ujijengee nidhamu binafsi ili uweze kujidhibiti na kufanya yale ambayo ni muhimu kwako.

9. Kuna wewe wawili, kuna wewe wa nje ambaye ndiye unaonekana kwa wengine na kuna wewe wa ndani ambaye hakuna anayekuona. Wewe wa nje anapenda sana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, hata kama hakina manufaa kwake. Wewe wa ndani anajua kabisa ni nini anataka na kipi muhimu kwako kufanya. Tatizo huyu wewe wa ndani anazidiwa nguvu na wewe wa nje. Anza sasa kumsikiliza wewe wa ndani na kumpa nguvu kuliko wewe wa nje.

10. Weka maisha yako yote kwenye kile ambacho umechagua kufanya. Usijaribu kitu chochote kwenye maisha, ni kupoteza muda wako ambao ni muhimu na huna wa kutosha. Kama umeamua kufanya kitu, weka maisha yako yote kwenye kitu hiko, ona kwamba hiko ndiyo kitu pekee ambacho unataka kisimame kwa niaba yako, weka akili, moyo na maarifa yako yote kwenye kile unachofanya. Kwa njia hii hakuna kitakachokuzia kufikia mafanikio.

11. Mashirika makubwa yanawatafuta watu ambao wanaweza kuyaingizia faida. Watu wengi wanatafuta mtu anayeweza kuwatatulia changamoto za maisha yao. Je wewe unaweza kuwa mtu huyu ambaye anatafutwa na wengi? Siyo vigumu kuwa mtu huyu, unachohitaji ni kutoa matokeo ambayo ni bora sana, ambayo watu wengine hawawezi kuyatoa.

12. Usikubali kutumika maisha yako yote. Katika kipindi fulani kwenye maisha yako, utatumika na wengine, lakini usikubali kubaki hapo maisha yako yote. Usikubali wengine wakutumie wewe kutimiza ndoto zao huku wewe ukibaki kuwa kawaida. Jiwekee muda ambao utatumika na baada ya hapo anza kujitumia wewe mwenyewe.
Kama upo kwenye ajira unatumika na wengine, usikubali kutumika maisha yako yote.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

13. Kuwa makini na wale wanaokuzunguka, zungukwa na watu ambao ni washindi, watu ambao wamefanikiwa na hawa watakupa hamasa ya kufanikiwa zaidi. Kama utazungukwa na watu walioshindwa, huwezi kupiga hatua. Hii ni kwa sababu watakurudisha nyuma kwa maneno na vitendo.

14. Maneno yana nguvu kubwa ya kujenga au kuharibu. Kuwa makini na maneno yako, kwa kuongea na hata kuandika. Hakikisha unaongea na kuandika kile ambacho una uhakika nacho na unaweza kukisimamia. Usiwe sehemu ya wanaosambaza maneno ambayo hayana msaada kwa wengine.

15. Uaminifu na uadilifu ni nguzo ambazo huwezi kuzikwepa kama kweli unataka kufanikiwa. Kuna watu ambao wanafanikiwa kwa njia ambazo siyo za uaminifu, lakini mafanikio yao huwa hayadumu. Hata uwe na uwezo mkubwa kiasi gani, hata uwe na biashara bora kiasi gani, kama siyo mwaminifu huwezi kufika mbali.

16. Dunia inakudai. Watu wote walioleta mabadiliko makubwa duniani, walifanya hivyo kwa sababu waliona maisha ya watu yangeweza kuwa bora zaidi. Zikagundulika simu, kompyuta, mtandao wa intaneti na kila kitu ambacho tunatumia na kufurahia. Swali ni je wewe unawezaje kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi?
Dunia inakudai wewe utoe mchango kwa wengine kama ambavyo umetumia michango iliyotolewa na wengine. Unawezaje kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi kwa wengine kuishi?

17. Kisiasa na kijamii tumefundishwa kuwachukia watu ambao wametuzidi kifedha au kimafanikio. Tunaona wamefika pale walipo kwa sababu walipata bahati au kuna njia ambazo siyo halali wamezitumia. Huku ni kujidanganya ili tusijione sisi ni wadhaifu.
Ukweli ni kwamba watu wote ambao wamefanikiwa na wakadumu na mafanikio hayo kwa muda mrefu wamepigana sana kufika pale walipo. Wanapambana usiku na mchana kuongeza ubora kwenye kile wanachofanya.
Unapokutana na watu wanasema fulani kafanikiwa kwa sababu ni fisadi au kwa sababu ametokea familia bora, kimbia haraka sana, maana unapoteza muda wa kufikia mafanikio na wakati huo pia unapumbazwa uone mafanikio hayawezekani kwako.

18. Wafanye watu wakutegemee wewe. Hii ndiyo njia ya uhakika kabisa ya kufanikiwa. Kama watu wanakutegemea wewe kwa mambo ambayo ni muhimu kwenye maisha yako, hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa. Wafanye wateja wako wakutegemee wewe kwa bidhaa na huduma bora, na wawe na uhakika kwamba wakifika kwako lazima watapata suluhisho la matatizo yao. Mfanye mwajiri wako akutegemee wewe kiasi kwamba mambo yake hayawezi kwenda bila ya wewe kuwepo, hapa utajijengea thamani kubwa na kuweza kupata matokeo makubwa.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Hali Ya Kukosa Uthubutu Na Kuingia Kwenye Biashara Itakayokufikisha Kwenye Ubilionea.

19. Kuna vitu vitatu ambavyo vinawazuia wengi kwenye safari ya mafanikio;
Kitu cha kwanza ni kuchelewa kufanya maamuzi. Watu wengi wamekuwa wanachukua muda mrefu sana kufanya maamuzi, au wanafanya maamuzi lakini utekelezaji unawachukua muda. Wanapokuja kustuka wanakuta fursa imeshakwisha.
Kitu cha pili ni uvivu wa akili, hapa watu wengi hawapendi kufanya vitu ambavyo vitaumiza akili zao. Badala yake wanaangalia ni kitu gani wengine wanafanya na wao wanaiga. Au wanafanya vitu kwa mazoea.
Kitu cha tatu ni kuongea hovyo na kuwa hasi. Kuwa na mtazamo hasi wa kujikatisha tamaa kwenye kila jambo ni adui mkubwa wa mafanikio. Kuongea hovyo pia ni hatari sana, wengi wamekosa fursa nzuri kutokana na kuongea kwao.

20. Je kila mtu anaweza kufanikiwa? Hili ni swali ambalo wengi wamekuwa wanauliza na wengi wamekuwa wanajitetea nalo, kwamba kila mtu hawezi kufanikiwa, au kila mtu akiwa tajiri nani atamfanyia kazi mwenzake.
Jibu la swali hili ni NDIYO kila mtu anaweza kufanikiwa. Na kipimo cha mafanikio siyo kimoja kwa kila mtu, kila mtu ana kitu ambacho ni muhimu ziadi kwake.
Kuna mfanya usafi wa ofisini ambaye ana mafanikio kuliko rubani wa ndege. Mafanikio hasa yanaanzia kwa mtu mwenyewe, kwa kufanya kile ambacho anasukumwa kufanya kutoka ndani yake, na kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine.
Mafanikio ni yako, hakikisha kila siku unaishi maisha ya mafanikio.

Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza haya uliyojifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

MUHIMU; Kupata vitabu vya kiswahili vya kujisomea tembelea MOBILE UNIVERSITY kwa kubonyeza hayo maandishi. karibu sana tujifunze kwa pamoja.