Mtu ambaye hajui kama anakosea, huwezi kumrekebisha, kwa sababu anahisi yupo sahihi kwa kile anachofanya. Hivyo hata kama utamrekebisha namna gani, ataendelea kufanya kile anachofanya, kwa sababu anajua yupo sahihi. Hapa ndipo changamoto nyingi hasa za mahusiano na mafanikio zinapoanzia.
Kama wewe mwenyewe hukubali kwamba unakosea, huwezi kubadili kile unachofanya, badala yake utaendelea kufanya kile unachofanya sasa. Kama hujakubali kwamba njia unayotumia sasa haiwezi kukufikisha kwenye mafanikio, utaendelea kutumia njia hiyo, hata kama inakupoteza. Kama hujakubali kwamba umekosea, utaendelea kufanya kile ambacho umekuwa unafanya.
Hatua ya kwanza ni kukubali, kukubali kwamba unachofanya hakitakufikisha kule unakotaka kufika, kisha uchukue hatua ya kufanya kile ambacho kitakufikisha unakotaka. Ni lazima ukubali ya kwamba umekosea kwa kile ulichofanya, ndiyo uamue kurekebisha makosa yako.
Ni lazima ujikamate wewe mwenyewe ukiwa unapita kwenye njia ambayo siyo sahihi, au ukiwa unafanya kitu ambacho siyo sahihi ndipo uweze kujirekebisha. Tofauti na hapo itakuwa vigumu kwako kutoka hapo ulipo sasa.
Kwa kifupi ni kwamba utaendelea kuwa hapo ulipo sasa, ukifanya hiko unachofanya sasa, mpaka pale utakapokubali kwamba hapo ulipo siyo sahihi. Utaendelea kufanya kazi unayofanya, ambayo huenda haikupatii kile unachotaka, mpaka pale utakapokiri kwenye nafsi yako kwamba kazi hiyo haikufai, upate hasira na hamasa za kufanya kila juhudi ili kuondoka. Utaendelea kufanya biashara hiyo unayoifanya, kwa viwango hivyo unavyofanya mpaka pale utakapokubali kwamba njia unayotumia siyo sahihi ndipo uweze kuchukua hatua.
Kukubali kunaanzia ndani ya mtu mwenyewe, hakuna anayeweza kukulazimisha ukubali, wala wewe huwezi kumlazimisha mtu akubali kwamba amekosea au hayupo njia sahihi. Ndiyo maana waswahili walisema mtoto akililia wembe mpe, akijikata atajifunza. Unaweza kukazana kumwambia mtoto kwamba wembe unakata lakini hatakuelewa, siku akiushika ukamkata ndipo atakapojifunza kwa hakika kwamba wembe siyo kitu cha kuchezea.
Kuna watu unaweza kuwashauri vizuri lakini wasifanye kile walichoshauriwa, mpaka pale wanapojaribu njia tofauti na kujikuta wanapata matokeo ambao siyo bora.
Kubali kwanza ya kwamba njia uliyo sasa haitakufikisha pale unapotaka kufika, kubali kwanza ya kwamba umekosea kwenye kile ulichofanya. Hii ndiyo hatua ya kwanza na ya muhimu ya kujirekebisha na kukaa kwenye njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.