Habari mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema na kama hauko vizuri pole kwani changamoto ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Karibu tuweze kujifunza ndugu mpendwa msomaji.

Katika swala la kujifunza katika jamii yetu bado limekuwa ni gumu sana. Ukikutana na watu kumi ukiwauliza unapenda kusoma vitabu utasikia wakisema napenda kusoma vitabu ila sina muda. Muda umekuwa kisingizio kwa watu wengi kutupia lawama zao zote katika muda. Watu wanasingizia muda umekuwa tatizo lakini mimi nakataa nasema muda sio tatizo. Habari njema ni kwamba Mungu ametuzawadia zawadi au rasilimali muhimu kuliko zote ambayo ni muda. Kila binadamu aliye hai ana muda wa masaa 24 kwa siku hivyo kwa wiki moja kila mtu ana jumla ya masaa 168 sasa katika masaa 168 kwa wiki nzima unakosa muda kweli wakusoma vitabu na kuongeza maarifa?

Akili yako inahitaji maarifa kila siku ili iweze kukua, akili yako inahitaji chakula kila siku kama unavyolisha tumbo lako nalo linahitaji maarifa. Hazina ya akili yako ni maarifa na maarifa yanapatikana katika kusoma vitabu, makala chanya, na siyo kusoma magazeti ya udaku, kusikiliza habari nyepesi nyepesi zisizokuwa na upembuzi yakinifu. Jinsi unavyokaa bila kusoma ndivyo akili yako inakaa inazidi kulala ukisoma nayo inazidi kuamka. Jitahidi kusoma na kufikiri kila siku ndio zoezi la akili yako. Kuwa na shahada, astashahada, stashahada, uzamili na uzamivu siyo mwisho wa kusoma au kujifunza bali huo ndio mwanzo wa kujifunza. Usiridhike na maarifa uliyonayo bali kuwa na njaa kali ya maarifa elimu uliyopata darasani ni msingi tu wa kusoma. Mtu anayesoma anakuwa tofauti sana na mtu asiyesoma vitabu tafadhali nakuomba anza kujifunza kuna faida nyingi zisizoelezeka.
Sasa leo ni siku ya kuondoa visingizio vya kukosa muda wa kusoma vitabu kwani leo utaweza kujifunza sehemu za kupata muda wa kusoma vitabu na kuongeza maarifa. 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Zifuatazo ni sehemu ambazo unaweza kupunguza au kuacha kabisa na kupata muda wa kusoma vitabu;

1. Kuangalia Luninga au Tv;
Kuangalia televisheni ni moja ya adui wako mkubwa anayekumalizia muda na kuharibu afya yako ya mwili wako. Kuna watu wanaangalia tv zaidi ya masaa mawili kwa siku. Kama umeamua kusoma vitabu punguza muda wa kuangalia tv na soma kitabu. Kabla hujafikiria kuangalia tv fikiria kwanza kusoma kitabu kwani utakua umejikomboa. Hivyo basi, kama wewe unakosa muda wa kusoma vitabu tafadhali punguza kuangalia tv, kufuatilia filamu au tamthilia mbalimbali na utapata muda wa kusoma kitabu. Kuangalia tv, filamu na tamthilia vitakuongezea msongo wa mawazo na kukujaza mtazamo hasi na kuishi maisha ya kuigiza kama vile mwigizaji filamu.

2. Kutembelea Mitandao Ya Kijamii;
Mitandao ya kijamii kwa karni ya sasa umekuwa ni ugonjwa unaopotezea watu muda. Watu wanapoteza umakini katika kazi zao na kupata matokeo mabovu. Kama ulikuwa unatembelea mitandao ya kijamii kila saa moja na unahisi usipoangalia unapitwa kubali kupitwa na habari za mitandaoni lakini usikubali kupitwa na kusoma kitabu. Punguza muda wako mwingi unaotumikia katika mitandao ya kijamii na pata muda wakusoma kitabu. Kama unaweza kutumikia mitandao ya kijamii kwa muda wa saa moja hadi mawili toa hapo na muda wa kusoma kitabu utakua umejikomboa kutoka katika hatari.

3. Kukaa Vijiweni Na Kupiga Stori;
Huwa napenda sana kuwahamasisha watu kusoma vitabu nikiona watu wamekaa vijiweni na kupiga stori na kubishana mambo ya siasa, mipira nakadhalika huwa naumia sana jinsi wanavyopoteza na kusahau kuwa maisha ni muda bila kutumia muda wako vizuri utakua unajipunguzia muda wa kuishi duniani kama tunakubali kuishi katika falsafa ya maisha ni muda. Badala ya kusingizia huna muda wa kujifunza acha kwenda vijiweni au punguza na tumia muda huo kusoma kitabu utakua mbali sana kifikra kwani umasikini wa mtu unaanzia akilini siyo mfukoni.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Sign-Posts On The Road To Success (Alama Muhimu Kwenye Safari Ya Mafanikio).

4. Kuchati na Kuongea na Simu;
Kuna watu ni wataalamu wa kuchati na kuongea na simu tena wanajisifu mimi kwa kuchati meseji mia moja zinaisha mara moja na hakuna kitu cha msingi katika kuchati huko bali ni kukosa kazi ya kufanya. Kama una kazi ya kufanya huwezi kuchati utaweka umakini wako katika kazi. Kwa hiyo, kama kisingizio ni muda basi punguza muda wa kuchati hovyo na kuongea na simu na utapata muda wa kusoma kitabu na kuongeza maarifa.

5. Kutokuwa na Ratiba;
Kama unaishi maisha yasiyokuwa na ratiba basi maisha yako ni sawa na mtu ambaye anasafiri na hajui anapokwenda. Usipokuwa na mwelekeo basi mwelekeo wowote utakuchukua kwa kingereza wanasema if you don’t have a direction, any direction will take you. Kuwa na ratiba ndugu, utapata muda wa kusoma kitabu na ratiba yako ndio itakua mwongozo wa siku yako hivyo huwezi kurukia na kufuatilia mambo ambayo hayako katika ratiba yako kwani ikifika jioni utajithamini siku yako ilikuwaje na kama utakua hujafuta ratiba yako utakua hujatimiza malengo yako.

6. Kuamka Mapema Alfajiri;
Kama unataka kupata muda wa kusoma na kuendelea na shughuli za kila siku amka mapema soma kwanza kabla kelele za dunia hazijaanza hapo utakua umeanza siku yako vema. Acha tabia ya kulala zaidi ya masaa elekezi ya watu wa afya inavyoelekeza, kama una tabia ya kulala hovyo kupita kiasi ni hatari pia kwa afya yako. Kama una tabia ya kusifika wewe ni bingwa wa kulala sana tafadhali acha na tumia hiyo fursa kujiongezea maarifa kwa kusoma vitabu.

7. Kuacha Uvivu; kama mtu ni mvivu hata wa kuhudumia mazingira anayoishi, mwili wake mwenyewe ni shida hata kuhudumia akili yake pia itakua ni shida. Uvivu ni mbaya sana unaharibu mambo mengi ya watu. Dawa ya uvivu ni kufanya sasa na siyo baadae hakikisha sababu zote za uvivu unakwenda kuzizika na uwe huru. Hivyo, kupitia kuacha uvivu utapata muda wa kusoma vitabu utakua unafanya shughuli zako kwa wakati
SOMA; KITABU CHA JULY; MIMI NI MSHINDI, Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu.

8. Acha Kauli Za Kujifariji;
Kuna mabingwa wa kujifariji kupita maelezo nitasoma baadae, nitaanza kusoma nikiwa nimepata kitu fulani, nitaanza kusoma nikimaliza masomo yangu na kauli nyingi za kujifariji na kujiona wewe ndio mshindi kumbe ni mshindwa. Kujifariji ni kuongozwa na hisia. Maamuzi ya hisia yanaongozwa na ubongo wa kati ambao ndio unatawala hisia zote, hasira, furaha nk ukikubali kuongozwa na ubongo wa juu ambao ni ubongo unafanya maamuzi sahihi kwa njia ya mantiki. Acha kauli kama hizi na jipatie muda wa kusoma kitabu.

9. Kuwa Na Shauku Na Maamuzi Ya Utayari;
Kuwa na shauku ni nguvu yenye hamasa ndani yake. Ukiamua kufanya maamuzi ya utayari wa kusoma vitabu na hamasa iliyoko ndani yako huwezi kukosa muda wa kusoma kitabu. Kama vile unavyotafuta muda wa kula chakula na hata kwenye kusoma nako utakua na njaa ya kusoma na hatimaye utapata muda wa kujifunza.

10. Umbea, Majungu, Kusengenya Na Kuhukumu;
Kabla hujaanza kupiga umbea, kuhukumu, kusengenya , majungu na wivu jiulize sababu kumi kwanza unapata faida gani chanya? Kama hakuna acha chukua kitabu na anza kusoma kwani utapata maarifa ya kutosha. Maarifa ndio silaha ya mtu makini utapimwa kama wewe ni mtu makini kulingana na madini adimu yanayotoka ndani ya kinywa chako na siyo umefanya umbea kiasi gani. Kwa hiyo ukiacha vitu hivi umbea, majungu, kusengenya, kuhukumu, watu bila kujua ukweli na kuwa na wivu na wenzako bila sababu na muda huo ukautumia kwenye kusoma utakua mbali sana kama ukianza sasa zoezi hili.

Hatua ya kuchukua;
Kama umeamua kubadilika na kuzizika sababu zote hizo hapo juu hongera sana. Kama unataka kuanza kuwa mtu wa kusoma vitabu na hujui wapi pa kuanzia fuata maelekezo haya; kuna kundi la kusoma vitabu liitwalo Tanzania Voracious Readers (TVR) katika kundi hili tunasoma vitabu viwili kwa wiki na kujadili mambo tuliyojifunza kupitia vitabu hivyo siku ya jumamosi kupitia mtandao wa Telegram.
Pia kuna vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambavyo utaweza kuvipata na kukufikia hapo ulipo na kuanza kuongeza maarifa.

Kupata vitabu vya kiswahili vya kujisomea tembelea MOBILE UNIVERSITY 

Hivyo kama utahitaji kujiunga na kundi la Tanzania Voracious Readers wasiliana na mimi ( Deogratius Kessy ) kwa simu namba 0717101505 au Makirita Amani kwa simu namba 0717396253.

Mwisho, kila binadamu ana muda sawa, punguza mambo hasi uliyojifunza leo na jifunze mambo chanya. Punguza hata kukaa baa na kunywa pombe utapata muda kusoma kitabu, kuhudhuria vikao visivyokuwa na tija, kulalamika na kulaumu utapata muda mzuri wa kujifunza. Kumbuka maarifa ndio hazina ya akili yako na adui wa akili yako ni wewe mwenyewe.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com