Kupata unachotaka kwenye maisha yako inawezekana, ila siyo kitu rahisi. Na hii ndiyo sababu ni wachache sana ambao wameweza kupata kile wanachotaka, wengi wanapokutana na ugumu wanaacha na kukubali kile ambacho wamekipata.

Hakuna kitu kizuri na chenye thamani ambacho kinapatikana kwa urahisi, unahitaji kuweka juhudi, kuwa mvumilivu na kutokukata tamaa. Najua haya yote unayajua, lakini leo nataka nikuongezee kitu muhimu sana.

Kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, hapa ni baada ya kujua ni nini unataka na umeshaweka malengo yako, zingatia haya matatu;

Kwanza weka juhudi za kutosha, ninaposema juhudi za kutosha ni kwamba uwe tayari kuweka juhudi kubwa sana, tofauti na wengine walivyo tayari kuweka juhudi hizo. Unahitaji kujisukuma hata pale unapokuwa umechoka.

Pili jiwekee deni ndani yako, ona kwamba kuna kitu kikubwa ambacho dunia inakudai, dunia inataka kitu kutoka kwako na ni wewe pekee unayeweza kuipatia dunia kitu hiko. Hii itakusukuma katika kuweka juhudi kubwa zaidi.

Tatu tumia akili yako katika kufikiri na kuota. Huhitaji tu fikra ili kupata kile unachotaka, pia unahitaji kuwa na ndoto, unahitaji kuwa na taswira ya kule unakotaka kufika, unahitaji kujiona pale ambapo unataka kuwepo. Hii itakupa hamasa zaidi kwa sababu utakuwa unajiona pale ambapo upo tayari.

Angalia mambo hayo matatu, hayajali kabila lako, umri wako, wala elimu yako. Hayajali kama umetokea familia ya kitajiri au kimasikini. Yanachojali ni uwe unajua ni nini unataka a umeweka malengo ya kupata unachotaka.

Hivyo mtu yeyote anayetaka kufanikiwa, hakuna kinachoweza kumzuia bali yeye mwenyewe. Usiwe kikwazo cha mafanikio yako mwenyewe.

Kila la kheri.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Usipigane Na Usichokitaka Na Jinsi Ya Kupata Unachotaka.