Unapoanza kufanya kitu chochote kipya kwenye maisha, unaanza kwa kuiga. Unaangalia wale ambao ni bora kwenye kile unachotaka kuwa bora, unaona wanafanyaje kisha na wewe unaanza kufanya kama wao. Kwa kuiga utapiga hatua kubwa, kutoka mtu ambaye hajui kabisa mpaka mtu anayejua kile anachofanya.
Changamoto moja ya kuiga ni kwamba haitakufikisha kwenye ubora wa hali ya juu, haitakuwezesha kuwa na mafanikio makubwa sana. Badala yake itakufanya uwe chini ya yule ambaye umekuwa unamuiga, au anayekuhamasisha kuwa kama yeye.
Hivyo baada ya kuanza na kujua kile unachofanya, unahitaji kuacha kutumia sheria za wengine na kutengeneza sheria zako mwenyewe, ambazo zitaendana na wewe kwa uwezo wako, mazingira yako na pale unapotaka kufika.
Mpaka sasa unajua ya kwamba hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu hapa duniani. Na pia unajua hakuna njia moja sahihi au jibu moja sahihi ambalo kila mtu akilitumia atapata matokeo bora sana. Bali kuna njia tofauti kwa watu tofauti. Unahitaji kuijua njia yako ni ipi na kuifuata. Hutaweza kuijua kama utaendelea kutumia sheria za wengine, wale ambao unataka kuwa kama wao.
Muue mhamasishaji wako.
Kwenye mchezo wa kong fu wa kichina, inasemekana kwamba ili aweze kuwa masta, mwanafunzi ni lazima aweze kumpiga au kumuua mwalimu wake. Na hapa ndipo anapopata uhuru wa kutengeneza mbinu zake mwenyewe.
Je wewe ni masta gani ambaye upo chini yake? Ambayo unamuiga na anakuhamasisha? Ambaye unafanya kama anavyofanya yeye? Mjue masta huyu na muue mara moja ili uanze kuwa huru kutengeneza na kutumia sheria zako mwenyewe. Nina imani ninaposema muue tunaelewana vizuri, siyo uende kutoa uhai wake, bali taka kuwa bora zaidi yake.
Kuna wakati ambao unahitaji kuwa chini ya watu, kuna wakati ambao unahitaji kujitoa chini yao na kutengeneza njia yako mwenyewe.
Utajuaje kama wakati wa kutoka chini ya wengine umefika? Utajua utakapokuwa tayari kwa sababu utaona kila kitu kama kinafaa kuboreshwa na ukianza kuboresha unapata matokeo bora zaidi ya wengine. Hapo ndipo unapoanza kutengeneza sheria zako mwenyewe zitakazokuletea matokeo bora kabisa.
Usikubali kuendelea kuwa chini ya wengine maisha yako yote, utakapofika wakati ondoka na tengeneza himaya yako mwenyewe, hivi ndivyo watu wanavyofikia mafanikio makubwa.
Kila la kheri rafiki.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
SOMA; UKURASA WA 284; Maisha Hayasimami, Unakuwa Bora Au Unakuwa Hovyo.