Linapokuja swala la maisha ya mafanikio, uwezo unaweza usitumike sana. Ndiyo tunajua ya kwamba kila mtu ana uwezo wa tofauti, uwezo mkubwa ambao upo ndani yake, ambao ndiyo unamwezesha kupata matokeo ya tofauti na wanayopata wengine.

Lakini katika kufikia mafanikio makubwa, uwezo pekee unaweza usitoshe, badala yake unahitaji kuwa tayari kufanya chochote kinachohitajika kufanya. Ili uweze kuwa tayari kufanya chochote unachohitajika kufanya, inabidi usahau kuhusu uwezo kwa sababu vingi utakavyohitajika kufanya vitakuwa nje ya uwezo wako.

Mafanikio makubwa hayategemei kwenye uwezo pekee, bali yanategemea kwenye nini unachotaka kupata na upo tayari kiasi gani kufanya chochote unachohitajika kufanya.

Kuna watu ambao wana uwezo mkubwa sana lakini hawajaweza kufanya jambo lolote kubwa. Pia kuna watu ambao wana uwezo mdogo lakini wameweza kufanya makubwa. hapo ndipo juhudi zinapoleta tofauti.

Yule anayekuwa tayari kufanya kila anachohitajika kufanya ili aweze kufika pale anapotaka kufika, uwezo hauhusiki tena, bali mbinu, maarifa na juhudi zake ndiyo zinahusika.

Wakati mwingine ni vigumu sana kujua uwezo ambao upo ndani yetu, hasa kwa malezi tunayopata ambapo tunaaminishwa vitu ambavyo siyo vya kweli kuhusu sisi wenyewe na nini tunaweza kufanya.

Hivyo sahau kuhusu ndani au nje ya uwezo wako, na badala yake jua hasa ni nini ambacho unataka kupata au unataka kufikia na kuwa tayari kufanya chochote unachohitajika kufanya ili kufika pale. Unapofikia maamuzi haya, usijionee tena huruma, badala yake unahitaji kuweka juhudi kubwa sana.

Hakuna kilichopo nje ya uwezo wako kama kweli umedhamiria kukipata, mara zote ipo njia kwa wale ambao wamegoma kukata tamaa, hebu na wewe uwe mmoja wa watu hawa wasiokata tamaa.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Getting Results The Agile Way (Mbinu Za Kuwa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Na Kupata Ufanisi Mkubwa.)