Moja ya tabia ambazo wanadamu tunazo ni wivu, tunachotofautiana ni namna gani tunaweza kudhibiti na kutumia wivu wetu.
Kwa upande mmoja kuna ambao wanaweza kudhibiti wivu wanaoupata na hivyo kutokufanya jambo lolote baya, pia kuna wanaoweza kuutumia kama changamoto kwao kufanya makubwa zaidi.
Kwa upande mwingine kuna ambao hawawezi kudhibiti wivu wanaoupata kuhusu wengine, na pia hawawezi kuutumia kama changamoto kwao kufanya makubwa, badala yake wanautumia wivu huo kuwaharibia wale ambao wanawaonea wivu.
Leo hapa tutaangalia jinsi ya kuzuia wivu wa wengine kuharibu mipango yako, kwa sababu kuna wengi sana wanaokuonea wivu na watakaokuonea wivu kwa namna unavyoishi maisha bora.
Kuna kitu kimoja ukikifanya kitapunguza kwa kiasi kikubwa wivu ambao wengine wanao kwako. Kitu hiko ni kutoruhusu watu wengine wajue sana kuhusu wewe. Usiweke wazi sana taarifa zako, hasa taarifa binafsi. Wivu wa watu unaongezeka kutokana na taarifa nyingi walizonazo kuhusu wewe. Na mara nyingi taarifa hizi ni za ndani na wewe mwenyewe ndiye unayezitoa kwa wengine.
Taarifa binafsi kuhusu maisha yako kama afya yako, kipato chako na hata mahusiano yako, usizifanye kuwa wazi kwa kila mtu. Wacha watu waone kwa nje tu, lakini wasielewe hasa ni nini kinaendelea ndani. Watu wanapokosa taarifa za kutosha hawawezi kufanya chochote cha kukudhuru wewe.
Kwenye wivu pia unahitaji kuwa makini na watu wa karibu sana kwako kama ndugu na hata marafiki. Ndugu zako kabisa wanaweza kuwa chanzo kikuu cha wivu, au rafiki uliyemwamini sana ndiyo anaweza kuwa chanzo kikuu cha wivu.
Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida, wape watu zile taarifa zinazowahusu na siyo kuweka taarifa zako binafsi. Unaweza kuona unawashirikisha kitu cha kawaida, ukawaona wanakuchekea lakini kwa ndani wanaumia sana kwa nini wewe uweze na wao washindwe. Kadiri unavyoongea sana ndivyo wanavyopata upenyo wa kukuharibia.
SOMA; UKURASA WA 283; Dawa Ya Hofu, Wivu, Chuki Na Hisia Zote Hasi…
Hakuna mtu anayeweza kukuharibia mipango yako kama wewe hutatoa nafasi kwao kwa kuwaonesha udhaifu wako uko wapi. Na utawaonesha udhaifu wako kadiri unavyoongea sana.
Ninachosema hapa siyo uwe msiri au mbinafsi, badala yake chagua taarifa ambazo kila mtu anaweza kuzijua kuhusu wewe na chagua taarifa ambazo ni marufuku watu kuzijua kuhusu wewe. Kwa sababu hazitawasaidia na zaidi zitawafanya wakuonee wivu na kutaka kuvuruga mipango yako.
Mitandao ya kijamii imeongeza sana shida hii ya wivu, kwa sababu tunashawishika kuonesha kila kitu kuhusu maisha yetu kupitia mitandao hii, kuanzia kuvaa mpaka kula. Epuka hili, mambo matatu yasiwe wazi kwa kila mtu, afya yako, kipato chako na mahusiano yako.
Usiwape watu upenyo wa kutumia udhaifu wako kukuharibia, dhibiti taarifa zako zinazowafikia wengine.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)