Kila mtu anapenda wengine wafanye kile ambacho anataka yeye, kwa kuamini kile anachotaka kifanyike ndiyo bora. Inawezekana kile ambacho mtu anataka kifanyike ni kweli ni kitu bora au wakati mwingine siyo bora.

Hivyo kwa kutaka kuwabadili wengine, watu huwa wanatumia njia mbalimbali, na mara nyingi njia hizi huwa hazileti matunda ambayo watu wanayataka.

Njia maarufu na inayotumiwa na wengi ni kutishia, usipofanya hivi basi kitu hiki kibaya kitatokea kwako. Na njia hii inaweza kuwasukuma watu kuchukua hatua, lakini baadaye watagundua kwamba walidanganywa kwa vitisho na hawatakubali tena kuchukua hatua.

Njia nyingine ya kuwabadili watu imekuwa ni kudanganya na kulaghai. Ambapo mtu anawapa watu matumaini ya uongo ili waweze kuchukua hatua. Kama ilivyo kwenye vitisho, watu watachukua hatua mwanzoni ila baadaye watajua ni uongo na hawatakubali tena kuchukua hatua.

Je ni njia ipi bora ya kuwabadili watu?

Kama wewe ni mfanyabiashara, unataka wateja wanunue kwako, waache kununua kwa wengine na waje kwako. Unahitaji mbinu bora ya kuwabadili watu.

SOMA; Sababu tatu kwa nini biashara nyingi zinakufa haraka.

Kama wewe ni mwajiri au mwajiriwa, unahitaji kuwafanya wale wanaokuzunguka kukamilisha majukumu yao kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Unaweza kufanya hivyo kwa vitisho lakini matokeo hayatakuwa mazuri.

Kwenye familia pia unahitaji kuwabadili watu ili waweze kwenda vizuri.

Ipo njia nzuri na ya uhakika ya kuwabadili watu, njia hii inaanzia na mtu mwenyewe.

Njia ya uhakika ya kumbadili mtu ni kumfanya yeye mwenyewe aone umuhimu wa kubadilika. Hivyo wewe huhitaji kumlazimisha, bali unahitaji kumpa sababu kwa nini anahitaji kubadilika. Na sababu hutampa kwa maneno tu, bali unahitaji kumwonesha kwa vitendo.

Watu wanapenda ushahidi, hivyo tumia ushahidi kuwafanya watu wasukumwe kuchukua hatua ya kubadili na kuboresha maisha yao.

Kama ni kwenye biashara onesha jinsi ambavyo bidhaa au huduma unayotoa ni bora. Kama ni kwenye kazi onesha jinsi wale wanaofanya kazi zao kwa ubora wanavyofanikiwa kuliko wengine. Kwenye kila hali, onesha mifano ambayo watu wanaweza kuiga moja kwa moja.

Kitu kingine unahitaji uvumilivu, sababu inayowafanya watu kutumia vitisho au kudanganya ni kwa sababu matokeo unayaona haraka. Lakini kwenye ushawishi huu wa mtu kuchukua hatua mwenyewe, hutayaona matokeo haraka. Unahitaji uvumilivu, unahitaji kurudia tena na tena na tena mpaka watu wakuelewe na kuchukua hatua.

Uzuri ni kwamba wakishaelewa na kuchukua hatua, watafanya hivyo kwa maisha yao yote, kwa sababu wamechagua wao wenyewe.

Wafanye watu watake kubadilika wao wenyewe, kwa kuwapa sababu kwa mifano kwa nini wabadilike, na kuwa mvumilivu kwenye hilo.

Nakutakia kila la kheri katika kuwawezesha watu kubadilika.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)