Habari ya wakati huu mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema katika kutimiza majukumu yako ya kila siku na hatimaye kujenga taifa imara. Maendeleo yako yanaletwa na wewe mwenyewe na taifa letu linajengwa na mimi na wewe katika yale mambo ambayo tunayafanya kila siku kwenye kazi zetu. Kiongozi pekee katika maisha yako anaweza kukuletea mabadiliko ni wewe mwenyewe. Wala usitegemee serikali ndio itakuletea mabadiliko au kiongozi fulani. 
 
Hakuna mtu anayefikiria maisha yako zaidi ya wewe mwenyewe. Ukiendelea kusubiria kiongozi au serikali ikufanyie mabadiliko utakua unachelewa kwenye kila kitu katika maisha yako. Aliyekuwa gavana, mwigizaji na raisi wa awamu ya 40 wa Marekani Ronald Reagan aliwahi kunukuliwa akisema ‘’ Government is not solution to our problem; Government is the problem’’ akiwa na maana ya kwamba ‘’serikali siyo suluhisho la matatizo yetu; Serikali ni matatizo’’ kama ulikuwa hujui ukweli kuhusu hili ukweli ndio huu sasa. Kama ulikuwa hujui jua leo na amka na badilika.

Ndugu msomaji, hutakiwi kumlalamikia mtu yeyote wala kumlaumu mtu yeyote kwa maisha uliyo nayo sasa hivi. Jambo muhimu unalotakiwa kufanya ni kuchukua hatua na kuboresha pale ambapo panahitajika kuboreshwa.
Habari njema ni kwamba ndugu msomaji, leo tutakwenda kumjua ‘staa’ au mtu muhimu sana wa kumfuatilia kila siku katika maisha yako ili kuishi maisha sahihi. Na kama unajiuliza maswali mengi katika akili yako je ni ‘staa’ gani au mtu muhimu unayepaswa kumfuatilia katika maisha yako jibu la swali lako utalipata hapa endelea kusoma mpaka mwisho.

SOMA; Hawa Ndiyo Watu Muhimu Sana Wanaoleta Mabadiliko Katika Jamii Yetu.

Siku hizi watu wamekuwa wakifuatilia mambo ambayo hayana mchango kwao na kuamua kufuatilia watu ambao siyo sahihi katika maisha yao. Mtu muhimu au staa muhimu unayepaswa kumfuatilia katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Ni bora kutumia nguvu na juhudi ulizonazo katika kufuatilia maisha ya watu wengine na kuelekeza juhudi na nguvu zako katika kuboresha maisha yako.

Ni utumwa kila siku ukiamka na kuanza kufuatilia leo msanii fulani amevaa nguo gani? Ameweka picha gani?, ameposti kitu gani, anatoka na nani au uhusiano wao umekuwaje ni kupoteza muda na nguvu zako bure. Badala ya kufuatilia mahusiano ya mastaa fulani katika maisha yako na anza kujifuatilia wewe mwenyewe katika maisha yako kwani wewe ndio staa wa maisha yako. Tumia muda na nguvu zako katika kufuatilia maisha yako na hapo ndio utaona mabadiliko katika maisha yako. Una mambo mengi ya kujifuatilia katika maisha yako, kujichunguza na kujitathmini kila siku. Watu wanatafuta muda wa kufuatilia maisha yao na siyo kutafuta muda wa kufuatilia maisha ya watu wengine. Wewe ndiyo staa pekee unapaswa kujifuatilia kila siku katika maisha yako.

Maeneo matatu muhimu unayopaswa kujifuatilia kila siku kabla ya kufutilia ya watu wengine ni kama ifuatavyo; unatakiwa kujifuatilia kila siku na kujitathimini kimwili, kiroho na kiakili. Jiulize kila siku maisha yako ya kiroho yako katika hali gani? Kila siku ni siku bora na mpya katika maisha yako ya kukua kiroho. Kaa katika hali ya ukimya yaani mahali palipo tulia anza kutafakari maisha yako, tafakari maisha yako wapi umetoka na wapi unakwenda? Kabla ya kuhukumu watu wengine jihukumu kwanza wewe mwenyewe. Usiwe mtu wa kuyahukumu maisha ya watu wengine anza kujihukumu kwanza wewe je wewe uko katika njia sahihi? Hakuna mtu ambaye amekamilika kuliko mtu mwingine ukisema umekamilika basi unajidanganya mwenyewe. Endelea kukua katika sekta hii na kumfuatilia staa muhimu katika maisha yako ambaye ni wewe mwenyewe.

Fanya tafakuri na siyo tafakari katika kujichunguza maisha yako ya kimwili yanaendaje. Kuna tofauti kati ya kutafakari na kutafakuri. Kutafakari ni kutafakari kwa kina na kutafakuri ni kutafakari kwa undani zaidi yaani unachimba kiundani kwa kingereza unaweza kusema ‘indeep’’ je unapata muda wa kufanya mazoezi? Unakula vyakula bora vinavyojenga mwili wako na kukupa kinga dhidi ya magonjwa? Unapata muda wa kutosha wa kupumzika yaani muda wa kupumzisha mwili wako ili kuamka na nguvu mpya? Mwili wako nao unahitaji mapumziko siyo kufanya tu kazi bila kujali afya. Jali afya kwanza kwani kazi unayofanya haiwezi kufanyika kama afya yako ikiwa mbovu. Kuna mambo mengi ya kujifuatilia katika maisha yako kabla ya kumfuatilia mtu mwingine. Unafuatilia malengo yako uliyojiwekea? Unafanya kazi zako kwa ubora na ufanisi? Unaongeza thamani katika eneo lako la kazi ulilopo? Kwa hiyo, chunguza na kutafakari kwa undani zaidi juu ya maisha yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; START WITH WHY, Jinsi Viongozi Wakubwa Wanavyohamasisha Watu Kuchukua Hatua.

Hazina ya akili yako ni maarifa. Je una maarifa ya kutosha katika akili yako? Unatakiwa kutumia muda wako katika kukua kiakili. Hakikisha unapata muda kila siku wa kulisha akili yako maarifa ya kutosha. Usipende kufuatilia habari hasi kwani habari hasi moja ina zaa hasi nyingine. Pendelea kuingiza habari chanya katika ubongo wako kwani ndio hazina ya akili yako. Badala ya kufuatilia habari za udaku fulani kafanya nini anza kujifuatilia umesoma vitabu vingapi na vinakusaidiaje kuboresha maisha yako. Maisha ni muda na ni marefu kama ukitumia muda wako vizuri. Tafuta maarifa chanya kwa faida ya maisha yako na ishi maisha yako kwa faida yako.

Mwisho, mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema maisha ambayo hayachunguzwi ni maisha ambayo hayana thamani kuishi. Hivyo basi, ni vema kuchunguza maisha yako kila siku na kujihukumu mwenyewe kabla ya kuhukumu mwingine. Mwandishi Makirita Amani aliwahi kuandika hivi katika ukurasa wa 481; jifukuze kwanza wewe mwenyewe. Usisubiri mpaka ufukuzwe bali jifukuze wewe mwenyewe ili uweze kuwa bora zaidi.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com