TAO TE CHING kwa matamshi ni DAO DE JING ni kitabu ambacho kinaeleza kwa undani falsafa ya Uchina inayojulikana kama TAOISM kwa matamshi DAOISM. Taoism ni falsafa ya zamani sana ya china ambayo imekuwa ikichukuliwa kama dini. Falsafa hii ilitoa mwongozo kwa watu jinsi ya kusihi maisha yanayoendana na sheria za asili za dunia.

Falsafa hii imekuwepo kwa muda mrefu kabla haya ya falafa na dini nyingine kama ukristo na uislamu. Kupitia falsafa hii, msisitizo unawekwa kwamba kama kila mtu ataishi kama sheria za asili zinavyotaka maisha yaende, basi tutakuwa na dunia bora. Neno Tao limekuwa likichukuliwa kama njia iliyo sahihi, au msingi wa kufanya jambo fulani.

Kuna mambo mengi kuhusu maisha tunayoweza kujifunza kupitia falsafa hii. Leo kupitia uchambuzi wa kitabu hiki TAO TE CHING nitakwenda kukushirikisha yale muhimu. Angalia jinsi unavyoweza kuyatumia kwenye maisha yako ili kuwa bora sana. Kumbuka huna haja ya kuipokea falsafa hii kama ilivyo, au kuamini kila kitu kilichopo kwenye falsafa hii, badala yake unachagua yale yanayoendana na maisha yako.

Kitabu hiki kimeandikwa zaidi ya miaka 500 kabla ya kuja kwa Kristo, lakini mafundisho yake yanatufaa sana kwa dunia ya sasa. Hapa kuna madini yenye karibu miaka elfu 3 lakini bado yanatufaa kwenye maisha yetu ya sasa.
Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

1. Ili kuwa na maisha bora, unahitaji kufanya yale yanayoendana na asili ya dunia. Ukizingatia sheria za asili utafanikiwa, ukienda kinyume na sheria za asili utakutana na ugumu. Kama ilivyo unahitaji kupanda ndiyo uvune, ukivuna kabla hujapanda, utajikuta kwenye wakati mgumu.

2. Uzuri na ubaya vyote vina asili moja. Panapokaa uzuri ndipo panapokaa ubaya. Hivyo mtu hawezi kuwa mzuri na mbaya kwa wakati mmoja, ni lazima achague kuwa mzuri au kuwa mbaya.

3. Kitu chochote ambacho ni kigumu sasa, kuna wakati kilikuwa rahisi. Na kwa mantiki hiyo, kitu unachoona ni rahisi sasa, baada ya muda kitakuwa kigumu. Hivyo kuwa makini na vitu rahisi unavyovichukulia poa sasa, vitakuja kuwa vigumu na vikushinde.

4. Kadiri unavyokazana kupata kitu au kuonekana na wengine, ndivyo unavyozidi kukosa kitu hiko. Yaani kama unakazana kuwafanya watu wakuone wewe ni mwema, hawatakuona mwema. Huhitaji kulazimisha vitu, unahitaji kufanya kilicho sahihi na utapata matokeo sahihi. Kama unataka watu wakuone mwema, huhitaji kujionesha, unahitaji kufanya mema, kila wakati bila ya kujali watu wanakuona au la.

5. Ni bora kuwa kama maji, maji ndiyo kitu chenye nguvu kubwa sana duniani. Na sababu hiyo ni kuwa tayari kubadilika. Maji huwezi kuyapasua kwa jiwe, kwa sababu ukiyapiga na jiwe yanabadili muundo wake. Lakini ukipiga jiwe kwa jiwe, yanapasuana. Maji yanaweza kupenya kwenye uchochoro wowote. Kuwa tayari kubadilika kama maji, endana na mazingira yoyote unayojikuta upo, na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

SOMA; Njia Mbili(2) Rahisi Unazoweza Kuzitumia Kutengeneza Kipato Kupitia Mtandao Wa Intaneti.

6. Sema kila unachoweza kukisimamia, na simamia unachosema. Simamia au ongoza wengine kwa usawa, fanya unachofanya kwa ubora, fanya mambo yako kwa wakati. Usilalamike wala kulaumu wengine. Hii ndiyo njia ya asili, ifuate.

7. Watu wanapoacha njia ya asili (Tao) ndipo mabaya yanapowakuta, watu wanadhulumiana na taifa kuangamia. Kama kila mtu ataifuata njia ya asili, tutaishi kwa amani na kushirikiana.

8. Kujisifu hakutakufanya ufanikiwe, kuonesha vile ulivyonavyo hakukufanyi uwe na maisha bora. Kujiona wewe ndiyo bora siyo njia nzuri ya kuongoza. Kufanya hayo yote ni kuenda kinyume na njia ya asili.

9. Hakuna kitu chochote unachoweza kukidhibiti kwenye dunia hii. Hivyo kujaribu kudhibiti vitu ni kujiweka kwenye nafasi ya kuumia. Fanya kwa kadiri ya uwezo wako, lakini jua kuna vitu vingi huwezi kudhibiti, hivyo kuwa tayari kupokea matokeo utakayopata.

10. Usitake kufanikiwa kwa kuwaangusha wengine, usifurahie kuanguka kwa wengine kunakokuweka wewe juu. Fanikiwa kwa juhudi unazoweka kwenye kile unachofanya, na siyo kwa kuwarudisha wengine nyuma.

11. Kuwaelewa wengine kunakufanya uwe na busara, kujijua wewe mwenyewe unakuwa umefikia kwenye kiwango cha juu kabisa cha uelewa. Kuwashinda wengine unahitaji nguvu, kujishinda wewe mwenyewe unahitaji mamlaka/utawala. Wajue wengine, lakini muhimu zaidi jijue wewe mwenyewe vizuri.

12. Kuna watu wanaonufaika kwenye kupoteza na kuna watu wanaopoteza kwenye kunufaika. Yaani hali yoyote ile inayotokea iwe nzuri au mbaya, kuna watu wanapata matokeo yasiyotegemewa. Yaani wakati ambao mambo ni magumu kuna watu wananeemeka, na katika wakati ambapo mambo ni mazuri kuna ambao wanataabika. Ukitaka kuneemeka hata pale mambo yakiwa magumu, fuata njia ya asili.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Matumizi Mabaya Ya Mtandao Wa Intaneti Na Kutumia Vizuri Muda Wako Kujiongezea Kipato.

13. Kila kitu kinapaswa kuwa na kiasi, ili kuwa na maisha bora, na uweze kuishi kwa muda mrefu, jua kipi ni kiasi kwako, jua ni wakati gani wa kuacha, usitake kupata kila kitu, usitake kushinda kila kitu, wakati mwingine acha na utanufaika zaidi.

14. Using’ang’ane na vitu ili watu wakujue kwa vile ulivyonavyo. Bali ng’ang’ana na kufanya ili watu wakujue kwa sifa zako. Utakapoondoka hapa duniani, hakuna atakayehadithia ulimiliki nini bali watu watahadithia ulibadilije maisha ya wengine. Chochote unachofanya, hakikisha unaongeza thamani kwa wengine.

15. Kadiri sheria zinavyokuwa nyingi, ndivyo wahalifu wanavyokuwa wengi. Kadiri vizuizi vinavyokuwa vingi ndivyo watu wanavyokuwa na maisha ya hovyo. Kadiri taifa linavyokuwa na silaha kubwa, ndivyo taifa hilo linavyokuwa ovu.

16. Jipange kwa ugumu wakati mambo ni rahisi, dhibiti makubwa wakati yakiwa bado ni madogo. Mambo yote magumu yanaanza kwa urahisi, na yale makubwa yanaanzia kwenye udogo. Unapoona mambo ni rahisi sana, jua kuna wakati utakutana na ugumu, jiandae mapema.

17. Safari ya maili mia moja inaanza na hatua moja. Ghorofa kubwa imejengwa kwa matofali. Hivyo chochote kikubwa unachotaka, unahitaji kuanza kwa hatua ndogo mpaka kuja kukipata. Usikate tamaa.

18. Kuna hazina tatu muhimu unazoweza kuzitumia kwenye maisha yako ili yawe bora;
Hazina ya kwanza ni huruma, kuwa na huruma kwa wengine.
Hazina ya pili ni kutokutumia zaidi ya unachopata, wengine wanaita ubahili.
Hazina ya tatu ni kutokwenda kinyume na sheria za asili.

19. Watu wanapoona hawashurutishwi kufuata kitu, wanachagua kukifuata wao wenyewe. Asili ya watu ni kupinga, hivyo unapolazimisha watu wafanye kitu, watakataa kufanya kwa sababu hawataki kulazimishwa. Lakini unapowafanya wachague kufanya wenyewe, wanafanya bila ya shida. Wape watu sababu, usiwalazimishe.

20. Maneno ya kweli siyo ya kufurahisha. Maneno yanayofurahisha siyo ya kweli. Vitu vizuri haviwavutii watu, na vitu vinavyowavutia watu siyo vizuri. Watu wenye busara siyo waliosoma, na waliosoma siyo wenye busara. Vitu vinavyoonekana kwa nje ni tofauti kabisa na vilivyo kwa ndani. Usidanganyike kwa kuona kwa nje, mara nyingi unachoona nje ni tofauti na kilichopo ndani.

Ni imani yangu mpaka sasa una falsafa ya maisha yako, kwa sababu maisha bila ya falsafa hayana mwelekeo wowote. Haya uliyojifunza leo, ongeza yanayofaa kwenye falsafa yako. Na kama mpaka sasa huna falsafa ya maisha yako, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz na ujiandikishe ili uwe unapokea makala za FALSAFA MPYA YA MAISHA kila siku ya jumapili.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita