Ni kitu ambacho wote sasa tunajua ya kwamba huwezi kufanikiwa kama unafuata kundi la watu. Hii ina maana kwamba kama unaendesha maisha yako kama kila mtu anavyoyaendesha, kwa kufanya kile ambacho wengi wanafanya na kwa namna wanavyofanya, itakuwa vigumu kwako kufikia mafanikio makubwa.
Kwa nini?
Kwa sababu watu wengi hawapendi kuteseka, watu wengi hawapendi kujisumbua, watu wengi ni wavivu kwa asili. Na mafanikio hayataki tabia hizo. Mafanikio yanataka mtu ajitume, aende hatua ya ziada, aweke juhudi kubwa ili kupata kile ambacho anakitaka.
Hivyo basi yeyote ambaye anataka kufanikiwa, kwanza inabidi ajiondoe kwenye kundi, aanze kuweka juhudi kwenye kile alichochagua kufanya na kutokukata tamaa.
Changamoto inakuja unaondokaje kwenye kundi?
Ni rahisi, huhitaji kugombana na mtu au kumkimbia mtu ili usiwe kwenye kundi. Badala yake unahitaji kufanya maamuzi muhimu sana. Maamuzi hayo ni kuacha kuchukulia vitu kirahisi.
Wengi wanaishia kwenye kundi pale wanapoanza kuchukulia mambo kirahisi. Unakuta mtu anaingia kwenye biashara akiwa na hamasa kubwa lakini baada ya muda anafanya kama ambavyo kila mtu anafanya. Au mtu anaajiriwa na kuingia na hamasa kubwa, lakini muda siyo mrefu anakuwa anafanya kwa kawaida kama kila mtu anavyofanya.
Yote haya huwa yanaanza pale mtu anapochukulia mambo kirahisi, anapoona hakuna haja ya kuweka juhudi kubwa, ni bora kufanya kama wengine wanavyofanya. Na hapa ndipo ndoto zote kubwa zinapoishia.
SOMA; NENO LA LEO; Umuhimu Wa Kuchepuka…
Usikubali kuchukulia mambo kirahisi, endelea kufuata mawazo yako, endelea kuishi ndoto yako hata kama kila mtu anafanya tofauti. Usipokata tamaa, utapata matokeo makubwa unayotarajia.
Simama imara na usiangukie kwenye kundi kwa kuchukulia mambo kirahisi.
Kama hutaki kubaki kwenye kundi, acha kuchukulia mambo kirahisi.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)