Kwa macho ya juu juu kila kitu unachoambiwa kinaonekana ni sahihi na kizuri. Bila ya kuwa makini na kuchimba kwa ndani, huwezi kupata ukweli wenyewe.
Kwa kuchukulia mambo kwa juu juu unaona yanakufaa na bora kwako, lakini unapoingia ndipo unagundua ya kwamba kuna vitu hukujua kabla ya kuingia.
Watu wengi wamekuwa wakichukua maneno na ushauri unaotolewa na kila mtu kuhusu kila kitu, na wanapofanyia kazi ushauri wanaopewa ndipo wanagundua ukweli kwamba kuna vingi hawakuvijua.
Kuna ushauri mwingi sana unaotolewa kuhusu biashara, ujasiriamali, kilimo na hata mafanikio. Lakini mara nyingi ushauri huu umekuwa unatolewa kwa upande chanya pekee. Kwamba fanya biashara fulani na utapata faida ya mamilioni. Au lima zao fulani na utapata faida ya mamilioni. Kwa jinsi inavyoelezwa unapata hamasa kwamba ni fursa nzuri.
Lakini utakapochimba ndani na kutaka kujua changamoto ndipo utakapopata ukweli kwamba siyo rahisi kama ambavyo uliambiwa awali. Utaona namna ambavyo unahitaji kujipanga na kuvumilia ili kuweza kufanikiwa kwenye chochote unachotaka kupata.
SOMA; Usifanye Maamuzi Yako Kwa Kigezo Hiki, Utajuta Sana…
Usichukulie kitu chochote kwa juu juu, chimba ndani zaidi, hoji zaidi ili upate taarifa za kutosha ndipo uweze kufanya maamuzi sahihi. Kwa kuchukulia juu juu hata taarifa ndogo utaiona ni sahihi, lakini itakupoteza pale utakapochukua hatua.
Mbinu ya mwisho ambayo nataka kukushirikisha rafiki yangu kwenye hili ni hii; usikimbilie kufanya maamuzi, na wala usilazimishwe kufanya maamuzi. Kama mtu anakuambia chukua hatua sasa kwa sababu ukichelewa unaikosa fursa, usikimbilie kufanya maamuzi kama bado hujapata taarifa za kutosha. Ni bora fursa ikupite kuliko kufanya maamuzi ukiwa huna taarifa za kutosha, itakugharimu sana.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)