Kwenye dunia ya sasa, haijalishi unajua nini bali unamjua nani. Hii ina maana kwamba mahusiano yako na wengine ni muhimu sana. Kupitia wengine ndiyo unaweza kupata fursa nzuri za kuweza kufikia malengo yako. hivyo unahitaji kuwajua na kujulikana na watu wengi.

Wanasema utajiri wako ni sawa na idadi ya watu wanaokujua. Kadiri unavyojulikana na wengi ndivyo inakuwa rahisi kwako kushirikiana nao katika yale ambayo unayafanya.

Kutokana na umuhimu huu wa kujulikana na wengine, wengi wamekuwa wanatumia njia rahisi ya kujulikana, ambayo siyo sahihi. Njia hii ni kuwa mtu wa maneno, mtu wa kujisifia kwa mambo mbalimbali. Njia hii siyo nzuri kwa sababu kila mtu anaweza kuongea, kila mtu anaweza kujisifia kwa lolote na hivyo watu wanachoka kusikiliza maneno ya aina hii.

Watu wengi wamekuwa wanatafuta njia za kujipendekeza kwa wengine, hasa wale wenye madaraka na mamlaka ili wawajue na kuwaona. Lakini hata kwa kufanya hivi wamekuwa hawatengenezi mahusiano bora, kwani watu hao husahau haraka sana kuhusu kile ambacho wengine wanawaambia kuhusu wao.

Kuna njia moja nzuri na ya uhakika ya kukufanya wewe ujulikane na wengine. Kwa njia hii utajenga mahusiano mazuri na wengine na watakukumbuka kila mara. Njia hii ni kufanya kazi iliyo bora sana, kutoa matokeo ambayo ni bora na watu hawajawahi kuyapata kwingine. Kwa njia hii wale wanaotaka kile unachofanya watalazimika kukutafuta, na hawana haja ya kusikiliza unachoongea, kwa sababu wanaona unachofanya.

Kazi nzuri na bora inakufanya ujulikane, inakufanya ujitofautishe na wengine, inawavutia wengine kutaka kufanya kazi na wewe. Kwa kufanya kazi iliyo bora na kutoa matokeo mazuri, hutaomba tena kukutana na watu, bali watu wataomba kukutana na wewe.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Getting Results The Agile Way (Mbinu Za Kuwa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Na Kupata Ufanisi Mkubwa.)

Fanya kazi iliyo bora, toa matokeo mazuri sana kiasi kwamba watu hawawezi kukukwepa bali kukutafuta na kufanya kazi mwenyewe. Hiki ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako, kama utajali, kuweka juhudi na maarifa.

Usipoteze muda wako kupiga kelele ili ujulikane, usipoteze muda wako kujipendekeza kwa wengine ili ujulikane, badala yake tumia muda huo kufanya kazi iliyo bora sana, na kila mtu atasikia kuhusu wewe.

Nakutakia kila la kheri.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)