Hakuna ambaye anapenda kuteseka kwenye maisha, hakuna anayependa kuumia. Lakini uhalisia wa maisha upo tofauti kabisa na matakwa yetu, chochote tunachotaka kwenye maisha yetu, kinahusika na kuumia.

Japokuwa watu wengi wamekuwa wakidanganyana kwamba kuna njia rahisi ya kupata kile ambacho wanataka bila ya kuumia, hakuna kitu kama hicho.

Sasa kuna vitu viwili ambavyo vitakuumiza na lazima uchague kimoja ambacho utakubali kikuumize. Hakuna namna tunavyoweza kuepuka vyote kwa pamoja, lazima tuchague kimoja au tukishindwa kabisa tunajikuta tunaumizwa na vyote viwili.

Kitu cha kwanza ambacho kitakuumiza ni nidhamu ya kupata kile ambacho unakitaka. Kama kuna kitu kikubwa ambacho unataka kupata, huwezi kukipata kwa kuendelea kufanya vile unavyofanya sasa, ni lazima ubadilike. Kuna mambo unayoyapenda sasa ambayo itabidi uyaache, na kuna mambo ambayo huyapendi ila hakuna namna ni lazima uyafanye. Nidhamu ya kuweza kuwa na afya bora, kuwa na kipato kikubwa, kuwa na mafanikio inakutaka uwe mkatili kidogo kwa mwili wako na yale ambayo unatamani. Unaweza kuchagua kuteseka na nidhamu au ukakataa kuteseka kwa nidhamu lakini ukateseka kwa….

Kitu cha pili ambacho kitakuumiza ni majuto au kukata tamaa. Kama utakataa kuumia kwa nidhamu sasa, subiri siku zijazo ambapo utaumia kwa majuto na kukata tamaa. Utajuta namna ambavyo ulikuwa na fursa lakini ukashindwa kuzitumia. Na tatizo la majuto ni kwamba yanakuja wakati ambapo huwezi tena kurudi nyuma kurekebisha, na ni mateso ya maisha yako yote.

SOMA; Uhusiano Wa Nidhamu Binafsi Na Mafanikio Makubwa.

Mfano wa haraka;

Unaweza kuchagua kuumia kwa nidhamu ukiwa kijana, utunze kipato chako badala ya kuishi kwa mashindano na wengine, ukabana muda wako na kuanza biashara badala ya kupumzika na wengine, baada ya miaka michache ukawa na biashara imara. Au unaweza kusema unahitaji kula ujana kwani haurudi tena, ukatumia kila unachopata, ukapumzika kama wengine, halafu unapofika uzeeni ukakumbuka muda mwingi uliopoteza na namna ambavyo huwezi kuchukua tena hatua.

Maisha ni kuchagua, wewe unachagua nini? Kuumia kwa nidhamu au kuumia kwa majuto? Maisha ni yako, uchaguzi ni wako. Nakutakia kila la kheri katika kuchagua kilicho sahihi.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)