USHAURI; Jinsi Ya Kutengeneza Biashara Isiyokutegemea Wewe Moja Kwa Moja Na Kupata Uhuru Wa Kibiashara.

Habari za wakati huu rafiki yangu?
Hongera kwa juhudi kubwa unazoendelea kuweka kwenye maisha yako na hivyo kuweza kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha yako. Najua mpaka sasa haupo kama ulivyokuwa hapo awali, kwa kujifunza na kufanyia kazi yale unayojifunza, maisha yako yameweza kuwa bora zaidi.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya kipengele cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia maisha ya ndoto zetu. Kama ambavyo nimekuwa nasema mara kwa mara, changamoto ni sehemu ya maisha yetu, hatuwezi kuzikimbia badala yake tunatakiwa kuzitatua na kusonga mbele. Kama unakutana na changamoto ni dalili nzuri kwamba kuna mambo makubwa unafanya kwenye maisha yako, lakini kama huna changamoto, kuna uwezekano mkubwa hakuna mambo makubwa unayofanya.
Katika makala yetu ya leo ya ushauri, tutakwenda kuangalia namna unavyoweza kutengeneza biashara ambayo haikutegemei wewe moja kwa moja.

Changamoto moja kubwa kwenye biashara ndogo na za kati ni biashara kumtegemea mfanyabiashara moja kwa moja. Hii ina maana kwamba kutokuwepo kwa mfanyabiashara kwenye eneo la biashara, basi biashara inakuwa imefungwa. Na pale mmiliki wa biashara anapoumwa au kupata matatizo, moja kwa moja na biashara yake pia inapata matatizo.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Moja ya malengo na faida za kuanzisha biashara, ni kupata uhuru wa kazi na kipato. Unaanzisha biashara ili uweze kuchagua namna unavyofanya kazi zako na mtu asikuwekee kikomo kwenye kipato chako. Lakini kama biashara yako inakutegemea wewe moja kwa moja, unakuwa hujapata uhuru uliokuwa unafikiria, badala ya kumiliki biashara, biashara inakuwa imekumiliki wewe.

SOMA; Wazo Bora Na Mtaji Pekee Havitoshi Kuifanya Biashara Ifanikiwe, Unahitaji Kitu Hiki Kimoja Muhimu Sana Kwa Mafanikio Ya Biashara Yako.

Je unawezaje kuondoka kwenye kumilikiwa na biashara mpaka kuweza kuimiliki biashara? Hiki ndiyo tutakachojadili na kujifunza kwenye makala yetu ya leo. lakini kabla hatujaingia na kujadili kwa kina, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na hili;

Habari coach? Naomba unisaidie ni namna gani mtu unaweza kutengeneza mfumo bora wa biashara na biashara unaweza kujiendesha bila kukutegemea mmiliki moja kwa moja (kuweza kumiliki biashara sio biashara kukumiliki wewe) kwa biashara ndogo na za kati. Ahsante. Seleman E. M.

Kama ambavyo ametuandikia msomaji mwenzetu hapa, kuna watu wafanyabiashara wengi wadogo na wa kati ambao wamemilikiwa na biashara zao na siyo kuzimiliki biashara zao. Tunafanyaje ili kuondokana na hili, tunajadili kwa kina hapo chini. Karibuni sana tujifunze ili kuboresha biashara zetu na maisha yetu kwa ujumla.

1. Usianze biashara bila ya kuwa na ndoto kubwa.

Sababu moja kubwa inayowafanya wafanyabiashara kubaki kwenye utumwa wa biashara kwa miaka mingi ni ndoto zao za kibiashara. Wengi wamekuwa wakianza biashara kama sehemu ya kutengeneza kipato cha ziada. Kwa hiyo wanapotengeneza kipato hicho cha ziada hakuna kingine kikubwa kinachowasukuma, hivyo wanaishia hapo.
Unahitaji kuwa na ndoto kubwa za kibiashara, unahitaji kuiona biashara yako ikikua na kuwasaidia watu wengi zaidi kuwa n amaisha bora. Ndoto hii kubwa ndiyo itakusukuma na kutengeneza biashara inayojitegemea.

Unaruhusiwa kuanza biashara kidogo, lakini usianze biashara bila ya kuwa na ndoto kubwa. Uzuri wa ndoto ni bure, hakuna anayekutaka ulipie ndoto kubwa ulizonazo, hivyo jiwekee ndoto kubwa za biashara yako, jinsi itakavyokuwa kubwa na kugusa maisha ya wengine.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

2. Tengeneza mifumo ya biashara mapema kabla hata hujaihitaji.
Tatizo jingine kubwa kwenye biashara ndogo na za kati ni kukosekana kwa mfumo wa biashara. Wengi wamekuwa wakifikiria kwamba biashara ni kuuza na kununua, au kutengeneza na kuuza. Hivyo wanapeleka nguvu zao maeneo hayo, wanajikuta wametingwa kila siku, lakini hawaoni hatua kubwa wanazopiga.
Unapoiendesha biashara nzima kama kitu kimoja, biashara haiwezi kujitegemea, kwani ni wewe pekee unayeweza kuielewa biashara hiyo vizuri. Ukiajiri mtu mwingine hawezi kuielewa vizuri kama wewe na hivyo kukutana na changamoto.

Tengeneza mifumo inayoeleweka ya biashara yako, ambapo majukumu kwenye mifumo hiyo yanaweza kupewa watu wengine. Kwa kuanzia na kwa biashara ndogo na za kati, angalau weka mifumo mitatu. Uzalishaji, usimamizi na masoko na mauzo. Kwenye uzalishaji hapa ndipo bidhaa au huduma inaposimamiwa katika manunuzi au matengenezo. Masoko na mauzo hapa ndipo biashara inamfikia mteja wako, usimamizi hapa ndipo shughuli zote za biashara zinaposimamiwa.

3. Ajiri watu bora na waamini.
Kitu kingine kinachowafanya wafanyabiashara wadogo na wakati kuwa watumwa wa biashara zao, ni pale wanapofikiri kwamba hakuna mtu anayeweza kuendesha biashara zao vizuri kama wao wenyewe. Hali hii inawazuia kuweza kuajiri watu ambao wangeweza kuwasaidia kuendesha biashara zao, hivyo kukazana kufanya kila kitu wao wenyewe.

Unahitaji kuajiri wafanyakazi bora, kisha kuwaamini kwamba watatekeleza majukumu yao na kuwakabidhi majukumu hayo. Ukishaajiri haimaanishi ndiyo umemaliza, badala yake unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua maendeleo ya biashara yako yanakwendaje, hasa kwa maeneo hayo ambapo umeajiri.
Muhimu hapa ni kupata wafanyakazi bora, na siyo bora wafanyakazi. Kwa sababu wafanyabiashara wengi, wamekuwa wakiajiri watu ambao wanataka mshahara kidogo, mara nyingi watu hawa wanakuwa siyo bora kwa ukuaji wa biashara yako.

SOMA; Kitu Kimoja Ambacho Watu Wengi Wamekuwa Wanadanganywa Kuhusu Biashara.

4. Usiajiri mtu, ajiri nafasi.
Hapo juu tumeshaona kwamba unahitaji kuajiri watu watakaoweza kukusaidia kuendesha biashara yako. Hapa tutaangalia jambo moja muhimu sana katika kuajiri, kwa sababu hapa ndipo makosa makubwa sana yamekuwa yanafanywa na kuwaathiri wafanyabiashara wengi.

Wafanyabiashara wadogo na wa kati, wamekuwa wanaajiri mtu. Yaani wanamwajiri mtu, halafu akifika kwenye biashara ndiyo wanamfikiria anaweza kufanya shughuli zipi. Hii ni hatari kubwa kwa sababu siku akiondoka, ni vigumu kumpata mwingine kama yeye na hivyo biashara yako inatetereka.

Katika kuajiri, usimwajiri mtu halafu akifika ndiyo uangalie anaweza kufanya nini, badala yake ajiri nafasi za kazi. Yaani mwajiri mtu ukiwa tayari una majukumu ambayo anapaswa kuyatimiza, kulingana na mfumo wa biashara yako. unaweza kuajiri mtu kwa ajili ya uzalishaji, au masoko na mauzo na kadhalika. Muhimu ni kuhakikisha mfanyakazi anayajua majukumu yake kwenye biashara yako, na hata watakapotaka kuondoka, unaweza kupata wengine wa kuziba pengo lao.

5. Gawa majukumu yako kwa wengine.
Changamoto kubwa sana kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ni kung’ang’ania kufanya kila kitu wao wenyewe. Wakati mwingine wanafanya hivi wakiamini wanaweka ubora zaidi, wakati mwingine wanafanya hivi kuepuka gharama za kuwalipa wengine.

Lakini kuna vitu viwili ambavyo una uhaba navyo na ni muhimu sana kwako, muda na nguvu. Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani ya kufanya shughuli zako, kuna masaa 24 pekee kwenye siku yako, huwezi kuongeza hata dakika moja. Pia kadiri unavyofanya mambo mengi, mwili wako unachoka na nguvu zinatumia.

Kuondokana na hali hii, orodhesha majukumu yako yote kisha angalia ni majukumu yapi ambayo yanakuhitaji wewe kweli. Yale mengine ambayo kuna watu wanaweza kuyafanya vizuri, watafute watu hao na wayafanye. Siyo lazima uwe umeajiri watu hao, unaweza kuwapa wakufanyie kama vibarua au kwa mikataba maalumu.

Lengo kuu la kuanzisha biashara ni kupata uhuru wa kipato na muda, sasa kama biashara inakuwa inakutegemea wewe moja kwa moja, bado hujaweza kutengeneza uhuru wako kwenye muda na kipato. Fanyia kazi haya tuliyojifunza hapa na utaanza kuona mabadiliko kwenye biashara yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: