Moja ya vitu unahitaji ili kuwa na maisha ya mafanikio, ni kuweza kudhibiti hisia zako, hasa kudhibiti hisia za hasira. Hisia za hasira zina nguvu kubwa na zinaweza kuharibu misingi yote ambayo umeshaijenga kwa ajili ya mafanikio.
Wakati unafanyia kazi kudhibiti hasira zako, kama bado hujaweza kuzidhibiti, kuna mambo mawili muhimu kuyafanya ili usijikute kwenye hali ya hasira itakayopelekea kuharibu utulivu wako.
Jambo la kwanza ni kukaa mbali na zile hali zinazokuletea hasira. Ni muhimu ujijue wewe mwenyewe ni mambo gani ambayo yanakukasirisha haraka. Ukishayajua jitahidi kukaa nayo mbali, hata kama ni muhimu kaa nayo mbali kwa sasa wakati ukifanyia kazi kudhibiti hasira zako. Kama kuna watu ambao ukikaa nao wanakuletea hasira, punguza muda unaokuwa nao. Kama kuna mijadala au mazungumzo ambayo ukishiriki unapata hasira, kaa nayo mbali. Kwa njia hii utajiweka mbali na vichocheo vya hasira, wakati unafanyia kazi kudhibiti hasira zako.
Jambo la pili ni kufunga mdomo wako, kukaa kimya. Hii ni muhimu pale ambapo umeshajikuta kwenye hasira na unataka kuchukua hatua. Unapokuwa kwenye hali hii, kaa kimya, usiseme chochote, na usikimbilie kufanya maamuzi yoyote. Jipe muda wa kutafakari jambo lililokupa hasira, au achana nalo kabisa na njoo lifikirie baadaye, ukiwa umeshapumzika. Katika kukaa kimya pia unaweza kupumua kwa utulivu, hii itakusaidia kushusha hasira zako.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kwa Nini Hisia Bado Zinatushinda Kudhibiti Na Namna Ya Kuzidhibiti.
Usikubali hasira zikutawale, usiongee hovyo pale unapokuwa na hasira, na mara zote jitahidi kukaa mbali na mazingira, hali au watu wanakusababisha ukasirike. Huku ukiendelea kufanyia kazi udhibiti wa hasira zako.
Kesho tutajifunza jinsi ya kudhibiti hasira zetu ili ziache kuwa kikwazo kwenye mafanikio yetu.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)