Chochote unachotaka kujua, tayari kipo mbele yako, chochote ulichokosa ili kufikia malengo yako, kipo hapo ulipo.
Hakuna siri yoyote, hakuna chochote kilichofichwa, kila kitu unacho, au unaweza kukipata na kukifikia.
Kitu ambacho watu wengi wanakosa ni umakini, hatupo makini kuangalia kile ambacho tunakitaka. Tunazifunga akili zetu kwa kuamini kwamba tunachotaka kipo mbali au hatukiwezi sisi. Akili zetu zinapumzika na tunaendelea kubaki pale tulipo.
Leo hii nataka kukuambia AMKA, amka uanze kuangalia kwa umakini, amka na uanze kujiuliza vipi kama…
Vipi kama hicho unachoona ni kikwazo kwako sasa kikawa siyo kikwazo?
Vipi kama kuna njia mbadala ya kufika pale unapotaka?
Angalia hata wale waliofanya, ambao walianzia kama pale unapoanzia wewe, walifanya vipi na kutumia mbinu zipi?
Nakuambia wazi kabisa, hakuna chochote ambacho kimefichwa, kila kitu kipo wazi, ni wewe tu hujawa makini kuangalia, ni wewe tu hujawa na shauku ya kutafuta.
Tena tuna bahati kubwa ya kuishi zama hizi za taarifa, ambapo kila taarifa unayoitaka inapatikana kwenye viganja vyako. Unachohitaji ni wewe kuzitafuta, maana taarifa hazitakufuata hapo ulipo wewe.
Unataka kuanzia biashara mpya? Vizuri angalia unawezaje kuanzia hapo ulipo sasa.
Unataka kukuza biashara uliyonayo sasa? Safi sana, angalia hapo ulipo sasa, wateja ulionao sasa na bidhaa au huduma unazotoa sasa, ni kwa namna gani unaweza kufanya zaidi ili kukuza biashara yako zaidi.
SOMA; UKURASA WA 05; Anzia Hapo Ulipo, Anza Na Ulichonacho.
Chochote unachofikiria kufanya kwenye maisha yako, anzia hapo ulipo, paangalie vizuri, kuna njia nyingi sana unazoweza kuzitumia hapo ulipo sasa, na zikakufikisha kule unakotaka kufika.
Nimalize kwa kusema rafiki yangu, chochote unachotaka, unaweza kukipata ukianzia hapo ulipo sasa, hakuna siri, hakuna kilichofichwa, ni wewe kuongeza umakini ili kupata kile unachotaka. Maarifa yapo ya kutosha, ni wewe kuyatafuta na kuyafanyia kazi.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)