Habari za leo rafiki? 
Karibu tena kwenye mtandao wetu wa AMKA MTANZANIA ambapo tunajifunza mambo mbalimbali ambayo yanatuwezesha kuwa na maisha bora zaidi kila siku. Kama ambavyo tunajua, kila siku ni siku ya kujifunza, hakuna siku ambayo mtu utaamka na kusema tayari nimeshajua kila kitu. Kila siku kuna changamoto mpya na hivyo kujifunza kila siku ni muhimu.
Kwenye makala yetu ya leo, tunakwenda kuangalia njia bora ya kuepuka majungu na kukatishwa tamaa kwenye eneo lako la kazi. Hakuna sehemu ambazo zimekuwa na majungu kama sehemu za kazi, hakuna sehemu ambazo zimewakatisha watu tamaa, kuua ndoto zao na kuwafanya wawe kawaida kama sehemu ya kazi.

Ukikutana na mtu ambaye ndiyo anaanza kazi anakuwa na hamasa kubwa sana, anakuwa na mipango ya jinsi atakavyoitumia kazi hiyo kufanya makubwa kwenye kazi na kwenye maisha yake pia. Anakuwa amejipanga vizuri sana. Lakini baada ya kuanza kazi, ile hamasa yote inapotea, mipango yote mikubwa inayayuka na anaishia kuwa kawaida, kama walivyo wafanyakazi wengine.

Ukichunguza sababu kubwa zinazowafanya watu wachukie kazi zao, sababu inayopolekea wengi kuwa na msongo wa mawazo kwenye kazi zao, ni kutoka kwa wafanyakazi wenzao. Kwa kuwa mtu anatumia karibu nusu ya muda wa maisha yake kwenye kazi, wale wanaomzunguka kwenye kazi wana ushawishi mkubwa kwake.

 

Kumekuwa na majungu na ukatishwaji tamaa mkubwa sana kwenye maeneo ya kazi. Pale mtu anapojitahidi kufanya kazi yake vizuri, anaonekana ni kiherehere au anajipendekeza kwa bosi. Wengine wanamwambia usijisumbue, hayo makubwa unayofikiria hapa haiwezekani. Na wanaotoa maneno kama haya ni wale wazoefu kwenye kazi hiyo, ambayo wamekaa pale kwa muda mrefu. Ni vigumu sana kuwapinga watu hao kwa sababu ya ugeni wa mtu na uhalisia kwamba kama mtu amekaa kwenye kazi hii kwa miaka 20 anajua mengi kuliko mimi ambaye hata mwaka sina. Kwa kufikiri hivi, wengi wamekuwa wanaishia kukata tamaa.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuepuka Majungu Kwenye Eneo La Kazi

Leo nataka nikuambie ya kwamba, hupaswi kukata tamaa, hupaswi kuwasikiliza wale wanatoa majungu, hata kama ni aliyekuajiri, unachohitaji kufanya wewe ni kimoja pekee, fanya kazi iliyo bora, kulingana na ujuzi wako na uwezo mkubwa ambao upo ndani yako.
Kitu kimoja muhimu unachopaswa kujua ni hiki, huwezi kuwazuia watu kusema kile wanachotaka kusema. Ukikazana kufanya kazi bora watakusema kwamba una kiherehere na kujipendekeza. Ukifanya kazi a hovyo watakusema kwamba ni mzembe na huna ujuzi wa kazi. Kwa vyovyote vile wanaotaka kusema watasema, hivyo ni muhimu wewe ufanye kile ambacho ni sahihi kwako.
Hii ndiyo njia bora kabisa ya kuepuka majungu na kukatishwa tamaa kwenye eneo lako la kazi, fanya kile ambacho ni sahihi kufanya, kila wakati. Na siyo kwamba ukifanya hivi wataacha kutoa majungu na maneno ya kukatisha tamaa, hapana, wataendelea kutoa maneno hayo, lakini kwa kuwa wewe hutawasikiliza na kuacha, watafika wakati watachoka, kwa sababu watajifunza wewe husikilizi, wewe ni mtu wa viwango vyako na hakuna namna wanaweza kukurudisha nyuma. Baada ya muda watu watakuwa wanakuheshimu kupitia kazi yako, na watakuona wewe ni mtu wa tofauti na pekee.

SOMA; Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio.

Rafiki wacha leo nikupe siri moja kuhusu saikolojia ya binadamu, mara zote watu hupinga kile kitu ambacho wao hawawezi kufanya au hawawezi kuwa nacho. Kwa sababu hawataki kuamini kwamba kuna watu wengine wanaoweza kufanya kile kinachowashinda wao kufanya. Hivyo wanatafuta njia ya kuhakikisha mtu hafanyi tofauti na wanavyofanya wao. Siri nyingine kubwa ya kisaikolojia ni kwamba watu huheshimu na wakati mwingine kusujudu kile ambacho kinaonekana ni kikubwa kuliko wao, kile ambacho kinaonekana ni kikubwa kuliko maisha ya kawaida. Sasa hapa ndipo ilipo nafasi ya wewe kutokea, onekana kuwa na uwezo na ufanisi mkubwa kuliko ilivyo kawaida, mwanzoni watafikiri wewe ni viwango vyao, hivyo watajaribu kukupinga na kukukatisha tamaa. Lakini wakigundua hurudi nyuma, moja kwa moja wanaanza kukuheshimu, kwa sababu unakuwa umevuka ile hali ya ukawaida ya binadamu.

Jiwekee viwango vyako mwenyewe na fanya kazi kwenye viwango hivyo, viwe viwango vya juu sana, ambavyo wengine wanaviangalia kwa mbali tu, hawathubutu hata kuvifikiria. Fanyia kazi viwango vyako hivyo na watu wataanza kukuelewa.

SOMA; Kama Utafanya Mambo Haya, Hakuna Tena Wa Kukuzuia Kufanikiwa.

Kitu kingine muhimu sana unapaswa kujua ni kwamba watu wanawaheshimu sana wale watu wanaoonekana kuwa na msimamo. Kama kuna kitu ambacho unakisimamia kwa kujiamini, hata kama siyo kitu sahihi, kuna watu wengi watakuamini na kukuheshimu. Lakini kama kila wakati unabadilika kutokana na watu wanavyokupinga, basi wanakuona wewe huna msimamo na hivyo kukudharau.
Rafiki, nimalize kwa kusema kwamba, majungu na kukatishwa tamaa kwenye maeneo ya kazi ni kitu ambacho hakitaisha kwa wewe kuwasikiliza wale wanaosema, bali kitaisha kwa wewe kuendelea kufanya kile ambacho ni sahihi mara zote. Hivyo basi jiwekee viwango vyako vya utendaji, na visimamie hivyo mara zote. Usiwasikilize watu wanaokushauri jambo lolote ambalo ni tofauti na viwango vyako na siyo sahihi.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)