Pamoja na mapinduzi na maendeleo makubwa kwenye teknolojia, jambo moja bado linabaki kama lilivyokuwa tangu kuwepo kwa dunia hii. Jambo hilo ni KAZI.

Hakuna mafanikio yanayoweza kutokea bila ya watu kufanya kazi, hakuna na hayatakuja kuwepo. Hata kama tunapata mashine bora kabisa za kufanya kazi, bado zinahitaji kuendeshwa na watu, bado zinahitaji kurekebishwa na watu pale zinapoharibika.

Hivyo basi, ambacho nimekuwa nasisitiza kwa sisi wanamafanikio, tuipe kazi uzito wake, tuipe kazi kipaumbele inachostahili, hakuna mafanikio bila ya kazi.

Lakini sasa kuna tofauti kubwa kwenye kazi zetu. Kuna kazi za kawaida na kazi hasa.

Ukifanya kazi za kawaida utapata matokeo ya kawaida na kuwa na maisha ya kawaida.

Ukifanya kazi ya tofauti utapata matokeo ya tofauti na kuwa na maisha bora. Hivyo ndivyo ilivyo, yeyote unayeona maisha yake ni ya tofauti, jua pia anafanya kazi kwa utofauti.

Sasa rafiki, moja ya njia za kufanya kazi yako kwa utofauti, ni kwa kuweka muda mwingi zaidi kwenye kazi yako kuliko wengine wanavyoweka muda. Na hapa ndipo dhana ya WA KWANZA KUINGIA, WA MWISHO KUTOKA inapoingia.

Kwenye chochote unachofanya, iwe ni kazi au biashara, kuwa wa kwanza kuingia na wa mwisho kutoka. Kama upo kwenye ajira, kuwa wa kwanza kufika eneo lako la kazi na wa mwisho kuondoka, kila siku. Kama unafanya biashara, kuwa wa kwanza kufungua na wa mwisho kufunga.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DEEP WORK (Mbinu Za Kufanya Kazi Yenye Maana Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu).

Kwa kufanya hivi watu wanajijengea kwenye akili zao kwamba kama nataka kupata kitu mapema nitakipata sehemu fulani, na kama nataka kupata kitu nikiwa nimechelewa nakipata sehemu fulani. Kama ni kwenye kazi yako, watu wanajua nani wa kutegemewa kama kazi inatakiwa kufanyika mapema.

Ni muda kidogo unaongeza kwenye kazi na biashara yako, lakini matokeo yake ni makubwa sana. Anza kufanyia kazi hili sasa na utaona matokeo makubwa na bora kwenye kile unachofanya.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)