Mara zote matendo yanaongea kwa sauti kuliko maneno. Kuna usemi wa wanafalsafa kwamba matendo yako yanaongea kwa sauti sana kiasi kwamba mtu hasikii kile unachoongea.

Ukweli ni kwama unaweza kupiga kelele utakavyo, unaweza kusema chochote unachotaka kusema, lakini mwisho wa siku watu wataangalia matendo yako. Je unaishi maneno yako? Je unachosema ndiyo unachofanya?

Nina hakika kwenye maisha yako kuna watu ambao unawajua, ambao huwa wanaongea sana lakini kufanya wanayoongea hawafanyi. Unawajua watu ambao wakianza kukuambia mambo unajua wanakupotezea tu muda kwa sababu hawatafanya chochote.

Kama kweli unataka kuwa na maisha bora, kama unataka watu wakuheshimu na kusikiliza kile ambacho unakisema, basi fanya yale ambayo unayasema. Ile misingi ambayo unainadi kwa wengine, anza kuiiishi wewe, ule ushauri ambao unatoa kwa wengine uwe unatokana na maisha ambayo unayaishi mwenyewe.

Hata ndani ya familia zetu, kuanzia wenza wetu mpaka watoto wetu, wameshatusoma na wanajua kama tunamaanisha kweli tunachosema au tunasema tu. Ukiwa mtu wa maneno sana kuliko vitendo unashusha heshima yako, na watu wanaacha kukupa uzito, wanakuchukulia kawaida, kwa sababu wanajua hutafanya. Lakini unapokuwa mtu wa kuyaishi maneno yako, kila mtu anakuheshimu na anachukulia neno lako kama sheria.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Art Of Living(Mwongozo wa kuishi maisha ya furaha na mafanikio.)

Chanzo cha heshima kwenye maisha yako ni kuishi maneno yako, fanya kile ambacho unasema na kushauri wengine wafanye na pia timiza kile ambacho umeahidi. Ni vigumu sana hata kama wewe ni mzazi kumlazimisha mtoto wako afanye kitu fulani ambacho anaona wewe hufanyi. Utatumia nguvu nyingi kumwambia afanye, lakini kama anaona na wewe hufanyi, hatafanya.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maeneo ya kazi na hata ya biashara, kama kuna mabadiliko unataka yatokee, anza kuyaishi mabadiliko hayo, usiyahubiri tu, bali yaishi. Ni rahisi watu kuiga unachofanya, kuliko kusikiliza na kufanya.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)