Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri na unaendelea kuboresha maisha yako kupitia falsafa ambayo umekuwa unajijengea kila siku. Endelea kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku maana kadiri siku zinakwenda, tunapaswa kuwa bora zaidi.
Leo tunakwenda kuangalia jambo moja muhimu sana kwenye maisha yetu, siyo jambo zuri lakini pia hatuwezi kulikwepa. Jambo hili limekuwa linawasumbua watu tangu enzi na enzi na ni wanafalsafa pekee ambao wameweza kuishi kwa furaha kwa kujua ukweli wa jambo hili.
Kabla hatujaingia kuliangalia jambo hili nikupe mfano wa kichekesho kimoja ambacho nimewahi kukisoma mahali fulani.
Kichekesho hicho kinasema kwamba jamaa ameenda kwenye msiba wa rafiki yake kijijini kwao. Sasa utaratibu wa kijiji kile ni kwamba kuna mzee ambaye baada ya mazishi huwa anasema nani atafuatia kufa. Basi baada ya mazishi, mzee akasema atakayeondoka hapa kaburini wa kwanza ndiye atakayefuatia kufa. Baada ya kauli hiyo kila mtu akawa anazunguka kwenye kaburi lile kwa zaidi ya siku tatu, ikiwemo yule mzee aliyetoa tangazo hilo.
Hiki ni kichekesho lakini kimebeba funzo kubwa sana, kwamba hakuna anayependa kufa. Wewe unapenda? Hakuna anayependa kufa, lakini kwa sheria za asili ni kwamba kila chenye uhai ni lazima kitakufa, hakuna anayeweza kukwepa hilo.
Huu ndiyo kweli, kwamba hakuna mtu yeyote kati yetu ambaye anaweza kukwepa kifo. Kifo ni sehemu ya maisha yetu, na kila mmoja wetu atakufa. Tutakufa siyo kwa sababu tutakuwa na ugonjwa, au kwa sababu tutapata ajali, au kwa sababu ya matatizo mengine yoyote, bali tutakufa kwa sababu tunaishi. Hizo nyingine ni njia tu za kukamilika kwa jambo hili ambalo hatuwezi kulikwepa.
Hii ni habari mbaya na ya kusikitisha sana, kwamba pamoja na juhudi hizi kubwa tunazoweka kila siku, siku moja tutakufa, na ndiyo utakuwa mwisho wa juhudi zote tunazoweka sasa.
Tunaweza kuhofu tutakavyo juu ya kifo, lakini hatuwezi kukikwepa. Japo kuna njia za kuepuka hili kutokea mapema, lakini bado kwa sehemu kubwa ni nje ya uwezo wetu. Ndiyo wakati mwingine tunafanya uzembe mkubwa ambao unakaribisha vifo vyetu mapema zaidi, lakini bado kifo hakikwepeki.
Tangu kuwepo kwa maisha hapa duniani, swala la kifo limekuwa mjadala na changamoto kubwa kwa wengi. Je tukifa tunaenda wapi? Je kuna maisha baada ya kifo? Je tunarudi duniani kwa njia nyingine baada ya kufa? Kila imani ya kidini na falsafa imekuwa inakuja na majibu yake kuhusu kifo, kama kutakuwa na maisha baada ya kifo au kurudi tena duniani.
Lakini kuna wanafalsafa ambao wameweza kulipokea hili la kifo vizuri na kuweza kuishi nalo kwa furaha. Hii ndiyo njia ambayo tunakwenda kujifunza kwenye makala ya leo ya falsafa mpya ya maisha.
Unawezaje kuishi maisha ya furaha huku ukijua ya kwamba utakufa?
1. Ishi leo.
Kwenye jamii zetu tumekuwa tunaishi siku nyingine zote lakini siyo leo. Tumekuwa tunaishi jana kwa kuangalia yale ambayo tulifanya au hatukufanya, tunatumia muda mwingi kwenye jana yetu wakati hakuna chochote ambacho tunaweza kubadili. Tumekuwa pia tunaishi kesho yetu, kwa kuwa na hofu juu ya yale yatakayotokea, wakati hata bado hayajatolea. Hii pia imekuwa sehemu ya kupoteza muda wetu.
Ili kuishi maisha yetu vizuri, ni muhimu tukaishi leo. Ishi leo, fanya kile ambacho umepanga kufanya leo. Chochote kinachowezekana kufanya leo kisingoje kesho. unapojifunza kuishi leo, unafanya yale muhimu leo, huku ukijiandaa na kesho yako. Itumie jana yako kama sehemu ya kujifunza, ila ishi leo.
- Kufa mtupu.
Wazungu wanasema DIE EMPTY, yaani hakikisha hakuna kitu kimebaki ndani yako pale unapokufa. Toa kila kilichopo ndani yako, na ufe ukiwa mtupu. Na kwa kuwa hujui siku gani utakufa, basi hakikisha kila siku unakuwa mtupu, hakikisha kila siku unatoa kile ambacho kipo ndani yako. Usibanie chochote ambacho unajua unataka kufanya au unaweza kufanya. Kila siku weka juhudi zako zote kwenye kile ambacho umechagua kufanya, usiguse kitu chochote juu juu. Bali kifanye kwa uwezo wako wote.
- Acha alama.
Wanafalsafa wanasema hujaishi leo kama hujaweza kumfanyia mtu kitu ambacho hawezi kukulipa. Hii ndiyo maana nzima ya maisha, kuwa na mchango chanya kwenye maisha ya wengine.
Kwa chochote ambacho unachagua kufanya, chagua kuacha alama kwa wengine. Acha alama kwa kuyabadilisha maisha ya wengine, acha alama kuwawezesha wengine kuwa na maisha bora kabisa. Na wala huhitaji kuwa na kundi kubwa la watu ili uwasaidie, anza na wale ambao wanakuzunguka, ndugu jamaa na marafiki.
- Kufa kila siku.
Ili uweze kuwa na maisha bora, na uache kufikiria kuhusu kifo chako ni kufa kila siku. Kila siku unayoishi, ichukulie kama ndiyo siku yako ya mwisho kuishi hapa duniani. Kwa kila siku unayoishi, chukulia kwamba ndiyo siku ya mwisho, usiahirishe chochote kwenda kesho, kwa sababu hutaifikia kesho hiyo. Unapopata nafasi ya kufanya kitu, kifanye kama hutakuja kukifanya tena. Unapopata nafasi ya kuongea na mtu, ongea naye kama hutakuja kuonana naye tena.
Kwa njia hii utaweka vipaumbele vyako vya siku vizuri ili uweze kuikamilisha siku yako vizuri. Mara nyingi tumekuwa tunajidanganya kwamba tuna muda wa kutosha wa kufanya yale tunayotaka kufanya. Lakini muda siyo rafiki yetu, tumekuwa tunajikuta hatuna tena muda na tuna mengi ya kufanya. Anza sasa kufa kila siku, na utaishi kila siku kwa kuwa na vipaumbele.
Kukubali kwamba kila mmoja wetu ipo siku atakufa ni hatua muhimu kwetu. Kuchagua kuishi kila siku yetu vizuri ili tutakapokufa tuwe tumeacha alama kwenye dunia hii ni hatua kubwa kabisa kwenye maisha yetu. Tuzingatie haya ili kuweza kuwa na maisha bora kila siku, yenye furaha na mafanikio makubwa, ambayo yanagusa maisha ya wengine pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK