Mafanikio ni haki yako ya kuzaliwa, hiki ni kitu muhimu sana ambacho nataka wewe rafiki yangu ukielewe na ukifanyie kazi kila siku. Asitokee mtu yeyote yule akakuambia kinyume na hayo, labda kuna watu fulani ambao ndiyo wana haki ya kufanikiwa ila siyo wewe. Hiyo siyo kweli kabisa, wewe, hapo ulipo una haki ya kufanikiwa, na kwa kwenda pamoja na mimi, utajifunza yote muhimu unayopaswa kujua ili kufanikiwa.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Nirudie tena hili ambalo nimekuwa nalisema mara kwa mara, na ndiyo ukweli wa maisha, kama hakuna changamoto, hakuna maisha na hivyo hakuna mafanikio. Changamoto ni sehemu ya maisha yetu, hivyo tunahitaji kuzitatua ndiyo tufanikiwe.

KUPATA MAELEZO KUHUSU SEMINA HII BONYEZA PICHA AU MAANDISHI HAYA.

Kwenye makala yetu ya leo tunakwenda kuangalia jinsi unavyoweza kupata wateja wa kudumu kwenye biashara yako na kuweza kuikuza biashara hiyo zaidi. Hii ikiwa ni changamoto ambayo tumeandikiwa na rafiki na msomaji mwenzetu Monie. Karibu usome changamoto hii na ushauri muhimu wa kuzingatia;

Changamoto inayonikabili ni kwamba ninawezaje kupata wateja wa kudumu na jinsi gani ya kukuza ama kutanua biashara ninayotaka kuanzisha? Monie P. P.

Kupata wateja wa kudumu kwenye biashara ni changamoto kubwa sana, na hili ndiyo limekuwa linaua biashara nyingi. Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kuanzisha biashara ndipo mahali pagumu sana, lakini huu siyo ukweli, kuanzisha biashara ni kugumu, lakini kuendesha biashara mpaka ipate mafanikio makubwa, ni pagumu zaidi.

Ukianzisha biashara ni rahisi wateja kuja, wanataka kuja kupima biashara hii mpya ikoje, wanapokuja mara ya kwanza, ndiyo wataamua kama wataendelea kuja tena au hawatakuja tena kwenye biashara yako. Hivyo ni lazima uwe makini sana na uendeshaji wako wa biashara ili uweze kuwa na wateja wa kudumu.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kujua Biashara Inayolipa Eneo Ulipo.

Kumshawishi mteja aje kwenye biashara yako mara ya kwanza inaweza isiwe kazi ngumu, unaweza hata kudanganya ili tu afike, lakini kumfanya mteja arudi tena na tena na tena, na pia awalete wenzake, ni kazi ambayo wewe kama mfanyabiashara unahitaji kuifanya, na siyo kazi ndogo.

Je ni hatua zipi ambazo zitakuwezesha kupata wateja wa kudumu kwenye biashara yako?

1.     Tekeleza kile unachoahidi. Uaminifu ni muhimu.
Kuna mambo mengi ambayo utamuahidi mteja ili aje kwenye biashara yako, labda kupitia matangazo utakayotoa. Kuna sifa ambazo utaipa biashara yako na changamoto za wateja ambazo utasema biashara yako inatatua. Wateja watakuja kwako wakiwa na mategemeo ya kupata kile ulichosema watapata. Kama watafika na kupata, watakuamini na kuja tena na tena. Lakini kama watafika kwenye biashara yako na kupata huduma au bidhaa tofauti na ile uliyowaambia watapata, hawatakuamini na hawawezi kurudi tena.

2.     Nenda hatua ya ziada. Toa zaidi ya ulivyoahidi.
Kutekeleza kile ulichoahidi kila mtu anaweza kufanya hivyo, hivyo inaweza isikutofautishe sana na wafanyabiashara wengine. Kipo kitu kimoja cha kukutofautisha kabisa na wafanyabiashara wengine, na hili ni kwenda hatua ya ziada. Mfanye mteja akija kwenye biashara yako ashangazwe, aone kama anakuibia hivi. Asiamini huduma au bidhaa anazopata kwa bei ambayo amelipia. Angalia namna unaweza kufanya hivi bila ya wewe kupata hasara, na hilo linawezekana vizuri sana kama utaijua biashara yako vizuri.

3.     Usiwe na wateja, kuwa na marafiki.
Najua hapo juu nimekupa mbinu za kuwapata wateja, na hapa nakwenda kinyume kabisa na niliyokuambia hapo juu. Usiwe na wateja, badala yake kuwa na marafiki. Neno mteja linaweza kuwa na tafsiri ya kimaslahi pekee, kwamba huyu ni mteja ninachoaka kwake ni faida. Lakini biashara siyo faida pekee, bali pia kutoa mchango kwenye maisha ya wengine. Wachukulie wateja wako kama marafiki zako, na kama unavyojua, marafiki wanajaliana, hivyo jali kuhusu wateja wako a wao watajali kuhusu wewe. Watakuwa na wewe kwenye biashara yako mara zote.

SOMA; Hii ndiyo changamoto kubwa inayoua biashara ndogo hapa Tanzania.

4.     Usifikirie faida pekee.
Najua unafanya biashara ili upate faida, lakini hili lisiwe lengo lako kuu, kama unataka kujenga wateja wa kudumu kwenye biashara yako. Unapoangalia faida pekee kuna fursa utazikosa za kuwasaidia wateja wako, ambapo watakuthamini mno. Msukumo wa kwanza wa biashara kwako uwe kutoa mchango na thamani kwenye maisha ya wengine, kwa kufanya hivi faida itakuja bila hata ya kutumia nguvu kubwa.  Unapoangalia kuongeza thamani na maana kwenye maisha ya wengine, wanaliona hilo na wanakuamini zaidi. Watakuwa wateja wako wa kudumu.

5.     Tatua changamoto za wateja marafiki zako.
Marafiki wa biashara yako, kuna wakati ambapo watakutana na changamoto kupitia biashara yako. Labda watalipia huduma halafu wasiipate vizuri, au watanunua bidhaa na washindwe kuitumia. Au hata wakati mwingine watafanya makosa fulani ambayo yanawafanya washindwe kutumia au kufurahia bidhaa au huduma waliyonunua kwako. Wasaidie wateja wako kuondokana na changamoto hizo na watakuwa wateja wa kudumu kwenye biashara yako.

Je unawezaje kuikuza biashara yako?
Kwa kuanza na kutoa huduma bora kabisa kwa wateja wako, utakuwa na wateja ambao wanakuamini na kuiamini biashara yako, hii ni hatua muhimu kabisa na ya kwanza ya kukuza biashara yako.

Baada ya kuwa na wateja wa kudumu kwenye biashara yako, kila siku boresha biashara yako, wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kutokana na kufanya kwa mazoea, sasa wewe usiwe hivyo. Badala yake badili na boresha biashara yako kila siku.

Wafikie wateja wengine wa biashara yako kupitia wateja ulionao sasa. Hii ni mbinu muhimu ya kuikuza zaidi biashara yako. Tumia wateja ulionao sasa kuwafikia wateja wengi zaidi. Unaweza kuwaomba wateja hao kuwaambia watu wao wa karibu ili nao wawe wateja wako.

SOMA; Njia tano (5) za uhakika za kuweza kuikuza biashara yako na kufikia mafanikio makubwa.

Mwisho kabisa endesha biashara yako kisasa, usiendeshe kwa mbinu za kizamani. Weka vizuri kumbukumbu zako za kibiashara, kuwa na wafanyakazi waaminifu na wanaojituma na pia kadiri biashara inavyokuwa, wekeza faida kwenye biashara ili iweze kukua zaidi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza ili uweze kuanzisha na kukuza biashara yenye mafanikio, na uweze kufikia ndoto za maisha yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz  

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.