Umewahi kuona mtu anakazana na kazi au biashara kwa muda mrefu, kipato chake kinakuwa kidogo lakini baadaye ghafla kipato chake kinaanza kukua kwa kasi sana? Au huenda imewahi kutokea kwako mwenyewe, unaanza kazi au biashara na unakuwa na kipato kidogo, lakini baada ya muda kipato chako kinakua.

Kwenye kazi au biashara yoyote ile, upo mlango wa kipato kikubwa, mlango huu una ufunguo wake ambao wale wanaoweza kuupata wananufaika, na wale wanaoukosa wanaishia kutaabika. Wanaopata ufunguo huu ndiyo wanaoweza kutengeneza kipato kikubwa.

Vipi kama leo nakupa ufunguo wa mlango huo? Je utautumia kufungua mlango huo wa kipato kikubwa?

Kama jibu ni ndiyo basi karibu uchukue mwenyewe ufunguo wa mlango huu.

Ufunguo wa mlango wa kipato kikubwa ni kujiamini kwenye ule mchango unaotoa. Pale unapojiamini kwa kile unachofanya, iwe ni kazi au biashara, ndipo unapofungua milango ya kipato kikubwa kwenye maisha yako.

Pale unapoweza kusimama na kusema wazi mimi nafanya hiki na hiki, na kuweza kuwahakikishia watu kwamba unaweza kuwapa kile wanachotaka au kutatua changamoto wanazopitia, ndipo unapofungua milango ya kipato kikubwa.

Kwa nini inakuwa hivi?

Iko hivi rafiki, unapoanza kufanya kitu chochote kipya, mwanzoni unakuwa hujiamini sana, tena wakati mwingine unaweza kujistukia. Unaweza kujiuliza kama kweli unaweza kutatua matatizo makubwa ya watu watakayokuletea. Na hata inapofika kwenye kuhitaji malipo, unaogopa hata kutaja malipo makubwa kwa sababu hujiamini sana kwenye kile unachofanya.

Kadiri unavyofanya, unaanza kujiamini kwa jinsi unavyowasaidia watu kupitia unachofanya. Na hapa sasa unaweza kuwaambia watu kwa kujiamini kwamba unaweza kuwapa kile wanachotaka, au kutatua changamoto zao. Na kwa kuwa unajiamini pia utakuwa tayari kudai malipo makubwa yanayoendana na kile ambacho unawapatia watu.

Hivi ndivyo unavyofungua milango ya kipato kikubwa, jiamini kwenye kile unachofanya, na toa mchango na thamani kubwa kupitia kile unachofanya. Unapojiamini na wale wanaokutegemea nao wanakuamini na hivyo kuwa tayari kufanya kazi au biashara na wewe.

Anza kujiamini na amini kwamba mchango wako ni muhimu. Amini unaweza kutoa thamani kubwa kwa wengine, kutatua changamoto zao na kuwapa kile wanachotaka. Utaona jinsi utakavyowavutia wengi kufanya kazi na wewe na kipato chako kuwa bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK