Kuna wakati katika safari ya mafanikio, hujikuta tuna malengo mazuri sana ambayo huamini kabisa yatatufikisha kwenye mafanikio makubwa. Hata hivyo, pamoja na uzuri  wa malengo hayo, hujikuta tena tunaanza kukata tamaa katika kuelekea kutimiza malengo hayo.
Je, umeshawahi kujiuliza ni nini hasa huwa chanzo ama sababu ya wengi kukata tamaa kuelekea kwenye ndoto zao? Kama ni malengo wanayo mazuri, kama ni hamasa wameanza nayo vizuri, je, sababu ipi ya ziada ambayo hupekea wao kukata tamaa ?
Yapo mengi sana ya kujiuliza, lakini kwa kusoma makala haya utajifunza na kupata majibu kwa nini hata wewe unaweza kukata tamaa kuelekea kwenye ndoto zako ambazo ulikuwa unaziamini.
Zifuatazo Ndizo Sababu 4 Kwanini Unakata Tamaa Mapema Kwenye Ndoto Zako.
1. Huamini tena kama utafanikiwa.
Kwa kawaida unapoanza kufanya jambo fulani, unaweza ukawa na matumaini makubwa sana ya kulifanikisha jambo hilo. Hata hivyo jinsi siku zinavyokwenda, pengine kutokana na changamoto za hapa na pale ni rahisi kujikuta unaanza kukosa tumaini la kufanikisha ndoto zako.
Hii ni sababu kubwa sana inayopelekea wengi kushindwa tena kuendelea na ndoto zao. Unapokuwa unakosa imani au matumaini na kile unachokifanya na kuamini kwamba hakiwezi kufanikiwa tena, basi huo ndio unakuwa mwisho wako.
Acha kupoteza tumaini la mafanikio yako.
Suluhisho.
Ng’ang’ania ndoto zako mpaka ufanikiwe. Siri ya mafanikio ipo kwenye kung’ang’ania na kuweka imani kubwa kubwa kwamba kwa vyovyote ni lazima nifanikiwe
2. Kushindwa kuona matokeo ya haraka.
Watu wengi huwa ni wepesi sana wakuacha ndoto zao hasa pale wanaposhindwa kuona matokeo ya haraka. Utakuta mtu kaanzisha mradi fulani mwezi huu, lakini anataka kuona mradi huo ukimzalishia upesi na kumpa faida ya kutosha ndani ya kipindi cha muda mfupi sana.
Ili kufanikiwa, jenga tabia ya kufatilia kitu mpaka uone matokeo yake ya mwisho. Acha kuishia kati na kutaka mafanikio ya haraka. Hakuna mafanikio ya kweli ambayo unaweza ukayapata kwa haraka sana. Mafanikio yote yanajengwa hatua kwa hatua, tena wakati mwingine kwa muda mrefu sana.
Suluhisho.
Unaposhindwa kupata matokeo ya haraka hebu kuwa mvumilivu. Kwa bahati mbaya sana wengi ambao huwa wana haraka, kufanikiwa kwao huwa kugumu sana. Hebu vumilia ili ujenge mafanikio ya kudumu kwenye maisha yako.
3. Kukosa nidhamu.
Mafanikio yoyote yale yanahitaji nidhamu ili uweze kuyafikia. Wengi huwa ni watu wa kushindwa kufikia malengo yao kwa sababu ya kukosa nidhamu. Moja ya nidhamu inayokosekana na kupelekea kukata tamaa mapema ni nidhamu ya kutenda kwa bidii na kwa nguvu sana kwa kile unachokifanya.
Ipo haja kubwa sana ya kuendeleza nidhamu ya kufanya kile unachokifanya hata kama unaona hakikuletei matokeo chanya. Kama utakosa nidhamu ya kufanya kwa bidii, kwa juhudi kubwa na kujituma ni wazi kabisa huwezi kufanikiwa kwenye maisha.
Suluhisho.
“Ni muhimu kujitengenezea nidhamu kubwa ya mafanikio ili ikusaidie kukufikisha kwenye kilele cha mafanikio”.
4. Kuchukua ushauri mbovu.
Kati ya kitu ambacho huwa kinaonekana ni chepesi kupatikana ni ushauri. Pamoja na wepesi huo wa ushauri kupatikana, lakini kwa bahati mbaya ushauri mwingi huwa ni mbovu. Wengi wanaotoa ushauri huo huwa si wataalamu wa kile wanachokifanya.
Sasa inapotokea ukapewa ushauri mbovu na ukaufanyia kazi ni rahisi sana kukupoteza na kukufanya ukate tamaa kabisa juu ya ndoto zako. Ukiangalia kuna wakati wengi wamekatisha ndoto zao kwa sababu ya aina fulani ya ushauri ambao walipewa na kwa sasa umewapoteza.
Suluhisho.
“Jifunze kuchukua ushauri bora. Acha kubeba tu ushauri kwa kila mtu, hiyo itakuwa sio njia salama sana na sahihi kwako kama kila ushauri utaamua kuuchukua. Kumbuka ukipewa ushauri wa kitaalamu utafanikiwa”
Kabla sijaweka kalamu yangu chini, naomba uzingatie kwamba, kama huamini tena utafanikiwa, unataka matokeo ya haraka, umekosa nidhamu na unachukua ushauri mbovu kwa watu usiokusaidia, elewa hayo ndiyo baadhi ya mambo yanaweza kukufanya ukakata tamaa kwenye ndoto zako.
Chukua hatua za kubadili maisha yako na kwa makala nyingine za mafanikio tembelea DIRAYA MAFANIKIO kuweza kujifunza zaidi.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

www.amkamtanzania.com