Kuna falsafa muhimu sana ya maisha ambayo ipo nyuma ya kujitesa. Ni falsafa ambayo inatujengea ukakamavu wa kuweza kuendana na hali yoyote tunayokutana nayo kwenye maisha. Pia inatufanya tuweze kushukuru kwa kila tunachopata kwenye maisha yetu.
Kujitesa ni nini?
Kujitesa, japo siyo neno sahihi, ni pale ambapo unachagua kukosa kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kukipata. Kwa mfano unachagua kutokula siyo kwa sababu huna uwezo wa kupata chakula, bali unachagua kutokula. Chakula unacho lakini unaamua kukaa na njaa.
Au una uwezo wa kupata vitu vya starehe lakini unachagua kutokupata vitu hivyo. Tunasema neno kujitesa kwa sababu mara nyingi tumekuwa tunaendekeza miili yetu. Hivyo tunapojikosesha vitu hivi, tunaona tunaitesa miili yetu.
Ni zipi faida za kujitesa?
- Unajiandaa kwa nyakati ngumu.
Unapochagua kukosa kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kukipata, unakuwa na maandalizi mazuri kiasi kwamba kama itatokea ukawa huwezi kupata, basi maisha yako yanaendelea kama kawaida. Inakuwa siyo ugeni kwako kwa sababu ulishaweza kuishi bila ya vile vitu ulivyozoea kwenye maisha.
- Unathamini vitu.
Binadamu tuna tabia moja, huwa tunazoea vitu ambavyo tunavyo, na hivyo hatuvithamini sana. Mtu anakuwa na shauku kubwa ya kitu, lakini akishakipata anakizoea na hivyo kuona ni kawaida. Unapoweka utaratibu wa kujikosesha vile vitu unavyoweza kupata, unaanza kuvithamini. Kwa mfano kama umezoea kupata chakula bora kila siku, ukifunga, wakati unakuja kula, kwa njaa unayokuwa nayo, hutachagua chakula. Unapokuwa na njaa kila chakula ni kitamu.
- Unajiimarisha kiimani pamoja na kuwa mtu wa shukrani.
Unapofanya zoezi la kujikosesha kile ambacho umezoea kupata, unakuwa mtu wa shukrani. Unapokosa kitu ukikipata lazima ushukuru. Pia inakuimarisha kiimani, kama unaweza kuchagua kupata kitu ambacho unaweza kukipata, unajijengea nidhamu na utaweza kuepuka vishawishi vingi kwenye maisha yako.
Hatua gani uchukue?
Mara moja moja, jifunze kuishi bila ya vile vitu ambavyo umezoea kuishi navyo. Chagua kufunga kula, au kula vyakula ambavyo unavidharau. Labda kula ugali na maharage pekee kwa siku nzima. Au kutembea kwa miguu sehemu ambayo umezoea kutumia gari. Chagua chochote ambacho umeshakizoea kuwa nacho au kupata kwenye maisha, halafu chagua kutokukipata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK