Uchumi wa nchi yoyote inayoendelea au iliyoendelea unabebwa sana na biashara ndogo. Biashara ndogo ndiyo zinatoa ajira kwa wengi waliokosa ajira na pia zinawaongezea kipato wale ambao kipato cha ajira hakiwatoshi.

Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa biashara ndogo, bado ndiyo zinakumbwa na changamoto kubwa katika uendeshaji na ukuaji. Wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa watumwa wa biashara zao, zinawategemea moja kwa moja na bado hawawezi kuzikuza.
Mwandishi Michael Gerber anatufundisha kanuni kumi za kusimamia kwenye biashara ndogo ili iweze kuwa na mafanikio makubwa. Katika kitabu chake cha THE MOST SUCCESSFUL SMALL BUSINESS IN THE WORLD, THE TEN PRINCIPLES, Michael anatushirikisha dhana ya mara 10,000. Kwamba biashara yoyote ndogo inaweza kukua zaidi ya mara elfu kumi ya ilipo sasa.

Je ungependa biashara yako ndogo iwe na mafanikio makubwa sana? Ungependa biashara yako ndogo ikue zaidi ya mara elfu 10 ya ilivyo sasa? Kama majibu yako ni ndiyo karibu tujifunze kanuni kumi za kuzingatia kwenye kuendesha biashara ndogo ili ziwe kubwa na zenye mafanikio.

KANUNI YA KWANZA; Biashara ndogo, ikijengwa vizuri inaweza kukua mara 10,000 zaidi ya ilivyo sasa.

1. Mafanikio ya biashara yoyote yanaanzia kwenye msingi ambapo biashara hiyo imejengwa. Kama biashara itajengwa kwenye misingi sahihi basi itaweza kukua na kuleta mafanikio. Wewe kama mfanyabiashara unahitaji kuweka misingi sahihi ya biashara yako, usichukulie kama ni kitu unajaribu, bali chukulia kama kitu cha kukujengea uhuru wako.

 

2. Makosa makubwa ambayo yanazuia watu wanaoanzisha biashara kuzikuza ni pale wanapogeuza biashara zao kuwa kazi. Wanachofanya ni kuanzisha biashara na wao ndiyo wanaofanya kila kitu, wanakazana kufanya na kukosa muda wa kufikiria zaidi ya biashara waliyonayo sasa. Usiigeuze biashara yako kuwa kazi, bali igeuze kuwa mashine ya kuzalisha kazi.

3. Ili kuijenga biashara yako kwenye msingi sahihi, na ili uweze kuikuza, basi anza kufikiria mara 10,000. Fikiria biashara yako mara elfu kumi ya ilivyo sasa. Kama ni duka fikiria una maduka elfu kumi, kama ni nyumba fikiria una nyumba elfu kumi. Biashara yoyote, ifikirie kwa kiwango cha mara elfu kumi ya hapo ulipo sasa. Ukishafikiria hivi sasa jiulize unawezaje kufika hapo.

SOMA; Namna Unavyoweza Kukuza Biashara Yako Hadi Kufikia Utajiri.

KANUNI YA PILI; Biashara ndogo haiwezi kuwa bora zaidi ya wazo la biashara hiyo.

4. Kama wazo pekee la biashara yako ni kufanya kazi na kupata fedha, basi hapo ndipo biashara yako itakapoishia, kila siku utapata kazi ya kufanya na kupata kipato cha kukutosheleza pale ulipo. Biashara haiwezi kukua zaidi ya hapo. Ili biashara ikue zaidi, ni lazima mawazo yako yawe zaidi ya kupata kazi na kuingiza kipato.

5. Tengeneza biashara ya kipekee kwa kuja na wazo la biashara linaloendana na wewe, na linaloweza kukua zaidi ya kuwa tu biashara ndogo. Kwa biashara yoyote unayofikiria kufanya, fikiria unawezaje kuikuza zaidi, unawezaje kufia mbali zaidi ya kufanya kazi na kulipwa kila siku. Wazo lako la biashara ndiyo litaiwezesha biashara kukua au kubaki kuwa ndogo milele.

6. Unapofikiria kuingia kwenye biashara, unapoifikiria biashara yako, basi pata taswira ya biashara kubwa. Hata kama unaanza na duka moja, fikiria kuwa na maduka mengi ziadi, au kuwa na duka kubwa zaidi. Ona ukiwa na watu wa kukusaidia kwenye biashara yako na siyo wewe peke yako kwa miaka yote.

SOMA; Mambo 20 niliyojifunza kutoka kitabu cha The Innovator’s Dilemma

KANUNI YA TATU; Biashara ndogo ni mfumo ambao vipande vyote vinachangia kufanikiwa au kushindwa.

7. Hakuna biashara ambayo inafanikiwa au kushindwa kwa sababu ya kitu kimoja. Biashara yoyote ni mfumo kamili wenye vipande ambavyo vinategemeana. Vipande hivi ndiyo vinafanya biashara ifanikiwe au ishindwe.

8. Biashara yoyote ina vipande vya ndani na vipande vya nje.
Vipande vya ndani ni mikakati ya kibiashara, uongozi wa biashara na mpango wa ukuaji.
Vipande vya nje ni wateja, washindani, fedha na mawasiliano.
Vipande hivi vinapokuwa vizuri, kwa pamoja vinajenga biashara yenye mafanikio. Kama kuna ambacho kitapuuzwa basi biashara itakufa na kushindwa.

9. Biashara yenye mafanikio ila ulinganifu wa vipande vyote muhimu vya biashara, na ulinganifu unaleta usawa kwenye biashara na usawa unaleta msimamo wa biashara hiyo.

KANUNI YA NNE; Biashara ndogo ni lazima iwe endelevu katika nyakati zote za kiuchumi, kwenye soko lolote na itoe thamani kwa wateja wake.

10. Biashara yako ili iweze kukua nakufikia dhana ya mara 10,000 ni lazima iweze kudumu na kuwa endelevu katika nyakati zote za kiuchumi, uchumi ukiwa mbaya au ukiwa mzuri, lazima biashara yako iweze kuwa endelevu. Pia biashara hiyo iwe inawezekana kufanyika popote, iweze kumudu soko lolote na muhimu zaidi iwe inatoa thamani kwa wateja wake.

SOMA; Kanuni Sita (6) Muhimu Za Kuzingatia Ili Uweze Kuwa Mjasiriamali Bora Na Mwenye Mafanikio.

11. unapoijenga biashara yako, mara zote mfikirie mteja wako. Na hapa kuna maswali muhimu sana ya kujiuliza kuhusu mteja wa biashara yako. Yuko wapi, ana changamoto gani, atanunua kwako mara ngapi, na faida kiasi gani utatengeneza kupitia kila mteja.

KANUNI YA TANO; Biashara ndogo ni shule ambapo kila mfanyakazi ni mwanafunzi mwenye lengo la kukua.

12. Ukuaji wa biashara yako, unategemea ukuaji wako binafsi na ukuaji wa wafanyakazi wako. Wewe mwenyewe na wafanyakazi wako mtakua kama mtakuwa tayari kujifunza. Hivyo ni muhimu mno wewe ujifunze na pia uwafundishe wafanyakazi wao na wao wenyewe pia wajifunze. Kama hamjifunzi, biashara haiwezi kukua.

13. Wafanyabiashara wengi wanapoingia kwenye biashara zao, hutingwa na kukosa muda wa kujifunza. Wengine huona kujifunza siyo muhimu kwao kama kufanya kazi na kuingiza kipato, hii imekuwa inawakosesha fursa za kukua zaidi.

14. Moja ya somo unalotakiwa kulijua na kuwafundisha wafanyakazi wa biashara yako ni nadharia ya kazi sahihi. Ni lazima kila mfanyakazi wa biashara yako ajue ipi ni kazi sahihi kwenye biashara yako. Hii ni kwa sababu muda ni changamoto na mambo ya kufanya ni mengi. Lazima muweze kuweka vipaumbele na kufanya yale ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa biashara. Kwa sababu siyo kila kazi inaweza kukuza biashara yako.

KANUNI YA SITA; Biashara ndogo lazima iwe na kusudi na maono makubwa.

15. Ukuaji wa biashara yoyote utategemea kusudi la kuanzishwa kwa biashara hiyo. Hivyo biashara yenye kusudi kubwa na maono makubwa itakua kuliko ile ambayo haina maono makubwa. Kuwa na maono makubwa kuhusu biashara yako na yaishi kila siku.

16. Moja ya kusudi la biashara inapaswa kuwa kutatua changamoto za watu. Japokuwa faida ni sehemu muhimu, biashara haiwezi kukua kama hakuna changamoto na matatizo ya watu inatatua. Hivyo usifikirie faida pekee, bali fikiria ile maana ambayo biashara yako inatengeneza kwa wengine.

KANUNI YA SABA; Biashara ndogo ni tunda la kusudi kubwa la yule anayeianzisha.

17. Biashara yako ni zao la mawazo yako, mtazamo wako na maono ya maisha yako. Huwezi kuwa na maono madogo ukaweza kuwa na biashara kubwa. Kama unaona biashara yako haikui, hebu anza kujiangalia wewe mwenyewe, ni maono gani makubwa unayo kwenye maisha yako.

18. Kila mtu ana kitu cha kipekee ambacho kipo ndani yake. Mtu akijua na kuweza kutumia kitu hiki ataweza kutoa mchango mkubwa kwenye jamii inayomzunguka. Kama unataka kujenga biashara kubwa na yenye mafanikio, jua kwanza ule upekee ulipo ndani yako. Kisha utumie kuanzisha na kukuza biashara yako.

KANUNI YA NANE; Biashara ndogo ina maisha yake yenyewe.

19. Biashara ni kitu ambacho kinajitegemea chenyewe, wewe kama mwanzilishi unaipa fursa ya kukua na kutoa mchango kwa wengine. Ichukulie biashara kama kitu kilichokamilika na kinachohitaji kusaidiwa ili kukua zaidi. Kwa dhana hii utaweza kukuza biashara yako.

20. Kisheria, kampuni ambayo inatambulika kama kitu kinachojitegemea, ndiyo maana inapofilisika mmiliki hahusiki kufilisiwa. Hivi ndivyo unavyopaswa kuifikiria biashara yako, itenganishe na wewe, usiifanye kuwa wewe, bali ifanye kuwa biashara unayoweza kujiendesha yenyewe, na hapo ndipo unaweza kupata uhuru wa kweli.

KANUNI YA TISA; Biashara ndogo ni chombo cha kiuchumi, kinachoendesha uchumi na kuimarisha uchumi wa jamii husika.

21. Dhana moja unayopaswa kujua kuhusu biashara ni kwamba biashara inajenga uchumi, na siyo kwamba uchumi unajenga biashara. Hapa ndipo wengi wanaposhindwa kuelewa na hivyo kuruhusu biashara zao kufa pale uchumi unapobadilika. Katika nyakati ngumu za uchumi ndiyo biashara yako inapaswa kukua kwa sababu inachochea uchumi kukua. Hapa ndipo unahitaji kutoa thamani kwa wengine ili waweze kutoka kwenye hali ngumu ya kiuchumi.

22. Fedha ndiyo sehemu rahisi ya biashara. Watu wengi wamekuwa wakifikiria inapokuja swala la fedha, basi ndipo ugumu wa biashara ulipo. Lakini ukweli ni kwamba fedha ni sehemu rahisi ya biashara kama utaielewa fedha vizuri. Jua msingi wa fedha na namna inavyohusika kwenye biashara yako, na hutahangaika tena na fedha.

KANUNI YA KUMI; Biashara ndogo inatengeneza viwango ambavyo biashara nyingine zinapimwa kama zimefanikiwa au la.

23. Ili biashara yako iwe kubwa na yenye mafanikio, lazima iwe biashara ya mfano, lazima iwe biashara ya tofauti na ya kipekee, ambayo watu wataitumia kama kipimo kwa biashara nyingine, kama zimefanikiwa au la. Lazima ifike mahali kama watu wanataka kupima biashara imefanikiwa au la, basi waangalie kama inafanya kama biashara yako.

24. Unahitaji kujijengea viwango vya hali ya juu sana kwenye biashara yako, viwango ambavyo ni WORLD CLASS, viwango ambavyo havipatikani kwenye biashara nyingine yoyote. Kila siku fanyia kazi viwango hivyo na hakuna kitakachokuzuia kuwa na biashara yenye mafanikio.
Naamini umejifunza mengi kuhusu kuanzisha na kukuza biashara yako ili ikuletee mafanikio makubwa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita