Rafiki yangu mpendwa,
Kama kuna kitu kinapoteza na kuua biashara nyingi, basi ni mafanikio madogo ambayo biashara hizo zinakuwa zimepata. Mtu anaanzisha biashara, akiwa na wazo fulani, la kutoa huduma ambayo watu wanaihitaji, na watu wanapokea vizuri biashara yake, anaanza kupata faida.
Sasa yale mafanikio anayokuwa amepata mwanzo yanamchanganya, anaanza kujiona ameshajua kila kitu kuhusu biashara na ameshajua kila aina ya biashara. Hapo sasa mtu anaanza kujaribu kila aina ya biashara. Akiambiwa na hiki kinalipa kweli, anajaribu.
Muda siyo mrefu mtu anajikuta anajaribu kila kitu na biashara uliyoonesha kukua vizuri mwanzoni inashindwa.
Wakati mwingine ni bidhaa au huduma zinaongezwa kwenye biashara moja kiasi kwamba mtu anashindwa kujua yupo kwenye biashara ya aina gani.
Kwa wengine ni uongezaji wa matawi ambayo mtu hawezi hata kuyafuatilia vizuri.
Ukuaji wa biashara ni mzuri, lakini usiwe ukuaji wa kurukaruka, bali unapaswa kuwa ukuaji wenye mpangilio, ili unapokua uondoke kwenye hatari ya kuanguka zaidi.
Yapo maswali sita muhimu sana ambayo unapaswa kujiuliza na kujipa majibu kila siku kuhusu biashara yako, ili uweze kujua kama bado upo kwenye mstari, na hata kama unakua basi ukuaji wako unakuwa wa mpangilio.
Moja; NANI.
Swali la kwanza kujiuliza ni NANI ni mteja wa biashara yako. Lazima uchague kwa uhakika ni wateja gani ambao unakwenda kuwahudumia kwenye biashara yako. Unawachagua wateja kulingana na changamoto au matatizo waliyonayo. Kama huwezi kueleza sifa za mteja unayemlenga, hujui biashara gani unafanya.
Mbili; NINI.
Swali la pili ni NINI unawapa wateja wa biashara yako. Ni bidhaa au huduma gani unawapatia, ambayo inatatua matatizo au changamoto ambazo wanazo. Hapa unaona umuhimu wa kuchagua kwanza wateja ili kuwaandalia kile kinachowafaa.
Tatu; WAPI.
Swali la tatu ni wapi wateja wako wanaweza kupata kile unachotaka kuwapatia. Hivyo unahitaji kuwa na njia ya kuwafikia wateja na wateja kukufikia wewe. Biashara yako lazima iwe kwenye eneo ambalo wateja wako wapo wa kutosha. Hivyo swali la wapi unafanyia biashara hiyo ni muhimu sana.
Nne; WAKATI GANI.
Ni wakati gani sahihi kwa wateja wa biashara yako kupata kile unachouza. Je mahitaji yao yapo wakati gani. Je ni kitu ambacho wanakihitaji kila siku, kila wiki, kila mwezi au wanakihitaji mara moja kwa mwaka? Ni muhimu ujue wakati gani ambapo wateja wako wanahitaji kile unachowauzia ili uweze kuwaandalia vyema na kuhakikisha hawakosi wanachotaka.
Tano; KWA NINI.
Swali la tano unalopaswa kujiuliza kuhusu biashara yako ni kwa nini wateja wa biashara yako waje kununua kwako na siyo kwenda kwa wengine ambao wanauza kile unachouza. Kama hujidanganyi, unajua kabisa kwamba biashara unayofanya wewe, kuna wengine wengi pia wanaifanya. Sasa kwa nini wateja wawaache wengine wote na waje kwako? Lazima uwe na kitu cha tofauti ambacho kinapatikana kwako tu, kwa wengine hakipi. Hivyo unahitaji kuwa na KWA NINI kubwa unayomfanya mteja aje kwako na kuwaacha wengine.
Sita; KWA VIPI.
Ni kwa namna gani mteja anapata kile ambacho biashara yako inatoa. Ni kwa jinsi gani ananufaika na kile unachotoa. Je mteja anajua kwa hakika kila thamani ambayo ataipata kwa kile anachonunua? Pia ni vitu gani vya ziada ambavyo mteja anapata baada ya kununua? Hapa unahitaji kuwa na njia ya kufanya manunuzi ya mteja kuwa rahisi na aweze kunufaika na kile alichonunua.
Jiulize maswali haya kila siku kwenye biashara yako, usijiambie unaijua biashara yako, jiulize maswali hayo na utashangaa ni kwa jinsi gani huijui biashara yako vizuri. Pia unaweza kushangaa ulishaachana na biashara yako zamani sana na sasa unahangaika na vitu vingine.
Hatua ya kwanza ya mafanikio kwenye biashara yako ni kuijua biashara yako vizuri kisha kuwa na msimamo kwenye kuiendesha na kuikuza biashara hiyo kwa mpangilio mzuri, na siyo kukimbilia kufanya kila unachoona unaweza kufanya.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL