Kuna mwanamuziki amewahi kuimba kwamba dunia haina huruma. Naweza kukubaliana naye kwa upande mmoja, na nisikubaliane naye kwa upande mwingine.

Nitakubaliana naye kwamba dunia haina huruma, kama tutaiangalia dunia kwa upande wetu sisi. Kwa sababu tunapenda kujiona kwamba dunia ina wajibu kwetu. Kwamba dunia inapaswa kufanya kile ambacho sisi tunataka ifanye. Kuna wakati tunataka dunia isimame kabisa kwa sababu ya matatizo yetu. Sasa pale dunia inapokwenda tofauti na mategemeo yetu, tunasema dunia haina huruma.

Sitakubaliana naye kama tutaiangalia dunia kwa upande wa dunia. Hebu weka hisia zako pembeni, na iangalie dunia, jiwe kubwa ambalo linazunguka jua, na wakati huo huo linajizungusha lenyewe kwenye mhimili wake. Hebu fikiria jiwe hili linafikiria nini kuhusu wewe? Hakuna. Jiwe hili ambalo tunasema ni dunia, halijali kama wewe upo au haupo, dunia haitaacha kuzunguka kwa sababu wewe una matatizo yako binafsi, dunia itaendelea kuzunguka, jua litaendelea kuchomoza na kuzama kila siku. majira yatakuja na majira yatapita, kila siku, bila ya kujali wewe unapitia hali gani.

Tunajifunza nini hapa?

  1. Tunachojifunza ni kwamba dunia kama dunia ipo, haijali kuhusu wewe inaendelea kuwepo, iwe wewe upo au haupo.
  2. Huidai dunia chochote, dunia haina wajibu wowote kwako, umekuja ukaikuta dunia, hivyo huwezi kusema kama dunia inapaswa kukufanyia wewe kitu.
  3. Ili kwenda vizuri na dunia, fuata sheria za asili, dunia inafuata sheria za asili, na wewe ukizifuata sheria hizi, utakwenda sawa na dunia. Sheria za asili ndizo zinawezesha viumbe wote kwenda sawa hapa duniani. Mfano unavuna ulichopanda, hii ina maana kwamba kabla hujavuna lazima upande, sasa utakapotaka kuvuna kabla hujapanda, unatengeneza matatizo makubwa na dunia lazima ikuadhibu.

Hitimisho.

Siyo kwamba dunia haina huruma, bali dunia haijali kuhusu wewe, kwanza haijui hata upo. Hivyo ni wajibu wako kwenda sawa na dunia, na siyo kutaka dunia iende sawa na wewe. Badala ya kulalamika kwamba dunia haina huruma, hebu angalia ni hatua gani unazoweza kuchukua ili maisha yako yawe bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK