Moja ya vitu ambavyo kila mfanyabiashara anapaswa kujifunza , ni tabia za binadamu. Hii ni kwa sababu mahusiano ya kibiashara, kati ya mfanyabiashara na mteja wake, yanategemea sana uelewa ambao mfanyabiashara anao juu ya tabia za asili za binadamu. Na kama unavyojua, biashara za zama hizi ni biashara za mahusiano, mtu hanunui kwako kwa sababu unauza, ila ananunua kwako kwa sababu anakujua wewe na biashara yako.
 

KUPATA TIKETI YA SEMINA PIGA SIMU 0717396253/0755953887


Leo nataka nikushirikishe tabia moja ya asili ya binadamu ambayo unaweza kuitumia kunufaika kibiashara. Kwa kujua tabia hii na kuitumia vizuri, utaweza kuikuza biashara yako mara dufu na kupata wateja wengi watakaodumu kwenye biashara yako.  Kabla hatujaanza kuangalia tabia hii, niseme wazi kwamba tabia utakayoenda kujifunza hapa siyo ya kuwalaghai watu, bali kuwapa watu kile wanachotaka na wao wanakupa unachotaka.

Sheria moja ya dunia ni nipe nikupe, yaani watu ni rahisi sana kutoa pale ambapo unakuwa umeshawapa. Hii nayo ni tabia nyingine muhimu ambayo inaendana sana na ile tutakayojifunza leo. Lakini hii hatutaijadili kwa kina, tutafanya hivyo kwenye makala zijazo.

SOMA; Tabia Nne(4) zinazowatofautisha wafanyabiashara wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Kuna tabia moja ya asili ya binadamu ambayo kila mfanyabiashara anatakiwa kuijua na kuweza kuitumia vizuri. Tabia hii ni UBINAFSI. Kila binadamu ni mbinafsi, ndiyo namaanisha hata wewe na mimi ni wabinafsi. Tunachotofautiana ni viwango vya kuonesha ubinafsi wetu. Lakini mara zote huwa tunajifikiria sisi. Na ubinafsi siyo jambo baya, kwa sababu ndiyo unatuwezesha kujijali na hatimaye kuweza kuishi. Tatizo ni pale ubinafsi wako unapoingilia maslahi ya wengine, ndipo matatizo huanza.

Sasa turudi kwenye matumizi ya ubinafsi wa watu kwenye biashara yako. Iko hivi, kila mtu anapenda kupata vitu bora kwa kutumia fedha kidogo. Ndiyo maana mara nyingi watu wanapopewa bei, huwa wanataka kupata punguzo. Ukipewa vitu viwili vyenye ubora sawa, kimoja kikawa ghali, na kingine kikawa rahisi, utachukua kile cha bei rahisi. Au kama unapewa mikate miwili kwa bei sawa, ila mmoja ni mkubwa na mwingine ni mdogo, utachukua ule mkubwa, labda kama mdogo una vitu vya ziada.
Unaona sasa rafiki, tunapenda kujipendelea, tunapenda kupata kilicho bora kwa gharama kidogo. Tunapenda kupata zaidi ya tunavyopata.

Je unawezaje kutumia tabia hii ya ubinafsi wa watu kunufaika kibiashara?

Kwanza tuangalie njia ambayo siyo sahihi kutumia njia hii.
Kuna wafanyabiashara wengi ambao wamekuwa wanatumia tabia hii, iwe kwa kujua au kwa kutokujua, ila wanaitumia kimakosa na inawagharimu baadaye. Wanachokifanya wafanyabiashara hawa ni kuweka bei kubwa ya vitu vyao kuliko uhalisia, ili mtu anapoomba kupunguziwa, basi wakipunguza ifike kwenye ile bei ambayo ni halisi.

Huku ni kudanganya na hakuna kitu ambacho watu hawapendi kama kudanganywa. Kadiri unavyofanya hivi watu watajenga tabia ya tofauti ambayo haitakuwa nzuri kwa biashara yako. Watajizoesha kwamba kila kitu kwako kinauzwa kwa bei ambayo siyo halisi, hivyo yule anayeweza kupambana akapunguziwa basi ndiyo anafaidi.

SOMA; Wazo Bora Na Mtaji Pekee Havitoshi Kuifanya Biashara Ifanikiwe, Unahitaji Kitu Hiki Kimoja Muhimu Sana Kwa Mafanikio Ya Biashara Yako.

Wakati mwingine inajenga picha mbaya kabisa, kwa mfano mtu mmoja kanunua kitu kwako, na yeye hakujua kama unapunguza bei, hivyo ulipomwambia bei yeye akalipa na kupata alichotaka. Sasa atakaposikia mwingine kanunua kwa bei ya chini kuliko yeye, ataona umemwibia fedha. Mteja kama huyu anaweza sirudi tena kwenye biashara yako. Na kama atarudi basi hatakuwa na imani kwako.

Njia sahihi ya kutumia tabia hii.
Ipo njia sahihi ya kutumia tabia hii ya ubinafsi ambayo kila mmoja wetu anayo. Njia hii ni kutoa thamani kubwa sana kuliko fedha ambayo mtu analipa. Hapa mtu lazima atakuja kwako na ataendelea kuwa mteja mzuri kama kweli atapata thamani hiyo mara zote.

Unachofanya ni kutoa thamani kubwa sana kwa bei ambayo haiendani na thamani hiyo, kiasi kwamba mteja anaona kama anakuibia hivi. Unatoa thamani ambayo mteja hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote, hii inamfanya akutegemee wewe na awe mteja wako wa kudumu. Kwa kutoa thamani kubwa, mteja atakuja yeye na pia atawaambia wengine. Tabia nyingine ya binadamu ni kwamba kizuri hawawezi kula wenyewe, hivyo watawaambia na wengine pia.

Kitu muhimu nataka ujue ni kwamba kutoa thamani kubwa haimaanishi uuze vitu kwa bei rahisi, unaweza kuuza bei ile ile ambayo imezoeleka lakini unaongeza thamani kubwa mno. Au wakati mwingine hata ukauza kwa bei ya juu lakini bado thamani ikawa kubwa sana kiasi kwamba watu wakawa tayari kulipia thamani hiyo.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

Njia hii ya kuongeza thamani inafaa sana kwa wale ambao wanatoa huduma au wanatengeneza bidhaa zao wenyewe. Lakini pia inawafaa mno wale wanaofanya biashara ya rejareja. Japokuwa kwenye biashara ya reja reja bidhaa ni ile ile na bei ni zile zile, bado unaweza kuongeza thamani kubwa kwa namna unavyowauzia wateja wako bidhaa zile. Kauli zako kwa wateja wako zinaweza kuwafanya wajisikie vizuri na wapende kuja kwenye biashara yako mara zote. Wewe mwenyewe unajua, kuna biashara ukienda unajisikia vizuri na nyingine unajisikia vibaya jinsi unavyopokelewa na kuhudumiwa. Sasa wewe wafanye wateja wako wajisikie vizuri kuwa kwenye biashara yako.

Ni asili ya binadamu kuwa wabinafsi, tunapenda kupata zaidi kwa kutoa kidogo. Angalia biashara yako, ona ni namna gani unaweza kuwapa wateja thamani zaidi na wao watakuwa tayari kununua kutoka kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK