Ni vigumu sana kujua sababu halisi ya watu kufanya kile wanachokifanya, kwa sababu mara nyingi hawatakueleza sababu halisi, hasa kama itakuumiza.
Kuna mtu anaweza kugombana na wewe, anaweza kukukasirikia na hata kukujibu vibaya. Anaweza kukupa sababu ya yeye kufanya hivyo, lakini mara nyingi hiyo siyo sababu halisi. Huwa kunakuwa na sababu kubwa ndani yake, ambayo wakati mwingine hata haikuhusu wewe. Labda ana changamoto nyingine za maisha yake, ila anachukulia nafasi uliyompa kutoa hasira zake kupitia wewe.
Kama unafanya biashara, unaweza kumweleza mteja vizuri kuhusu biashara yako na namna inavyoweza kumsaidia. Akakusikiliza lakini mwisho akakuambia hawezi kununua. Anaweza kukupa sababu labda hana fedha au tayari anacho kile unataka kumuuzia. Lakini mara nyingi hii siyo sababu halisi, huwa kuna sababu nyingine iliyopo ndani yake ambayo anaweza asiwe tayari kukuambia. Labda unachotaka kumuuzia hakina ubora anaotaka, au hana uhakika kama kwa kulipia unachouza atapata kama anavyotaka.
Kuna mengi ambayo watu wanakuwa nayo ndani yao, lakini hawakuambii kwa sababu mbalimbali.
Je unafanya nini kujua sababu halisi?
Kwa sababu watu hawapo tayari kujua sababu halisi, ipo njia unayoweza kuipata sababu halisi ya watu kufanya ua kutokufanya kitu. Njia hii ni kusikiliza kwa makini na kuuliza maswali.
Ninaposema kusikiliza kwa makini, siyo tu kutega masikio yako na kusikia, lakini pia kuangalia lugha za alama ambazo mtu anatoa, kujua hofu ambayo ipo ndani yake na pia kupata mtazamo wa mtu juu ya jambo husika.
Sikiliza kwa makini na uliza maswali, uliza maswali ambayo yatamfanya mtu afunguke na kukupa sababu halisi bila ya yeye kujua kama anakupa sababu aliyokuwa ameficha.
Kwa mfano kama mteja amesema hawezi kununua kile unamuuzia, mwulize ungefanya nini ndiyo angeweza kununua, mara moja atajisahau na kutoa sababu aliyokuwa anaificha.
Kadri unavyoongea na mtu kwa muda mrefu, utazidi kujifunza na kujua kwa hakika ni sababu zipi zinampelekea yeye kufanya au kutokufanya kitu fulani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK