Kupanga ni hatua moja, kufanyia kazi mipango yako ni hatua nyingine, ambayo ni ngumu na ina changamoto zake.
Kila mmoja wetu amekuwa anapanga mambo mbalimbali kwenye maisha yake, tumepanga mengi kulingana na malengo yetu kwenye maisha.
Lakini mpaka sasa tumeshajifunza kitu kikubwa, siyo kila tunachopanga kinatokea kama tulivyopanga. Mara nyingi mipango yetu na yale yanayokuja kutokea huwa tofauti kabisa.
Je tuache kupanga kwa sababu tunapata matokeo tofauti na tulivyopanga?
Jibu ni hapana, lazima tuendelee kupanga kwa sababu ni mipango yetu ambayo inatuonesha vipaumbele vyetu ni vipi na hatua za kuchukua ni zipi.
Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye mipango yetu.
1. Tupange tukijua siyo kila kitu kitakwenda kwa asilimia 100, kuna vitu vitakuwa tofauti a tutakavyopanga.
2. Tuongeze zaidi ya tulichopanga, kama ni muda basi ongeza zaidi na kama ni fedha basi hakikisha unatenga nyingi kuliko ulivyopanga. Mara nyingi vitu huzidi mipango iliyowekwa, unapojiandaa kwa kutenga zaidi ya ulichopanga, hutakwama njiani.
3. Jua mipango yako siyo torati. Mipango siyo kitu ambacho hakiwezi kubadilishwa, badala yake kuwa tayari kubadilika pale mazingira yanapokutaka ubadilike. Kuendelea kung’ang’ana na mipango yako hata kama hali hairuhusu ni kujiandaa kushindwa.
4. Fanya mapitio ya mipango yako mara kwa mara. Ukishaanga usitupe mipango hiyo na kuanza kufanya, unaweza kujikuta unafanya mambo ambayo yapo tofauti kabisa na mipango yako. Pitia mipango yako mara kwa mara, ili kuhakikisha upo kwenye njia sahihi.
5. Kuliko upange halafu usifanye, ni bora uanze kufanya halafu uje kupanga baadaye. Kuna watu ambao wamekuwa mabingwa wa kupanga, wanapanga kila mara lakini hawaanzi kufanya kile wanachopanga. Kama kupanga ndiyo kunakutisha, ni bora uanze kufanya, halafu upange baadaye.
Mipango siyo matumizi, lakini ni lazima upange.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK