Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawachanganya watu wengi, ni kutokuijua misingi, kutokuzijua kanuni. Hii inawapoteza wengi na kushindwa kupata kile ambacho wanakitaka.
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, mahali popote unapotaka kufika, unahitaji kwanza kuijua misingi, kuzijua kanuni na kisha kuzifuata na kuzisimamia.
Watu wengi wamekuwa wanashindwa kwa sababu hawajui misingi na hivyo hawaifuati na kuisimamia. Badala yake wanawafuata watu. Badala ya kufuata misingi, wanafuata watu. Na kama wote tunavyojua, binadamu ni viumbe ambao tunakosea. Kama unachagua kumfuata mtu, maana yake utalazimika kufuata makosa yake kwa kujua au kutokujua. Hii itakugharimu sana kwa sababu sasa utakuwa na makosa ya aina mbili unayofanya, makosa yako mwenyewe na makosa ya yule ambaye unamfuata.
Kuepuka kuwa na makosa hayo mengi, ambayo yanakurudisha nyuma, ijue misingi na kuisimamia.
Iwe upo kwenye ajira, jua misingi na kanuni za ajira yako, jua kila unachopaswa kufanya na njia za kufuata ili kukamilisha kazi zako. Fuata misingi hii, utafanya kazi zako vizuri kuliko kuacha misingi na kufuata wengine.
Hata kama upo kwenye biashara yako mwenyewe, ijue misingi ya biashara yako, zijue kanuni za kibiashara, na zifuate hizo. Usiangalie wengine wanafanya nini na kuchukua hiyo kama sheria. Hata kama kila mtu anafanya, kama ni kinyume na kanuni usifanye.
Mwisho kabisa kwenye swala la mafanikio, ipo misingi ya mafanikio, zipo kanuni za mafanikio. Zifuje hizo na zisimamie popote unapokuwepo na lazima utafanikiwa. Usiishie tu kuwaangalia wengine waliofanikiwa ukadhani na wewe utafanikiwa, hufanikiwi kwa kuangalia watu, unafanikiwa kwa kuijua misingi na kuisimamia. Kuwaangalia wengine ni hamasa nzuri, lakini haitakufikisha pale walipo. Ijue misingi, isimamie na mafanikio yatakuwa yako.
Popote ulipo, jiulize misingi ni ipi, kanuni za mafanikio ni zipi, kisha zifuate na kuzisimamia kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK