Habari rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi ya kipekee kwetu kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa. Tutumie muda wetu wa leo vizuri rafiki, kwa sababu hatutakuja kuupata tena.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUCHELEWA….
Kwenye maisha kuna wakati unajiona kama umechelewa.
Labda umekuwa unafanya mambo yako kwa mazoea na baadaye unakuja kugundua ya kwamba unaweza kufanya kwa ubora zaidi.
Au labda ni wenzako ambao mlianza pamoja, lakini wao wamefika mbali kuliko wewe.
Hapa unaweza kujiona umechelewa sana, lakini ukweli ni kwamba hujachelewa.
Kwenye safari ya mafanikio, kwenye kuyaishi maisha yako, hakuna kichelewa, badala yake kuna kujifunza na kuwa bora zaidi kila siku.
Pale unapoanza kupata hisia kwamba umechelewa, jua upo sehemu sahihi, kwa sababu kupata hisia hizo ni kiashiria kwamba unataka kwenda mbali zaidi.
Unachelewa pale ambapo umepotea na hujui kama umepotea. Pale ambapo unafanya mambo kwa kukosea lakini wewe unaona upo sahihi kabisa. Hapa ndipo unapokuwa umeejichelewesha wewe mwenyewe.
Kujua kwamba unakosea na kujirekebisha,
Kuona kama umeshachelewa na kuchukua hatua bora zaidi, ni nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Hivyo hujachelewa kama unajua umechelewa, bali umechelewa kama hujui umechelewa. Na kama unajua umechelewa lakini huchukui hatua, hapo sasa umeamua kujichelewesha.
Kama kuna kitu hakipo sawa kwenye maisha yako, chukua hatua sasa. Kesho utajishukuru kwa hatua ulizochukua leo na hutaona kama umechelewa. Ila kama leo itapita bila kuchukua hatua, kesho utakuwa umechelewa.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info